Uaminifu ni moja ya tabia muhimu sana unazohitaji kujijengea. Hii ni kwa sababu kwa tabia ya uaminifu itakuwezesha kufikia mafanikio makubwa sana kuliko ambayo ungeyafikia kama usingekuwa na tabia ya uaminifu. Leo tutaona uhusiano wa karibu kati ya tabia ya uaminifu na mafanikio makubwa kwenye maisha.
Kama tulivyoona kwenye siku ya kwanza, kutokuwa mwaminifu kunaweza kukuletea mafanikio, ila sio mafanikio unayoweza kujivunia na mafanikio hayo hayawezi kudumu. Chukua mfano wa mwizi au jambazi ambaye anapata fedha nyingi sana kwa kuwaibia wengine. Kwa nje anaweza kuonekana ana mafanikio ila maisha yake yanakuwa magumu sana. Na muda wowote chochote alichonacho kinaweza kupotea.
Chukua mfano wa mafisadi na wapokea rushwa. Wanaweza kuonekana wana fedha nyingi sana ila hazipimi mafanikio kwao. Chukua mfano wa mtu anayeiba mabilioni ya fedha na kwend akuyaficha nchi za nje. Ukweli ni kwamba anaweza asimalize kuyatumia mabilioni hayo mpaka atakapokufa, ila pia hawezi kuyafurahia, maana atayaweka kama siri. Na siku yoyote mambo yanaweza kugundulika na ikawa aibu kubwa kama ambavyo tumekuwa tunashuhudia hapa nchini kwetu mara kwa mara.
Badala ya kutafuta njia ambazo zitakupatia unachotaka ila pia zikakuacha na doa, kwa nini usitumie muda huo kupita njia ambazo ni za uaminifu na ukapata kitu ambacho unaweza kujivunia mbele za watu na unajua umewasaidia wengi katika kufikia hatua hiyo. Haya yatakuwa mafanikio ya kweli, kwani hata kama kipato chako ni kidogo, angalau utakuwa na uhakika wa kuwasaidia wengi zaidi kwa maisha uliyoishi.
Uhusiano kati ya uaminifu na mafanikio.
1. UAMINIFU unajenga IMANI.
Unapokuwa muaminifu watu wanakuamini na watu wanapokuamini wanaweza kufanya kile unachowaambia wafanye na hivyo inakuongezea ushawishi. Mafanikio yako yanatokana na watu wanaokuzunguka, kadiri watu wengi wanavyokuzunguka wanavyokuamini ndivyo nafasi yako ya kufikia mafanikio inazidi kuwa kubwa.
Kwa mfano kama unafanya biashara, ni lazima wateja waamini kwamba kile unachouza kitawasaidia kutatua matatizo yao. Wakishakuamini watanunua unachouza na kama kikiwasaidia watakuja tena kukinunua na kila wanapokutana na mtu mwenye tatizo kama lao hawatasita kumuelekeza aje kwako ili kutatuliwa tatizo lake. Lakini kama utawauzia kitu ambacho hakitawasaidia hawatakuja tena kununua na kila watakapokutana na mtu anayezungumzia habari zako watatoa ushahidi wao kwamba kwa nini wewe hupaswi kuaminiwa.
Kama umeajiriwa, majukumu utakayopangiwa yataendana na jinsi gani mwajiri wako anakuamini. Kama amewahi kukupa majukumu na ukayatekeleza vizuri bila ya matatizo, atakuwa na imani na wewe na kila akipata jukumu ambalo linahitaji umakini anakupatia wewe. Kwa kuendelea hivi unajikuta unapewa majukumu makubwa zaidi na baadae thamani yako kupanda hivyo kipato na ushawishi kukua zaidi. Unaweza kuishia kuwa kiongozi mkubwa kwenye kazi unayofanya.
Unaweza kuona kitendo kidogo cha uaminifu unachofanya hakuna anayekiona ila ukweli ni kwamba vitendo hivi vinajijenga na baada ya muda unakuwa mtu ambaye unaaminika, unakuwa na ushawishi na unafikia mafanikio makubwa sana.
2. UAMINIFU UNARAHISISHA MAISHA.
Kwanza hatua ya kwanza ya kuwa na mafanikio kwenye maisha ni kuwa na maisha rahisi. Na hatua ya kwanza ya kuwa na maisha rahisi ni kuwa mwaminifu. Baasi, ni hivyo tu na tunaweza kuishia hapa.
Kwa mfano kama wewe sio mwaminifu, maana yake kudanganya, kuiba na hata kudhulumu kwako ni jambo la kawaida. Sasa chukulia hali kwamba unadanganya, maana yake inabidi uwe na kumbukumbu sana kwenye maisha yako la sivyo utaishia kuumbuka mbele za watu. Sasa maisha ya kukazana kuweka kumbukumbu ya mambo gani umeshadanganya sio maisha rahisi.
Kama wewe ni mwizi, au jambazi, au fisadi au mtoa/mpokea rushwa wote maisha yenu hayawezi kuwa rahisi. Kuna wakati ambapo utalazimika kufanya mambo mabaya sana hata ikiwemo kuua ili tu kupata kile unachotaka au kutunza siri yako kubwa. Haya sio maisha rahisi.
Kama sio mwaminifu kwenye ndoa yako, maisha yako yanakuwa magumu sana. Utajikuta unalinda simu kama benki, unakwenda kuoga na simu, mara uweke neno la siri, mara udanganye majina ya watu na vitu vingine vingi vya ajabu. Haya sio maisha rahisi kuishi, yanachukua sana nguvu zako na yanakufanya ushindwe kuangalia lengo la msingi kwenye maisha yako.
Kuwa na maisha rahisi, maisha ambayo kila mtu akiyaangalia hapati wasi wasi wowote na mafanikio kwako yatakuwa ndio yamefika nyumbani. Yaani hayataondoka kamwe.
3. UAMINIFU HULETA UPENDELEO.
Ukiwa mwaminifu utapendelewa kwenye kila nafasi. Kama unafanya kazi, mwajiri atapenda kumpa nafasi zaidi yule ambaye ni mwaminifu, kuliko yule ambaye sio mwaminifu. Kama huelewi haya mambo unaweza kusema fulani anapendelewa ila ukichunguza kwa undani utakuta mtu huyo ana uaminifu zaidi kushinda wengine.
Kama umejiajiri au kufanya biashara nafasi nyingi zitakuja kwako zaidi ya wale ambao sio waaminifu. Wasiojua hili watasema unapendelewa au una bahati, ila ukweli ni jinsi ambavyo umejijengea uaminifu wako.
Kwa haya machache tunaweza kuhitimisha kwamba kama unataka mafanikio, kuwa mwaminifu. Kama hutaki mafanikio, endelea tu kutokuwa mwaminifu, utazunguka kila kona na kila ukifanikiwa kuyaona mafanikio yanakuponyoka, yanakimbia na inabidi uanze tena kuyatafuta. Ila unapokuw amwaminifu ukishayapata mafanikio, huna haja ya kuyazuia kwa nguvu ili yasiondoke, bali yenyewe yanafurahi kwa sababu yamefika nyumbani.
Nakutakia kila la kheri.
TUPO PAMOJA.