Zamani kidogo, kabla taasisi za kifedha hazijawa nyingi hapa nchini, kupata mkopo ilikuwa ni kazi kubwa sana. Ulihitaji kuwa na sifa nyingi zinazokuwezesha kupata mkopo na hata ukiwa nazo bado ulihitaji kusubiri mlolongo mrefu ndio uweze kupata mkopo unaohitaji.
Sasa hivi mambo yamebadilika sana, taasisi za kifedha zimekuwa nyingi sana na zinatoa huduma za mikopo kwa urahisi sana. Huhitaji kuwa na sifa nyingi sana ndio uweze kupata mkopo na hata ukihitaji mkopo wenyewe haikuchukui muda mrefu. Kuna taasisi nyingine unaweza kuondoka na mkopo wako siku hiyo hiyo ambayo umeomba.
Urahisi huu wa kupatikana kwa mikopo, je unakufanya na wewe uone unahitaji kupata mkopo? Au unahitaji mkopo ambao kweli una matumizi nao. Leo tutajadili jambo hili muhimu ili kuepuka matatizo yanayowakabili wengi hasa baada ya kuingia kwenye mikopo.
Mikopo ya kibiashara ni mizuri sana kama utajua jinsi ya kuitumia vizuri. Ila mikopo hii inaweza kuwamibaya sana na ikapelekea hata biashara yako kufa kama hutaweza kuitumia vizuri. Kuna watu wengi sana wamenufaika na mikopo na kuna wengine wengi ambao hawataki kusikia hilo neno mikopo, kwa sababu imewaharibia sana biashara zao. Haijalishi uko upande upi, tatizo kubwa sio mkopo unaopewa ila tatizo kubwa liko kwako wewe mwenyewe.
Sasa utajuaje kama biashara yako kweli inahitaji mkopo?
Kwanza kabisa mkopo wa biashara utakaoufurahia ni ule unaochukua kukuza biashara na sio kuanza biashara. Hili liko wazi kwa sababu biashara zina changamoto kubwa ambazo huwezi kuzijua mpaka uingie. Hivyo unapoingia kwa mkopo halafu ukakutana na changamoto unajiweka sehemu mbaya sana. Hivyo kigezo chako cha kwanza cha kushukua mkopo wa biashara ni uwe tayari umeshaanza biashara husika.
Pili biashara iwe inajiendesha kwa faida. Kama biashara inajiendesha kwa hasara maana yake kuna tatizo ambalo linaendelea kwenye biashara yako ambalo linanyonya fedha. Sasa ukikimbilia kuchukua mkopo kabla hujatatua tatizo hilo unakuja kupoteza fedha nyingi zaidi. Yaani ni sawa na uwe na ndoo ambayo inavuja ila ina maji kidogo, ukiongeza maji mengi zaidi inavuja zaidi. Kama biashara yako inaendeshwa kwa hasara kaa chini kwanza ujue hasara inatokea wapi kabla hujachukua mkopo.
Tatu kuna sehemu yenye faida kubwa ila haijitoshelezi. Baada ya kuwa kwenye biashara na kuona biashara yako inajiendesha kwa faida kuna baadhi ya maeneo ya biashara yako utaona hayajitoshelezi. Kwa mfano kunakuwa na bidhaa ambayo inatoka sana kila ukileta inaisha na watu wanaiulizia sana ila wewe huna uwezo wa kununua kiasi cha kutosha. Katika hali hii ukichukua mkopo unajua moja kwa moja unakuja kuongeza bidhaa hii ambayo inatoka sana.
Nne biashara inahitaji kutanuka zaidi. Kama umeanza biashara yako na umeshaweza kuiendesha vizuri unafika wakati ambapo unahitaji kutanua biashara yako zaidi. Inawezekana unataka kuitanua kwa hapo hapo ulipo au kufungua matawi sehemu nyingine. Katika hali hii mkopo utakusaidia sana kuweza kufikia lengo lako kwa kuwa tayari umeshabobea kwenye biashara hiyo. Kama biashara yako bado inakusumbua, usikimbilie kuitanua, tatua kwanza matatizo uliyonayo sasa.
Tano mkopo unaopata hautaweza kuutumia wote. Kigezo kingine muhimu sana cha wewe kuchukua mkopo lazima iwe mkopo unaopata hutoutumia wote. Yaani kama hitaji lako la fedha ni milioni kumi, mkopo wako usiwe hiyo milioni kumi kamili. Mkopo unaochukua inabidi utumie kiasi na kiasi uweke pembeni kwa ajili ya kuokoa pale mambo yatakapokwenda hovyo. Huombei mambo yaende vibaya, ila hakuna ambaye ana uhakika na jambo litakalotokea kesho. Unaweza kuwa unaijua biashara yako vizuri ila kukatokea kitu ambacho kipo nje ya uwezo wako na ukapata matatizo. Sasa unaokuwa hujatumia mkopo wote unakuwa na pa kuanzia pale mambo yanapokwenda vibaya.
Mikopo kwenye biashara ni mizuri kama wewe mwenyewe ni mzuri kwenye biashara yako. Kama bado unajiona hujawa vizuri chukua muda kwanza wa kujifunza na kufanya biashara yako kwa ubora kabla hujaingia kwenye mkopo.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
TUPO PAMOJA.