Mpaka sasa tumeshaona uaminifu ni tabia muhimu sana ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Hii ni kwa sababu unapokuwa mwaminifu watu wengi wanakuamini na wanakuwa tayari kushirikiana na wewe.

Leo tutajadili jinsi ya kuepuka mazingira ambayo yanakuondolea tabia ya uaminifu. Hapa tutaangalia mbinu muhimu ambazo zitakuondoa kwenye mtego ambao utakufanya ufanye jambo ambalo sio la kuwa muaminifu.

Kuna wakati ambao unajikuta kwenye wakati mgumu na inakubidi usiwe muaminifu ili uweze kutoka kwenye wakati huo mgumu. Japokuwa unaweza kuona kutokuw amwaminifu kumekusaidia, sio kweli, kuna kuharibia kuliko kulivyokusaidia. Maana unapokosa uaminifu kwenye eneo moja, inasambaa na kwenda kwenye kila eneo la maisha yako.

Zifuatazo ni mbinu unazoweza kutumia ili kuepuka mazingira yanayoweza kukufanya ushindwe kusimamia tabia yako ya uaminifu.

1. Acha kujilinganisha na wengine na jiamini.

Unapojilinganisha na wengine unaweza kuona wengine wamefanikiw akuliko ulivyofanikiwa wewe. Unaweza kuona wengine wanafanya vizuri kuliko unavyofanya wewe. Kwa kufanya hivi unajiondolea kujiamini na unapokosa kujiamini ni vigumu sana kuw amwaminifu. Unapokosa kujiamini inakuwa rahisi kwako kudanganya ili uonekane na wewe unakitu fulani.

Acha mara moja kujilinganisha na wengine, jua kwamba wewe ni wa pekee na hakuna anayefanana na wewe. Jiamini kw akile unachofanya na jivunie kwa hiko. Hata mtu atakapokuuliza unafanya nini unakuwa tayari kumweleza ukweli.

2. Acha kuishi maisha ya kuigiza na usitake kuwafurahisha watu.

Maisha ni maigizo, kama hutaki kufikia mafanikio unaweza kukubaliana na kauli hiyo na ukaendele akuigiza. Sehemu kubwa ya maisha ya kila mtu ni kuigiza, kufanya mambo ili kuwafurahisha wengine. Hii ni mbaya sana kwenye kujijengea uaminifu maana maisha yako yote yanakuwa yamejengwa kwenye kitu ambacho sio cha kweli.

Mara nyingi watu ili kutaka kuonekana wanafanya kitu muhimu au wana maisha mazuri wamekuwa wakidanganya. Wanadanganya ili maisha wanayoigiza kuishi yafanane na ukweli ambao hawawezi kuwa nao. Mtu anaweza kuwa anavaa vizuri na kuwaambia watu anafanya kazi ofisi kubwa kumbe sio kweli. Mtu anaweza kuonekana yuko ‘bize’ kwenye biashara na kuwaambia watu anapata faida kumbe sio kweli.

Kama ukiacha kuigiza maisha na kuacha kutaka kuwafurahisha watu utaanza kuishimaisha yako na utayafurahia kwa kiasi kikubwa sana. Utakuwa mwaminifu na watu hawatakuwa na wasi wasi na wewe.

3. Usisikilize umbea, majungu.

Kwenye kujijengea tabia ya uaminifu tulijifunza kutoshiriki kwenye umbea au majungu. Sasa ni rahisi kusema hujashiriki kwa sababu wewe hujaongea umbea au majungu, lakini ukweli ni kwamba kw akusikiliza tu tayari umeshiriki na inaweza kukuondole auaminifu.

Unapoanza kuongea na mtu na akakuambia, nakuambia siri hii…., au nakuambia wewe tu…. au usimwambie mtu yeyote…. kimbia haraka sana kwa sababu utakavyoendelea kusikiliza utajiingiza kwenye mtego wa kutokuwa mwaminifu. Kwa sababu kwa kusikiliza, unaweza kushindwa kukaa nacho na kujikuta umemwambia mwingine halafu ukazidi kusambaza umbea. Au unaweza kukaa nacho na usimwambie mtu yeyote halafu baadae ikaja kufahamika ulikuwa unajua ila hukuwaambia watu mapema na ukaonekana sio mwaminifu.

Hivyo kwa kusikiliza tu umbea, tayari unakuwa sio mwaminifu. Maana ukikaa nzao unakuwa sio mwaminifu na ukiusema unaweza pia kujiondole auaminifu wako. Suluhisho, kimbia unaponusa harufu ya umbea.

4. Jiwekee amri zako mwenyewe, misingi ambayo utaisimamia.

Kama hutasimama kwa chochote basi utaanguka kwa chochote. Hii ni kweli kabisa, kama huna misingi ambayo unaisimamia kwenye maisha, ni rahisi kushawishika kufanya mambo ambayo yatakuingiza kwenye matatizo.

Jijengee misingi ambayo utaiheshimu na hii itakuepusha kujikuta kwenye matatizo ambayo yatakuondolea uaminifu. Kwa mfano kama moja ya misingi unayoisimamia ni kazi ndio msingi wa maendeleo(jijengee msingi huu), hakuna atakayeweza kukudanganya na kukuingiza kwenye utapeli. Maana chochote ambacho sio kazi kwako kitakosa nafasi.

Unapokosa misingi, au unaposhindwa kuisimamia unatoa nafasi kwa tabia zisizokuwa za uaminifu kukunyemelea.

5. Kila mara jikumbushe kwamba uaminifu ni kitu muhimu kwako.

Njia bora kabisa ya kujinasua kwenye mtego utakaokufanya usiwe mwaminifu ni kujikumbusha kila mara kuhusu uaminifu na umuhimu wake kwenye maisha yako. Kila unapofanya jambo jiulize je jambo hili linanijengea uaminifu? Nenda mbali zaidi na kujiuliza je kama jambo hili lingeandikwa kwenye ukurasa wa kwanza wa magazeti yote, je ingekuwa ni kwa wema au kwa ubaya?

Na kikubwa zaidi jiulize je kama jambo unalofanya lingekuwa ndio sheria na kila mtu duniani angetakiwa kulifanya je dunia ingekuwa sehemu nzuri ya kuishi? Maswali haya yatakufanya utafakari mara mbili kabla hujafanya jambo lolote linaloweza kukuvunjia heshima yako. Na kwa kuwa mambo mengi yasiyokuwa ya uaminifu hufanyika kwa kificho, kama ukiweza kuwa mwaminifu na nafsi yako na kujiuliza maswali hayo utaweza kuepuka mazingira yanayokushawishi usiwe mwaminifu.

Uaminifu ni tabia muhimu sana unayohitaji ili kufikia mafanikio. Lakini tunaishi kwenye mazingira ambayo yanatushawishi na kutulazimisha kutokuwa waaminifu. Usikubali kabisa kubebwa na mazongira haya, tumia hizo mbinu hapo juu kujiondoa kwenye mazingira hayo ili kuweza kujijengea tabia ya uaminifu.

Nakutakia kila la kheri kwenye maisha ya mafanikio uliyoamua kuishi.

TUPO PAMOJA.