Kama upo humu kwenye KISIMA CHA MAARIFA hasa GOLD MEMBER mpaka sasa unatakiwa uwe umeshaanza kuwa WORLD CLASS. Kuwa WORLD CLASS kwenye jambo lolote unalofanya, kwa sababu kuwa chini ya hapo ni sawa na unapoteza muda wako.

Dunia tunayoishi sasa ina changamoto nyingi sana. Kazi unayoifanya kuna watu wengi sana wanaoweza kuifanya. Biashara unayoifanya kuna watu wengi sana wanaoweza kuifanya. Sasa kama utaendelea kuifanya kwa kawaida tu, unajitengenezea hatari kubwa sana ya kujikuta umeachwa nyuma au umewekwa pembeni kabisa.

Leo hapa tutajadili sheria namba moja ya wewe kuwa WORLD CLASS, yaani kufanya kile unachofanya kama ambavyo haijawahi kabisa kufanywa tokea dunia imeanzishwa na hakuna atakayeweza kuja kufanya miaka yote ijayo.

Unafikiri haiwezekani? Inawezekana sana kwa sababu kila mmoja wetu ni tofauti, wewe ni wa pekee una uwezo wa tofauti kabisa na mtu mwingine yoyote. Kama ukiujua na kuweza kutumia uwezo huu, utashangaa mambadiliko makubwa sana yatakayotokea kwenye maisha yako.

WORLD CLASS KWENYE KAZI.

Kama umeajiriwa au unafanya kazi yoyote ya mtu, huna ujanja zaidi ya kuwa WORLD CLASS. Sina haja ya kukueleza ni kwa nini kwa sababu kila mtu anaona jinsi ambavyo nafasi za kazi ni chache huku wanaozitafuta ni wengi. Kama ukifanya kawaida, unakuwa rahisi kuondolewa na kupachikwa mwingine ambaye anaweza kufanya kama unavyofanya wewe.

Katika hali hii msaada pekee kwako ni kuwa WORLD CLASS.

Ili kuwa WORLD CLASS kwenye kazi yako kwanza jua majukumu unayotakiwa kutekeleza. Uzuri wa ajira ni kwamba unapoajiriwa unapewa job description, yaani utaambiwa ni nini unachotakiwa kukamilisha unapokuwa kwenye kazi zako. Lakini ni wachache sana wanaokuja kusoma job description zao baada ya kuanza kazi. Wengi wanaingia kwenye kazi kwa mazoea na kuendelea kufanya kazi kama wanavyofanya wengine. Wakati mwingine mtu anapoanza na kuwa na hamasa ya kazi, wakongwe kazini wanamkatisha tamaa na kumwambia anajisumbua bure.

Sasa wewe kama WORLD CLASS usiingie kwenye mtego huu, jua unachotegemewa kukikamilisha, halafu kikamilishe. Kwa kukikamilisha vizuri bado hujawa WORLD CLASS, WORLD CLASS inakuja pale ambapo utakwenda hatua ya ziada. Utakamilisha majukumu yako, halafu unakwenda mbali zaidi, unafanya kwa hatua ya ziada, ambayo inaongeza thamani zaidi na thamani yako inakua.

Sehemu nzuri ya kwenda hatua ya ziada ni kuangalia matatizo ambayo yanaikabili sehemu yako ya kazi. Baada ya kujua matatizo haya yafanyie kazi, angalia ni jinsi gani unaweza kushauri na ukaleta mabadiliko makubwa. Kama ukilichukua tatizo, na kujipa utaratubu wa kuandika mawazo kumi au ishirini ya kutatua tatizo hilo, utakuja na njia nyingi sana za kuweza kulitatua.

Tafuta njia ya kutatua matatizo yanayoikabili sehemu yako ya kazi na utaleta mapinduzi makubwa kwenye kazi yako na kwenye maisha yako.

WORLD CLASS KWENYE BIASHARA/UJASIRIAMALI/KUJIAJIRI.

Changamoto ya biashara/ujasiriamali/kujiajiri ni kwamba kuna watu wengi sana ambao wanafanya unachofanya. Na wengine wengi wanaendelea kuja. Hivyo kama hutakuwa WORLD CLASS, kama hutafanya kwa utofauti, upekee na ubora wa hali ya juu sana, utaishia kwenye ushindani wa kijinga ambao utakuumiza kichwa na kukufanya ushindwe kufikia mafanikio.

Uzuri wa biashara au kujiajiri ni kwamba unakutana na mteja moja kw amoja, na mteja ndio anachagua. Anaweza kununua kwako, anaweza kununua kwa mpinzani wako na anaweza asinunue kabisa. Ni kitu gani unachoweza kufanya, bila ya kutumia nguvu na ukamfanya mteja anunue kwako leo, aje anunue tena kesho na awaambie wenzake wote waje wanunue kwako? Hii ndio WORLD CLASS.

Mpe mteja hali ambayo hajawahi kuipata popote. Kama mteja alitegemea kwa anacholipa atapata bidhaa au huduma kiasi fulani, nenda hatua ya ziada, mashangaze mteja mpaka aone kwamba alicholipa ni kidogo ukilinganisha na alichopata. Kumridhisha huku mteja sio lazima umuuzie kwa bei ndogo, au kumpa bidhaa/huduma nyingi bali jinsi ambavyo unamfanya ajisikie kwa kufanya na wewe biashara, hii ndio muhimu sana kwako na kwa biashara yako.

Mjue mteja wako vizuri, ijue vizuri bidhaa au huduma anayotaka na jua ni jinsi gani itaweza kutatua matatizo yake. Pia kuwa mshauri mzuri kwa mteja wako na kuwa mwaminifu, kama kuna kitu huwezi ni vyema ukawa wazi na kumwambia huwezi au hufanyi. Hii itakujengea heshima na wakati mwingine atajua ni nininunaweza au unafanya.

Usilalamike tena kwamba kwenye kazi yako wenzako wanapewa nafasi ila wewe unabadiwa. Usilalamike tena kwamba biashara yako ina kisirani, au umeligwa au wenzako wanatumia kizizi na wewe hutumiii. Vyote hivi vinaanza na wewe, hivyo unapokuwa WORLD CLASS unaamua ufikie mafanikio makubwa kiasi gani.

Kumbuka pia WORLD CLASS inaambatana na kujifunz akila siku. Na tabia zote za mafanikio tulizojifunza mpaka sasa zinahusika sana, zizingatie. Uvumilivu pia ni muhimu sana maana mambo haya yanahitaji muda.

Nakutakia kila la kheri wewe ambaye tayari ni WORLD CLASS.

TUPO PAMOJA