JINSI YA KUTUMIA KUJIJENGEA TASWIRA KIUHALISIA.

Mawazo ndio chanzo kikuu cha utajiri wote. Mawazo ni zao la kujijengea taswira.

Mfano wa mawazo yaliyoleta mapinduzi na kuleta utajiri mkubwa.

Miaka mingi iliyopita, daktari mmoja wa kijijini aliingia kwenye duka la dawa mjini akiwa amebeba birika lake. Alipofika kwenye duka lile alianza kuongea na karani wa pale na walikuwa wakiongea kwa lugha ya chini na kw amuda mrefu. Baadae walionekana kukubaliana na daktari yule alimpa karani birika alilokuwa amebeba. Karani alikagua birika lile na kuingia mfukoni kwake na kutoa fedha na kumpa daktari yule. Fedha zile zilikuwa dola 500 na ilikuwa ndio akiba pekee ya karani yule.

Baada ya kupokea fedha zile, daktari alichukua kipande cha karatasi na kuandika kanuni ambayo alimpa karani yule. Kanuni ile ilikuwa na siri kubwa sana ya utajiri. Kanuni ile ingewezesha birika lile lianze kutengeneza utajiri ila daktari yule wala karani hawakuwa na uhakika.

Daktari yule alifurahia kuuza birika lile kwa dola 500 na kuondoka zake. Alijua fedha zile zingemwezesha kulipa madeni yake na kumpa uhuru wa nafsi.  Kwa upande wa pili karani alikuwa anafanya kitu cha hatari kw akuweka akiba yake yote rehani kwa kununua kipande cha karatasi na birika la zamani. Hakujua kwamba alichofanya kingekuja kumletea utajiri mkubwa sana katika maisha yake na ya watu wengine pia.

Kitu ambacho karani yule alinunua kilikuwa ni wazo, birika lilikuwa la kawaida tu, ila wazo lililoandikwa kwenye kanuni lilikuwa kubwa sana. Maajabu ya birika lile yalianza kuonekana pale karani yule alipoanza kutumia kanuni ile na kuongeza siri nyingine ambayo yule daktari hakuijua. Endelea kusoma hadithi hii kwa makini na tumia uwezo wako wa kujenga taswira na uone kama utaweza kujua siri aliyoongeza karani yule. Kumbuka hadithi hii ni ya kweli na unaweza kujifunza mambo mengi sana hapa.

Birika lile limeleta maajabu makubwa sana kwa watu. Limekuwa chanzo kikubwa cha biashara na hata ajira kwa watu waliojihusisha na kile kilichozalishwa. Birika hili limefanya mapinduzi makubwa sana kwenye biashara, limewezesha maendeleo makubwa sana kwenye mji ambapo lilianzia na limekuwa kampuni bora sana duniani. Kampuni ambayo imeweza kustahimili vipindi vigumu sana vya kiuchumi. Wakati ambapo kampuni nyingi zimekufa kutokana na mdororo wa uchumi, kampuni iliyotokana na birika lile imeendelea kukua siku hadi siku.

Birika hili limetoa bidhaa ambayo kila mmoja wetu amewahi kuitumia kwenye maisha yake, na kuifurahia pia. Birika hili limetoa bidhaa inayoitwa COCA-COLA. Hii imetokana na wazo hilo ambalo daktari alimuuzia karani wa duka la dawa pamoja na birika. Karani yule alitumia kanuni aliyopewa na kuichanganya na siri moja kubwa sana ambayo imemuwezesha kufikia mafanikio makubwa sana. Siri hii daktari yule aliyegundua kanuni ya coca-cola hakuweza kuijua au kuitumia.

Je wewe umeshajua siri hii ni ipi? Umejua? Umeumiza kichwa uje na jibu…

Siri hiyo ni uwezo wa kujenga taswira. Daktari alikuwa na kanuni nzuri ya kutengeneza kinywaji ambacho kinaburudisha sana. Ila hakuweza kujenga taswira kubwa ya kuweza kutengeneza kinywaji ambacho kingekuwa kipenzi namba moja cha watu duniani. Siri hii ilimwezesha karani kupata mabilioni ya dola ila daktari aliyeigundua aliishia kupata dola 500 tu?

Mawazo ni nguvu zisizoonekana, lakini zina uwezo mkubwa sana kuliko hata akili iliyozalisha mawazo hayo. Mawazo yana nguvu ya kuendelea kuishi hata pale aliyeyatoa anapokuwa amekufa.

Usiogope kutengeneza mawazo yako, usiogope kuyafanyia kazi mawazo yako. Anza kidogo na siku moja wazo lako litakua sana. Unachohitaji ni uwezo wa kujenga TASWIRA kubwa kwenye maisha yako ya kukuwezesha kufikia mafanikio makubwa kupitia mawazo yako.

Je ni mara ngapi ambapo umekuwa unapata wazo, unalipuuzia halafu miaka michache baadae unashangaa kuna mtu amefanikiwa sana kwa wazo ambalo ulilipuuza? Ni mara nyingi sana na hii ni kwa sababu unapopata wazo haliishii kwako tu bali mtu yeyote anayefikiria anaweza kupata wazo kama la kwako. Na kama mtu huyo atakuwa na uwezo wa kujenga taswira kubwa kupitia wazo hilo anaweza kutengeneza mafanikio makubwa sana.

Je umejifunza nini kwenye mfano wa coca-cola hapo juu? Tushirikishe mambo matano uliyojifunza na utakayoanza kuyafanyia kazi ili uweze kufikia mafanikio na utajiri mkubwa.

Kumbuka unavyotushirikisha ndio unaelewa zaidi na unailazimisha akili yako na mawazo yako kufanya hiko ambacho umekiandika.

Karibu utushirikishe ili tuweze kujifunza zaidi.

Nakutakia kila la kheri katika maisha yako ya mafanikio na utajiri.

TUPO PAMOJA.