Tunaendele ana sehemu ya pili ya uchambuzi huu wa hatua ya pili ya kuelekea kwenye utajiri. Hatua hii ni imani, katika makala iliyopita tumeweza kuona jinsi imani inavyoweza kukuletea mambo makubwa.

Huu hapa ndio ukweli kuhusu imani na mafanikio;

Mawazo ambayo yamechanganywa na hisia na imani yanatengeneza nguvu ya sumaku ambayo inavuta mawazo mengine yanayofanana na mawazo hayo. Na hapo ndipo unapoweza kuzivuta fursa za kukuwezesha kufikia kile unachotaka. Unapokuwa na mawazo hasi uliyochanganya na hisia yanakuunganisha na mawazo mengine hasi na hivyo kuishia kupata matokeo hasi kama woga, umasikini, magonjwa, kushindwa, visirani. Unapokuwa na mawazo chanya yaliyochanganywa na hisia, yanakuvutia mawazo mengine chanya na hivyo vitu chanya kuweza kutokea kwenye maisha yako kama mafanikio, utajiri, afya njema.

Wazo lolote ambalo litatawala akili yako ni lazima litavuta mazingira ya kukamilisha wazo lile. Uko hivyo ulivyo na hapo ulipo kutokana na mawazo ambayo umeyaweka kwenye akili yako kwa muda mrefu. Ili uweze kubadilika unahitaji kuanza kubadili mawazo yako. Ndio maana tulitengeneza maelezo yale ambayo utakuwa unajiambia kila siku, yataondoa mawazo yote hasi na ya umasikini kwenye akili yako na kupandikiza mawazo chanya na ya utajiri.

Kama ukijichunguza vizuri kwenye uwezo wa akili yako, utagundua kwamba kitu kikubwa kinachokuzuia ushindwe kufikia malengo unayotaka ni kutokujiamini. Kutokujiamini kunaweza kukufanya hata kushindwa kuweka mawazo mazuri kwenye akili yako.

Hatua muhimu unayotakiwa kuchukua ni kujijengea kujiamini. Na utajijengea kujiamini kwa hatua sita ambazo zitaifanya akili yako ya ndani(subconscious mind) kuamini kwamba tayari wewe unacho kile unachotaka na hivyo kukutengenezea mazingira ya kuendelea kukipata.

Hatua sita za kujijengea kujiamini;

1. Najua kwamba nina uwezo mkubwa wa kufikia malengo na mipango niliyojiwekea kwenye maisha hivyo naamuru nafsi yangu iwe na uvumilivu, na kuendelea kuchukua hatua mpaka nitakapofikia ninachotaka.

2. Natambua kwamba mawazo yanayotawala akili yangu yatajitengeneza na kuwa kweli katika uhalisia hivyo kila siku nitatengeneza mawazo ninayoyataka na kuyaweka kwenye akili yangu kwa dakika 30 kwa kutengeneza picha ya kile ninachotaka.

3. Najua kwamba kujiamini ndio kutaniwezesha kufikia yote haya na hivyo kila siku kwa dakika kumi nitajijengea kujiamini.

4. Nimeshaandika lengo na dhumuni langu kubwa kwenye maisha na sitoacha kujaribu hata kama nitashindwa kiasi gani.

5. Natambua kwamba hakuna utajiri ambao unaweza kudumu kama haujajengwa kwenye misingi ya ukweli na haki, hivyo sitajihusisha na biashara ambayo haiwafaidishi wale ninaofanya nao. Nitafanikiwa kwa kuwa tayari kuwasaidia wengine na kuwa tayari kusaidiwa na wengine pia. Nitaondokana na chuki, wivu, majungu na ubinafsi kwa kuendeleza upendo kwa binadamu wote kwa sababu najua mawazo hasi juu ya wengine hayataniletea mafanikio kamwe. Nitawafanya wengine kuniamini mimi kwa sababu nitawaamini wao.

6. Naweka sahihi yangu kwenye maazimio haya sita na nitayasema kila siku kwa kuamini na kuchanganya na imani kwa sababu najua kwa kufanya hivi nitafikia mafanikio.

Kanuni hii itafanya kazi kwako kwa sababu itakwenda kukujengea msingi mpya wa mawazo wa kuona kila kitu kinawezekana. Kumbuka imani ndio nguvu kubwa sana inayotuwezesha kupata chochote tunachotaka, iwe tunajua au hatujui. Kanuni hii itakuamsha kutoka kwenye usingizi na kukuwezesha kutumia uwezo mkubwa ulipo ndani yako.

Ni kwa imani ambapo viongozi wakubwa wa dunia waliweza kuleta mabadiliko makubwa. Imani ndio itakayokuwezesha wewe kubadili maisha yako.

HAKUNA VIKWAZO ZAIDI YA VILE AMBAVYO TUMEJIWEKEA WENYEWE.

UTAJIRI NA UMASIKINI VYOTE NI ZAO LA MAWAZO.

Amua leo utatumiaje akili yako. Je utaitumia kwa kuweka mawazo ambayo yanakuletea utajiri? Au utaitumia kuweka mawazo ambayo yanakufanya uendelee kuwa masikini? Chaguo ni lako, hakuna wa kukusaidia, hakuna wa kumlaumu.