Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu THINK AND GROW RICH, leo tutachambua sehemu ya hatua ya sita ya kufikia utajiri ambayo ni Kuwa na mpango ulioandaliwa vizuri. Kupata makala zilizopita za uchambuzi wa kitabu hiki bonyeza hayo maandishi ya jina la kitabu.

Mpaka sasa umejifunza ya kwamba kitu chochote mtu anachotengeneza au kupata kinaanza na hamu au shauku ya kuwa na kitu hko. Na kiti kinaanza kama wazo ambalo linajengewa picha  na baadae mipango inabadili wazo hilo kuwa kitu halisi.

Ili uweze kufikia kile unachotaka unahitaji kuwa na watu ambao mtakwenda nao pamoja. Unaweza kuwapata watu hao kwa njia ifuatayo;

1. Ungana na watu ambao wana mawazo kama ya kwako na ambao wataweza kukusaidia kuweza kufikia mafanikio unayotarajia kuyafanya. Kundi hili la watu linaitwa MASTER MIND.

2. Kabla ya kutengeneza MASTER MIND, jua ni faida gani utakazopata kwa kuwa kwenye kundi hilo na ni kitu gani utakachotoa ambacho kitawanufaisha wengine waliopo kwenye kundi hilo. Hakuna mtu anayeweza kukubali kufanya kazi bila ya kupata malipo yoyote, japo malipo yanaweza yasiwe fedha.

3. Panga kukutana na watu hawa angalau mara mbili kwa wiki au mara nyingi iwezekanavyo mpaka pale mtakapokuwa mmeweka mpango mzuri wa kufikia utajiri.

4. Tengeneza uaminifu na maelewano mazuri kati yako na wengine waliopo kwenye MASTER MIND. Kushindwa kufanya hivi kutapelekea kundi hili kuvunjika.

SHIKA SANA MAMBO HAYA MAWILI;

KWANZA; Sasa hivi unajihusisha na jambo muhimu sana kwenye maisha yako. Kuwa na uhakika wa mafanikio, unahitaji mipango ambayo haina makosa.

PILI; Unahitaji kuwa na uzoefu, elimu, uwezo binafsi na taswira za wengine.  Hizi ni njia zilizotumiwa na watu wote ambao waliweza kujijengea utajiri mkubwa.

Hakuna mtu mwenye uzoefu wa kutosha, elimu ya kutosha na hata uwezo mkubwa wa kuweza kufikia utajiri mkubwa peke yake. Ndio maana ni muhimu sana kupata vitu hivi kutoka kwa wengine ambao utakuwa nao kwenye MASTER MIND GROUP. Unaweza kuandaa mipango yako mwenyewe lakini ni muhimu kuwashirikisha watu wa MASTER MIND ili waidhibitishe na kukupatia ushauri na marekebisho muhimu.

Kama mpango wa kwanza ulioweka hautazaa matunda, tengeneza mpango mwingine. Kama na huu nao utashindwa, tengeneza mwingine tena. Na kama na huu utashindwa kukupatia unachotaka tengeneza mwingine tena. Endelea kutengeneza mipango mizuri mpaka pale utakapopata unachotaka. Na hiki ndio kinachowashinda watu wengi, hiki ndio kinazuia watu wengi kufikia mafanikio, kushindwa kuwa na ung’ang’anizi wa kutengeneza mipango mipya baada ya ile ya mwanzo kushindwa.

Mtu mwenye akili sana hawezi kupata mafanikio na utajiri kama hatakuwa na mipango anayoweza kuifanyia kazi. Na mipango inaposhindwa sio ndio kushindwa bali ni changamoto ya kuvuka. Wakati mwingine inakufundisha kwamba mpango uliokuwa nao sio mzuri kama ulivyofikiria, hivyo unahitaji kupanga tena upya.

Hakuna mtu ambaye amewahi kufikia utajiri mkubwa bila ya kukutana na changamoto ambazo zilimfanya aweke mipango mipya. Unapokutana na changamoto usikimbie, jua kwamba mipango yako sio imara na hivyo unahitaji kujipanga tena. Endelea kufanya hivyo mpaka pale utakapofikia utajiri unaotaka. Ukikubali changamoto zikukatishe utakuwa mtu wa kukata tamaa.

Kumbuka; mtu anayekata tamaa kamwe hafanikiwi na mtu anayefanikiwa kamwe hakati tamaa.

Ishike sana hiyo kauli hapo juu na iandike mahali ambapo utaweza kuiona kila siku kabla ya kulala na pale unapoamka. Itakusaidia sana kuendelea na mapambano hata pale mambo yatakapokuwa magumu. Kama ambavyo Edison alivyoweza kuendelea na mipango yake ya kutengeneza taa hata baada ya kushindwa zaidi ya mara elfu kumi. Na wewe pia usikate tamaa mpaka pale utakapopata unachotaka.

Wakati unachagua watu wa kuwa nao kwenye MASTER MIND chagua watu ambao hawawezi kukatishwa tamaa haraka, yaani hawawezi kukatishwa tamaa kabisa.

Tukutane sehemu ya pili ya uchambuzi huu wa hatua ya sita ya kufikia utajiri.

Nakutakia kila la kheri kwenye maisha ya utajiri unayoishi.

TUPO PAMOJA.