Kujijengea taswira ndio sehemu kuu ambapo akili ya mtu inaweza kutengeneza mipango yote. Hamu ya kufikia mafanikio inatengenezewa umbo, kupewa sura na kufanyiwa kazi kupitia uwezo huu wa kujijengea taswira.
Imekuwa ikielezwa kwamba mtu anaweza kutengeneza chochote anachoweza kufikiria na kutengenezea taswira.
Katika miaka yote ambayo imepita, hiki ni kipindi kizuri sana cha kutumia uwezo wa kujijengea taswira kwa sababu ni kipindi cha mabadiliko ya haraka.
Kupitia uwezo wa kujitengenezea taswira, mtu anaweza kugundua na kutumia nguvu za asili katika kutimiza malengo yake. Watu wameweza kutumia hewa kupitisha mawimbi ya sauti na kuwasiliana kwa simu katika maeneo tofauti tofauti, hii yote ilianza na mtu kupata taswira ya watu kuweza kuwasiliana kwa urahisi. Sasa hivi kwa kutumia mtandao wa intaneti unaweza kuwasiliana na mtu yeyote popote alipo duniani. Hii yote ilianza na mtu kupata picha ya mawasiliano kuwa rahisi na kuweza kutumia nguvu za asili kukamilisha picha hiyo.
Katika maendeleo yote yanayotokea duniani, yanaanza na mtu anayepata picha ya maisha kuwa bora kuliko yalivyo sasa na kuweza kufanyia picha hiyo kazi.
Kikomo pekee cha uwezo wa binadamu kipo kwenye maendeleo na matumizi ya uwezo wake wa kujijengea taswira. Kwa kutumia vizuri uwezo huu wa kujenga taswira, mtu anaweza kufanya mambo makubwa sana.
AINA MBILI ZA KUJIJENGEA TASWIRA.
Uwezo wa mtu wa kujijengea taswira umegawanyika katika aina kuu mbili.
1. TASWIRA AWALI.
Hii ni taswira ambayo mtu anajijengea kwa kutumia mawazo au mipango ambayo tayari ipo. Kikubwa anachokifanya mtu ni kuoanisha mawazo au mipango mbalimbali na kupata wazo moja au mpango mmoja ambao ni bora sana. Kwa njia hii mtu anaweza kuboresha chochote anachotaka kuboresha.
2. TASWIRA BUNIFU.
Hii ni taswira ambapo mtu anajijengea baada ya kupata wazo jipya, au kitu kipya ambacho hakijawahi kufanyika ila kinaweza kuboresha sana maisha au mambo yanavyofanywa. Taswira hii inaweza kutengenezwa pale mtu anapoweza kufikia uwezo wake wa juu kabisa unaomuunganisha na uwezo mkubwa wa dunia na hatimaye kupata mawazo ambayo ni ya tofauti kabisa.
Taswira bunifu inasaidiwa sana na akili ya ndani, subconscious mind katika kufikia uwezo mkubwa na kupata mawazo mapya. Taswira hii inafanya kazi kwa kujiongoza yenyewe na hivyo inavyoweza kutumiwa vizuri inaleta majibu mazuri sana. Taswira hii inafanya kazi pale ambapo akili ya mtu(consious mind) inapata mawazo yenye shauku kubwa au yenye hisia kali.
Viongozi wakubwa, wafanyabiashara wenye mafanikio, wasanii wakubwa na hata waandishi wakubwa wameweza kufikia ukuu wao kwa kutumia uwezo wao wa TASWIRA BUNIFU. Uwezo wako wa kujijengea taswira unakuwa imara kadiri unavyotumika, na usipotumiwa huwa dhaifu ila hauwezi kufa kabisa. Wakati wowote utakapoanza kutumia tena uwezo wako huu unaweza kuanza kunufaika nao.
Hamu ya wewe kufanikiwa na kuwa tajiri ni mawazo tu. Bila mawazo haya kubadilishwa na kuw akitu kinachoonekana huwezi kupata utajiri. Unaweza kubadili mawazo haya kwa kujijengea taswira ya kile unachotaka na taswira hii ikakuwezesha wewe kuanza kuchukua hatua ya kuweza kufikia kile unachotaka.
Ili kuweza kubadili hitaji lako la kuwa tajiri na uweze kutengeneza fedha, unahitaji mpango au mipango. Mipango hii itatengenezwa kwa kujijengea taswira. Ili kuhakikisha mipango hii inatekelezeka ni muhimu sana kuiandika na kuieleza kwa njia ambayo itakuwa rahisi kwako kuifikia.
Dunia na vyote vinavyokuzunguka ni vitu vidogo vidogo ambavyo vimepangwa kwa ustadi mkubwa. Sayansi imeweza kuonesha kwamba ulimwengu mzima umeundwa na vitu viwili tu, maada(matter) na nguvu(energy). Vitu vingine vyote vimetengenezwa kutoka kwenye vitu hivi viwili. Hivyo kwa kuitumia uwezo wako mkubwa unaweza kutengeneza chochote unachoweza kukijengea taswira kwenye akili yako.
Sheria za asili zimeweza kutengeneza vitu vyote vinavyotuzunguka. Na wewe pia unaweza kutumia sheria hizi kutengeneza chochote unachotaka. Mfano wa jinsi sheria za asili zinatengeneza kitu kuanzia hatua ndogo kabisa ni maisha ya binadamu. Hapo ulipo wewe ulitokana na chembe ndogo sana mbili ambazo huwezi hata kuziona kwa macho. Chembe hizi ziliungana na hatimaye ukaanza kukua kama mimba, ukazaliwa na kuendelea kukua mpaka kufikia utu uzima.
Utumie uwezo wako wa kujijengea taswira bunifu kuweza kupata njia za kukuwezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Tutaendelea na sehemu ya pili ya uchambuzi huu kwenye makala ijayo.
Nakutakia kila la kheri kwenye maisha yako ya kitajiri.
TUPO PAMOJA.