Mtandao wa intaneti umerahisisha karibu kila kitu kwenye maisha yetu. Sasa hivi mtu kwa kuwa na mtandao, na akawa na kompyuta au simu yenye uwezo mkubwa(smartphone) anaweza kuanzisha biashara popote alipo na akiwa na mipango mizuri anaweza kufanikiwa sana.

Mtandao wa intaneti umerahisisha sana ufanyaji wa biashara, kwani kupitia mtandao huu mtu anaweza kutafuta soko la bidhaa au huduma anazotoa.

Pamoja na faida hii kubwa ya mtandao wa intaneti, kuna watu wengi ambao wanautumia vibaya kwa kuwatapeli wengine.

Njia zinazotumia kuwatapeli watu kupitia mtandao.

Kuna njia nyingi sana ambazo zinatumika kuwatapeli watu kupitia mtandao. Hapa nitazungumzia njia kuu mbili ambazo nimeona wengi wakitapeliwa kwa njia hizo.

1. Kupata mikopo rahisi.

Kwenye mitandao ya kijamii, hasa facebook kuna matapeli wanaotumia jina la vicoba saccos. Watu hawa wanaahidi kutoa mikopo rahisi na kwa haraka kupitia njia ya simu. Ili kuwakamata vizuri watu, wamekuwa wakitumia majina ya watu maarufu kusambaza habari hizi. Kwa mfano wanafungua account kwenye facebook kwa jina kama Zitto Kabwe, kisha wanaweka maelekezo kwamba kuna njia rahisi ya kupata mikopo. Kwa watu kuona habari hii inatolewa na mtu wanayemfahamu, inakuwa rahisi kwao kuchukua hatua na hatimaye wanatapeliwa.

Watu wengi sana wametapeliwa kwa njia hii. Na pia watu hawa wamekuwa wakitumia majina ya watu wanaojulikanan kwenye jamii na wakati mwingine wanatumia habari maarufu kujiwekea nafasi nzuri ya kuaminika.

Matapeli hawa huelekeza watu kwenye tovuti zao ambazo pia sio halisi. Tovuti hizo hukuta zimeishia na neno wapka.mobi, ukiona kitu kama hiki kimbia haraka sana.

2. Aina ya pili ya utapeli ni kufanyishwa kazi ambayo huna uhakika wa kulipwa. Katika aina hii ya pili, hakuna mtu anayekuambia utume fedha, ila wewe unapewa majukumu ya kufanya na pia kuambiwa ushawishi watu wengi wajiunge na kwamba utalipwa kulingana na kazi uliyofanya. Kwa uzoefu wangu mdogo, sijawahi kuona mtu aliyelipwa kwa kazi za aina hiyo.

Mifano ya utapeli huu ni link ambazo watu wanashirikishana, unakuta inakuambia pata dola 100 kila siku ukiwa nyumbani. Halafu kazi wanayokupa ni kubonyeza matangazo, na pia kualika wengi zaidi nao wajiunge.

Watu wengi wamekuwa wakisambaziana ujumbe wa aina hii wakiamini kwamba jinsi unavyoingiza watu wengi ndivyo unavyopata fedha nyingi, baadae wanapotaka kupata fedha zenyewe ndipo wanagundua kwamba ni utapeli.

Ni njia zipi halali unazoweza kutumia kutengeneza fedha kwenye mtandao.

Nimekuwa nafanya biashara kwa njia ya mtandao wa intaneti kwa muda sasa. Na kwa hapa tanzania kuna njia tatu muhimu unazoweza kutumia kujitengenezea kipato cha njia ya mtandao.

1. Njia ya kwanza, kuwa na website, au blog ambayo inatoa taarifa mbalimbali na watu wanaipenda kuifuatilia. Kama ukiwa na watu wengi unaweza kuweka matangazo ya watu wengine na ukalipwa. Unaweza kuweka matangazo ya moja kwa moja kutoka makampuni ya hapa Tanzania au unaweza kujiunga na mpango wa google wa matangazo na wao wakaweka matangazo yao kwenye website/blog yako na wakakulipa kulingana na idadi ya watembeleaji.

Njia hii ni rahisi sana na wengi sasa wanaitumia vibaya, kwa mfano kwa sababu watu wengi wanapenda udaku na kuona picha za uchi, basi kuna blog nyingi sana zimeanzishwa zinazotoa habari za udaku na picha za uchi. Jinsi mnavyotembelea wengi ndivyo wanavyopata kipato. Japokuwa hii pia sio njia nzuri ya kuvutia watu kwenye website au blog(kutumia picha za uchi).

2. Njia ya pili ni kuwa na bidhaa au huduma zako mwenyewe na kutumia mtandao kuzitangaza na hata kuziuza moja kwa moja. Kupitia njia hii unakuwa na tovuti au blog ambayo inaeleza kuhusu bidhaa au huduma unazotoa. Watu wanakujua kupitia mtandao na wanakutafuta ili uweze kuwauzia bidhaa au huduma hizo.

Kama upo kwenye biashara yoyote ila ni muhimu sana kuwa na blog ambayo itakuwezesha kuwafikia wateja wengi zaidi. Ni njia rahisi sana ya kutangaza na usambaaji wake hauna kikomo.

3. Njia ya tatu ni kuuza bidhaa za wengine. Unaweza kuanzisha tovuti au blog ambapo wewe unakuwa unatangaza na kuuza bidhaa za watu wengine au makampuni mengine. Kwa kiingerea hii inajulikana kama affiliate marketing. Kwa njia hii wewe unachagua bidhaa au huduma ambayo unaona watu wanaihitaji au inaweza kuwasaidia na klisha unawashawishi wainunue. Unaweza kutengeneza kipato kizuri sana kwa njia hii kama ukiweza kuchagua bidhaa/huduma nzuri.

Unawezaje kuepuka utapeli kwenye mtandao?

Siku moja tapeli mkubwa sana aliulizwa ni mtu gani rahisi kumtapeli, tapeli yule alijibu, ni rahisi sana kutapeli mtu ambaye sio mwaminifu, na ni vigumu sana kumtapeli mtu ambaye ni muaminifu.

Kwa kifupi ni kwamba ukiwa mwaminifu hakuna anayeweza kukutapeli. Ila unapokosa uaminifu na kuanza kutafuta njia rahisi za kujipatia fedha(ambazo hazipo) ndio unadondoka mikononi mwa matapeli na wao wanashangilia.

Ili kuepuka kutapeliwa kwenye mtandao, zingatia mambo yafuatayo;

1. Hakuna kitu cha bure. Ili upate fedha unahitaji kufanya kazi ambayo itazalisha thamani kwa mtu mwingine. Unapokutana nafursa yoyote ya kutengeneza kipato kwenye mtandao, jiulize je ni thamani gani ambayo natengeneza hapa? Yaani mtu mwingine anafaidika vipi na hiki ninachofanya kwenye mtandao ili kupata fedha. Kama hakuna anayefaidiaka usiingie kwenye biashara hiyo.

2. Hakuna njia ya mkato. Ili kupata kitu unachotaka, hakuna njia ya mkato. Unahitaji kufuata kila hatua muhimu ndio uweze kufikia kile unachotaka. Ukishaanza kutafuta njia za mkato umekwisha, ni lazima utatapeliwa.

3. Hakuna mkopo unaopatikana kirahisi. Njia hii ya mikopo kupitia mtandao imesababisha wau wengi sana kutapeliwa. Labda nikuulize swali, mtu akaja sasa hivi hapo ulipo akakuambia nikopeshe elfu 50 na nitakurudishia, hata kama unayo utamkopesha? Kumbuka huyo ni mtu ambaye humjui, hujui anakwenda kufanya nini na fedha hizo ila anataka umpatie. Mtu yeyote mwenye akili timamu hawezi kumkopesha fedha mtu asiyemjua, tena asiyejua anakwenda kufanya nini na fedha hizo. Ndio maana mabenki na taasisi nyingine wanakuwa na dhamana, ili mkopaji asikimbie. Sasa inakuwaje mtu uweze kuamini kwamba kwa kutuma fedha kidogo kwa mpesa unawez akupatiwa mkopo mkubwa?

Uanzie wapi kutengeneza fedha kwenye mtandao?

Kama upo makini na unataka kuanza biashara yako kupitia mtandao wa intanet, nimeandika kitabu kinachoelezea hatua kwa hatua ni jinsi gani unaweza kufanya hivyo. Kitabu hiki kinaitwa JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG ni kitabu kilichoandikwa kwa lugha rahisi ya kiswahili na kina maelekezo ya picha. Kwa maelezo zaidi bonyeza hayo maandishi ya jina la kitabu. Na kukipata tuma fedha tsh elfu 10 kwenye namba 0717396253/0755953887 na kisha tuma email yako na utatumiwa kitabu mara moja. Kitabu kipo kwa mfumo wa softcopy ambapo utaweza kusomea kwenye kompyuta au simu yenye uwezo mkubwa.

Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya kuboresha maisha yako.

TUPO PAMOJA.

kitabu-kava-tangazo432