Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu THINK AND GROW RICH kama hukusoma makala za uchambuzi uliopita bonyeza maandishi haya THINK AND GROW RICH.
Kuna aina mbili za maarifa, maarifa ya kawaida na maarifa ya kitaalamu.
Maarifa ya kawaida hata ungekuwa nayo mengi kiasi gani, hayawezi kukusaidia kufikia utajiri. Haya ni maarifa ambayo yamekuwa yakipatikana kwa urahisi kwenye jamii na hata kwenye mfumo wa elimu.
Maarifa ya kitaalamu ni yale maarifa ni yale maarifa yanayomfanya mtu kuwez akufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi na hivyo kuwa na uzalishaji mkubwa zaidi na hivyo kumuwezesha kufikia utajiri.
Maarifa yoyote utakayokuwa nayo hayawezi kukuletea fedha, mpaka pale autakapoweza kuyatumia na kuyafanyia kazi ndio yatakuletea fedha. Watu wengi wanasema kwamba maarifa ni nguvu, huu sio ukweli kwa sababu kuwa tu na maarifa sio nguvu. Ila kutumia maarifa uliyonayo ndio unaweza kupata nguvu ya kupata chochote unachotaka.
Kinachokosekana kwenye mfumo wa elimu ni jinsi mtu anavyoweza kutumia maarifa anayopata. Katika mfumo wa elimu mwanafunzi anafundishwa vitu vingi sana lakini jinsi anavyoweza kutumia vitu hivyo kwenye maisha yake ya kawaida hajui. Hii ndio inafanya wahitimu wengi wa vyuo vikuu kuwa na thamani ndogo, kwa sababu wanakuwa na maarifa mengi ambayo hawawezi kuyatumia.
Watu wengi hufikiri kwamba mtu ambaye hajaenda shule au hajafaulu vizuri shuleni hana maarifa. Ila ukiangalia kiuhalisia matajiri wengi hawana elimu kubwa na watu wengi waliosoma sana sio matajiri. Hii ni kwa sababu wasomi wamekuwa shuleni kwa muda mrefu wakipewa maarifa mengi ambayo hawawezi kuyatumia moja kwa moja kutengeneza fedha. Ila matajiri kwa sababu hawajapata nafasi ya kukaa kwenye elimu kwa muda mrefu, wanatumia muda wao kujifunza maarifa ambayo wanaweza kuyatumia kupata fedha.
Kuna kisa kimoja ambapo wakati wa vita vya dunia, mwandishi mmoja aliandika kwenye gazeti kwamba Henry Ford ni mtu mjinga na asiyekuwa na elimu. Henry kipindi hiko ndio alikuwa mtu tajiri sana duniani, na aelimu yake aliishia darasa la sita. Ford alikwenda mahakamani kwa kuchafuliwa jina lake.
Katika kesi, Ford aliitwa kutoa ushahidi na ili kudhibitisha kwamba Ford hana elimu walimuuliza maswali kama, ni wanajeshi wangapi wa uingereza walipelekwa marekani wakati wa vita vya mwaka 1776, na maswali mengine kama hayo. Ford hakuweza kujibu maswali yote hayo, baadae akawaambia wale wanasheria, kama nikitaka kupata jibu la swali lolote, naweza kuchukua mtu yeyote kutoka kwenye timu yangu anayeweza kuwajibu. Mimi nimezungukwa na watu walio na taarifa zote hizo, mimi sizihitaji, lakini nikizitaka kwa muda wowote nazipata. Sasa kwa nini nijaze kichwa changu na taarifa ambazo haziwezi kunisaidia? Wote walikaa kimya baada ya jibu lile, maana walijua ni jibu la busara sana.
Kabla hujatekeleza lengo lako la kuwa tajiri, unahitaji kuwa na maarifa ya kitaalamu kwa kazi au biashara ambayo umepanga kufanya ili kufikia kwenye utajiri. Unahitaji maarifa ambayo yatakuwezesha kutumia mazingira yanayokuzunguka vizuri ili uweze kufikia lengo lako hilo kubwa, Kumbuka maarifa unayohitaji wewe sio ya kawaida, bali ya kitaalamu. Kama ni biashara unahitaji maarifa yatakayokuwezesha kukuza biashara yako. Kama ni kazi au huduma nyingine unahitaji maarifa ambayo yatakuwezesha wewe kufanya kazi bora.
Moja ya njia nzuri sa kupata elimu hii ni kuwa na MASTER MIND GROUP. Hili ni kundi ambalo linakuwa na watu ambao mna malengo sawa ila mnaweza kuwa na maarifa tofauti tofauti na hivyo kusaidiana katika kufikia utajiri. Watu wote ambao wamefikia mafanikio makubwa walikuwa na master mind group zao ambazo ziliwawezesha kupata maarifa waliyohitaji ili kufika kileleni.
Kununua maarifa kutakulipa sana.
Unahitaji kununua maarifa, ambayo yatakuwezesha kufikia utajiri mkubwa. Maarifa hayo yatakulipa kwa kiasi kikubwa sana kuliko ulichotoa(kama kwenye KISIMA CHA MAARIFA)
Kabla ya kupata maarifa, amua kwanza ni maarifa gani unahitaji ili uweze kufikia lengo kubwa ulilojiwekea kwenye maelezo yako ya kufikia utajiri.
Baada ya kujua maarifa unayohitaji, sasa unaweza kuangalia ni wapi utapata maarifa hayo. Baadhi ya njia unazoweza kutumia kupata maarifa ni;
1. Uzoefu wako mwenyewe na elimu uliyopata.
2. Uzoefu na elimu za watu wengine ambao upo nao kwenye MASTER MIND GROUP.
3. Kwenye vyuo mbalimbali.
4. Kusoma vitabu, majarida na kwa sasa mitandao mbalimbali.
5. Kozi maalumu zinazotolewa.
Elimu utakayoipata ni muhimu kuiweka kwenye mipango na kuanza kufanyia kazi. Lakini kama utapata elimu na kukaa nayo tu haitakuwa na msaada wowote kwako.
Kama umesoma na unataka kurudi tena shule kuongeza elimu, jiulize elimu utakayoongeza itakusaidiaje kufikia malengo yako. Kama haina msaada wowote unapoteza muda wako na fedha pia. Maana muda utakaokaa shuleni ungeweza kufanya mengi ya kukufikisha kwenye malengo yako.
Watu wote waliofanikiwa ni watu ambao wanajua kujifunza hakuna mwisho. Ni watu ambao kila siku wanatafuta maarifa yanayowawezesha kuboresha maisha yako. Watu ambao hawana mafanikio hufikiri kwamba wanapohitimi masomo ndio mwisho wa kusoma. Ukweli ni kwamba elimu unayopata shuleni haina msada mkubwa kwako kufikia mafanikio, ila inakufungulia wewe mlango wa kuanza kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio.
Dunia pia imebadilika sana hasa kwenye mazingira ya kazi. Wale wanaoajiri, sasa hivi hawaangalii tena ufaulu wa alama za juu, bali wanaangalia watu ambao wanaweza kujifunza na kushirikiana na wengine. Ndio maana wanafunzi ambao wanaonekana kuwa na shughuli mbalimbali wakati wa masomo yao hupata kazi nzuri kuliko wale ambao walikuwa wakisoma tu.
Tukutane kwenye sehemu ya pili ya uchambuzi huu…