Hakuna mtu asiyependa kuwa tajiri. Na kama hupendi kutumia neno tajiri, basi hakuna mtu asiyependa kufikia uhuru wa kifedha. Uhuru wa kifedha na utajiri ni kitu kimoja. Na hii ni hali ambayo mtu anaifikia pale ambapo hana tena hofu ya hela.

Kwa kifupi tajiri au mtu mwenye uhuru wa kifedha anauhakika wa kuendelea kuishi maisha yake mazuri miaka mingi ijayo hata kama leo hii ataacha kufanya kazi. Mtu huyu hana tena hofu ndogo ndogo kwamba kesho nitaishije, au mwaka kesho nitaishije.

Hata wewe unaweza kufikia hatua hii, kama bado hujaifikia. Sio kitu rahisi ila kinawezekana kama kweli una nia ya kufikia hali hiyo.

Zifuatazo ni njia kumi za wewe kufikia utajiri.

1. Usitegemee chanzo kimoja cha mapato.

Kama chanzo chako cha kipato ni kimoja tu ni vigumu sana kufikia uhuru wa kifedha. Hii ndio maana waajiriwa wengi hawafikii uhuru wa kifedha kwa sababu wanategemea mshahara tu. Moja ya hitaji la msingi la kufikia uhuru wa kifedha ni kufanya biashara. Na kwa ulimwengu wa sasa kuingia kwenye biashara ni kitu rahisi sana.

Kwa chochote unachofanya, hakikisha pia unaingia kwenye biashara, itakuongezea vyanzo wa kipato na itakuweka kwenye nafasi nzuri ya kufikia mafanikio.

2. Wekeza faida kwenye biashara.

Tofauti ya watu wanaofanikiwa kupitia biashara na wasiofanikiwa ni moja. Wanaofanikiwa wanafanya biashara kwa ukuaji, wasiofanikiwa wanafanya biashara kwa ulaji. Kama unafanya biashara na kila ukipata faida unakula yote, jua kwamba safari ya kufikia uhuru wa kifedha umeshaachana nayo.

Endelea kuwekeza kwenye biashara yako ili iendelee kukua na kukutengenezea faidakubwa ambayo itakuwezesha kufikia uhuru wa kifedha.

3. Kuwa tayari Kuwa Tofauti.

Unataka uendeshe gari ambayo kila mtu anaendesha? Huwezi kufikia mafanikio. Unataka kufanya biashara ambayo kila mtu anafanya na kwa mtindo ambao kila mtu anatumia? Umeshaaga mashindano.

Ukweli ni kwamba jamii yetu imejaa watu ambao wanaigana na hawajui wanaelekea wapi. Kama na wewe utaungana nao, umeamua kuacha njia nzuri na kufuata njia isiyojulikana inaelekea wapi.

Kama unataka kufikia uhuru wa kifedha, kuwa tayari kuwa tofauti na wengine.

4. Usipoteze muda wako kufanya maamuzi ambayo sio ya msingi.

Kwanza usipoteze muda wako kufikiria mambo ambayo hayana mchango wowote kwenye maisha yako. Najua hapo ulipo unawaza mambo mengi ambayo hayana msaada wowote kwako kufikia uhuru wa kifedha. Ondoa mawazo haya kwenye kichwa chako na weka mawazo yatakayokuwezesha kufikia malengo yako.

Pia usipoteze muuda mwingi kwenye kufanya maamuzi, unaweza kukosa fursa nzuri kwa sababu ya kuwa taratibu.

5. Dhibiti garama ndogo ndogo.

Hakuna kitu kinachopoteza fedha kama gharama ndogo ndogo. Angalia matumizi yako na kama kuna kitu chochote ambacho sio cha msingi kiondoe. Hata kama gharama yake ni tsh 100 au 1000 kwa kudharau fedha hizi ndogo utajenga tabia ya kutokujali fedha na hivyo kujikuta unapoteza fedha nyingi.

Kuwa makini sana na kila gharama inayotumia fedha zako, maana gharama hizo ni kama matundu yanayovujisha maji kwenye pipa kubwa la maji.

6. Dhibiti kiwango chako cha ukopaji.

Mikopo ni mizuri sana hasa pale unapotumia mkopo kukuza biashara yako. Ila kama unakopa halafu unatumia fedha hiyo kula, wewe umeshaaga mashindano. Mkopo una riba, wewe unaenda kula na unajua ukishakula ndio imetoka, hiyo riba utaitoa wapi? Unajitengenezea umasikini mwenyewe.

Kwa wale wanaokopa kwa ajili ya biashara usikope tu kwa sababu mikopo inapatikana. Maana siku hizi benki zina uchu kweli, wanaweza kukufuata na kukuambia kulingana na biashara yako tunaweza kukukopesha kiasi kadhaa. Wewe unafurahia na kukopa, wale wapo pale kufanya biashara, hivyo kuwa makini kabla hujaingia kwenye mikopo maana inaweza kukurudisha nyuma. Hakikisha kabla hujachukua mkopo unajua utakapouwekeza kwenye biashara yako ili ukupatie faida ya kutosha kuulipa na wewe kukua zaidi.

7. Kuwa mvumilivu na king’ang’anizi.

Hili tumekuwa tukilitaja kwenye kila tunachojadili kuhusu mafanikio. Badala ya kuiruka kwa sababu umekuwa ukiisoma kila siku, hii ndio inayotakiwa kuwa nguzo yako ya kwanza kabisa. Kama Hutakuwa na uvumilivu utakata tamaa haraka. Na kama unataka utajiri wa haraka haraka kuna mambo mawili; moja utakufa masikini au utakufa haraka.

8. Jua wakati wa kuacha.

Kwa sababu tunasema unahitaji kuwa mvumilivu na king’ang’anizi haimaanishi utafanya hivi tu bila ya kufikiria. Kuna wakati ambapo utahitaji kufanya mabadiliko kwenye mipango yako. Ujue wakati huo na fanya mabadiliko yatakayokuwezesha kufikia uhuru wa kifedha.

9. Pima hatari.

Katika kufanya maamuzi yako, pima ni hatari kiasi gani ambayo unaweza kuingia. Na pia angalia hatari hiyo itakuwa na madhara kiasi gani ukilinganisha na faida unayopata. Watu waliofanikiwa wanafanya mamauzi ya hatari(ku take risk) ila hawafanyi hivyo bila ya kufikiri kwa kina. Kama kuna uwezekano wa kupata faida kubwa ila pia kuna hatari, unaweza kujipima uwezo wako wa kukabiliana na hatari hiyo na kisha ukachukua hatua.

10. Jua nini maana ya mafanikio.

Au jua ni kiwango gani cha fedha kinakutosha wewe kuishi maisha unayotaka wewe. Kwa bahati mbaya sana hakuna kiwango kimoja ambacho kinawatosha wote, hivyo kila mtu ana kiwango chake kulingana na maisha yake. Je kiwango chako ni kipi?

Fuata hatua hizi kumi na utafikia uhuru wa kifedha. Kumbuka kwamba mambo haya yanachukua muda hivyo jipe muda wa kutosha na endelea kufurahia maisha yako kwa kila hatua. Usisubiri kwamba ukishafikia uhuru wa kifedha ndio utafurahia maisha, utakosa maisha yako yote.

TUPO PAMOJA.