Imani ndio kiungo kikuu cha akili. Pale imani inapochanganywa na mawazo yenye hamasa, akili inachukua mawazo hayo na kuyafanyia kazi. Kwa njia hii inakuwezesha wewe kufikia kile unachotaka.

Hisia za IMANI, UPENDO na MAPENZI ni hisia zenye nguvu kubwa sana kwa binadamu. Hisia hizo tatu zinapochanganywa pamoja, zinamwezesha mtu kuweza kufikia uwezo mkubwa sana uliopo ndani yake. IMANI na UPENDO ni hali ya mawazo na ipo kiroho zaidi. MAPENZI ni hali ya kimwili. Hivyo kuchanganya hisia hizo tatu inakuwezesha kuunganisha mwili wako na uwezo mkubwa wa akili yako.

JINSI YA KUENDELEZA IMANI.

Imani ni hali ya mawazo/akili ambayo inaweza kutengenezwa au kuingizwa kwa mawazo yanayojirudia rudia kwenye akili yako ya ndani(subconscious mind). Mawazo unayoweka kwenye akili yako kwa muda mrefu na kama ukiamini mawazo haya yanawezekana akili yako itakutengenezea mazingira ya kuwez akufikia kile unachotaka. Hapa ndipo unapoweza kutumia imani yako kujitengenezea utajiri.

Kwa hatua zile sita ulizotengeneza kwenye uchambuzi uliopita(kama hukutengeneza fanya hivyo leo) unaitengenezea akili yako mawazo ya kukutengenezea wewe mazingira ya kuweza kupata fedha nyingi na kuweza kufikia utajiri.

Unaweza kujitengenezea imani kwa kuipa akili yako masharti kupitia kauli ambazo utakuwa unajiambia kila siku. Kama umeshatengeneza kauli yako ya kujiambia, kwa kusema kauli hiyo kila siku ni njia moja wapo ya kuanza kujijengea imani.

Kitu ambacho kinarudiwa kila mara kinakuwa kweli. Chukua mfano wa mtu anakuwaje mhalifu. Mtu anapokutana na uhalifu kwa mara ya kwanza anaupinga na kuukataa. Anapoendelea kuona uhalifu kila siku anaanza kuona ni kitu cha kawaida. Anapoanza kushirikiana na wahalifu na yeye anaona uhalifu ni kitu cha kawaida.

Hii ina maana kwamba mawazo ambayo yanaingia kwenye akili yako kila siku na kila mara yanakubalika na akili yako na akili inaanza kukutengenezea mazingira ya kutimiza mawazo hayo.

Mawazo yote ambayo yamechanganywa na HISIA na kuwekewa IMANI, hubadilika mara moja na kuwa uhalisia. Na mawazo yoyote ambayo yamechanganywa na hisia, iwe hisia chanya au hisia hasi hujengeka katika uhalisia. Hii ndio sababu kwa wale wanaoamini kwamba wana kisirani au bahati mbaya huendelea kukutana na hali hizo kwenye kila kitu wanachofanya. Na wale ambao wanaoamini kwamba wana bahati nzuri au wanauwezo wa kufanya mambo makubwa hufanya hivyo kwenye kila jambo wanalolifanya.

Kwa maelezo na mifano hii ni wazi kwamba akili yako ya ndani haiwezi kutofautisha ukweli na uwongo, hasi na chanya. Yenyewe inachukua mawazo yanayoingia na kuyafanyia kazi. Kama mawazo yataingizwa kwa hisia na imani yanafanyiwa kazi haraka kuleta kile kinachofikiriwa.

Kwa kuwa akili yako hiyo haina uwezo wa kutofautisha, ni rahisi sana kuidanganya ili kuweza kufikia kile unachotaka. Unaweza kuidanganya kwa kuwa na mawazo ya kile unachotaka ambayo unajiambia kila siku kwa hisia na imani na pia kufanya kama tayari umeshapata kile unachotaka. Kwa mfano unachotaka ni kuongez akipato chako, kama tulivyosema kwenye hatua zile sita, unasema kiwango unachotaka, na tarehe ya kukifikia, halafu unakuwa unajiambia kila siku kama vile tayari umeshapata fedha unayotaka. Na hata unavyoishi maisha yako ishi kama tayari umeshapata kile unachotaka. Kwa kufanya hivi subconscious mind yako inaona hayo ndio maisha yako na kuendelea kukutengenezea mazingira ya kuwa na maisha hayo.

Kumbuka imani ni chanzo muhimu cha kufikia mafanikio, ila kuwa na imani tu hakutakuletea mafanikio, ni lazima uzifanyie kazi fursa zinazojitokeza mbele yako. Ni lazima ufanye kazi kwa bidii na maarifa huku ukiamini kwamba unaweza kufikia kile unachotaka.

IMANI ni kitu ambacho kinalipa wazo lako maisha, nguvu na matendo.

IMANI ni hatua ya mwanzo ya kukusanya utajiri.

IMANI ni msingi wa miujiza na maajabu yote ambayo hayawezi kuelezewa na sayansi.

IMANI ndio kinga pekee ya KUSHINDWA.

IMANI ndio kitu ambacho kikichanganywa na maombi kinakuwezesha kufikia uwezo wako mkubwa na uwezo mkubwa wa akili.

IMANI ni kiungo muhimu kinachoweza kubadili mawazo ya kawaida kuwa kitu cha uhalisia.

Tukutane kwenye sehemu ya pili ya uchambuzi huu…