Karibu kwenye kipengele hiki cha jinsi ya kujijengea tabia za mafanikio na mwezi huu wa tatu tunajijengea tabia ya kuweka kipaumbele kwenye maisha yetu. Tunaishi kwenye dunia yenye kelele nyingi sana, bila ya kuw ana kipaumbele unaweza kuona muda unakwenda huku hujafanya chochote cha maana.
Katika makala hii ya leo tutaona jinsi unavyoweza kujijengea kipaumbele kwenye maisha yako.
Kwanza kabisa kabla hujajua jinsi ya kujijengea kipaumbele unahitaji uwe na malengo ambayo umeyaelezea vizuri. Malengo haya ndio yatakuwa nguzo yako ya kujua ufanye nini na kwa wakati gani. Kama huna malengo nasikitika kukuambia kwamba utakachoendelea kusoma hapa hakitakusaidia kwa njia yoyote ile.
Kama bado huna malengo, hebu kaa chini leo na uweke lengo moja tu, halafu ligawe katika mipangilio utakayofanya kila siku ili kulitimiza.
Mbinu ya kuweka kipaumbele tutakayojadili hapa inafanya kazi kwa siku, yaani unaangalia mipango yako yote ya siku na mambo mengine yanayoibuka kwenye siku yako. Kupitia mipango hii au mambo yanayoibuka ni muhimu sana kujua ni kipi unafanya na kipi hutafanya. Na hata kwenye vile ambavyo utafanya ni muhimu kujua utaanza na kipi na kumaliza na kipi.
Katika kuweka kipaumbele kwenye maisha yako na kazi zako, tutatumia picha ifuatayo;
JINSI YA KUTUMIA MCHORO HUO NA KUWEKA KIPAUMBELE.
Kwanza kabisa jua mambo yote unayofanya kila siku. Kila kitu unachokifanya kiorodheshe maana kinatumia muda wako. Katika kitu chochote ambacho unakifanya, kuna vipimo viwili; muhimu na haraka. Kuna vitu ambayo ni muhimu kufanya na ambavyo sio muhimu. Na kuna vitu ambavyo ni vya haraka kufanya na ambavyo havihitaji haraka.
Pili chora kwenye karatasi mchoro unaofanana na huo hapo juu na andika hayo maelezo kama yalivyoandikwa, ila usiweke hiyo mifano. Baada ya kufanya hivyo sasa tunakwenda kuchambua eneo moja moja kati ya maeneo hayo manne.
ENEO LA KWANZA; MUHIMU NA HARAKA.
Haya ni mambo ambayo ni muhimu sana kuyafanya na unahitaji kuyafanya haraka. Mambo haya ndio yanayotakiwa kupewa kipaumbele cha kwanza maana ndio ya muhimu sana kwako. Mambo haya ni yale yatakayokuletea manufa zaidi kwenye chochote unachofanya. Yajue mambo haya ni yapi na yaorodheshe kwenye jedwali lake. Katika siku yoyote hakikisha unaanza na mambo haya na utakapoyakamilisha ndio unaweza kuenda kwenye mambo mengine.
ENEO LA PILI; MUHIMU LAKINI SIO HARAKA.
Haya pia ni mambo ambayo ni muhimu kuyafanya lakini hayana haraka sana. Unatakiwa kuw amakini sana na mambo haya kwani husahaulika kufanyika na baadae kuja kuwa muhimu na haraka sana. Haya ni mambo ambayo yatakuwezesha kufikia mafanikio makubwa sana baadae, yatakayokuandalia mazingira mazuri ya kufanya kazi zako vizuri baadae. Haya ni mambo ambayo unatakiwa kuyapangia ratiba maalumu ya kuyafanya kila siku na kufuata ratiba hiyo. Bila kufanya hivi unaweza kuona kama muda upo, ila unapokwisha ndio unaona madhara yake.
ENEO LA TATU; HARAKA LAKINI SIO MUHIMU.
Haya ni mambo ambayo ungependa kuyafanya lakini sio muhimu kwenye kazi au biashara yako. Haya ni mambo ambayo yanaweza kutumia muda wako mwingi ila uzalishaji wake ni mdogo sana ukilinganisha na muda unaoweka. Na pia haya ni mambo ambayo unaweza kuyakabidhi kwa watu wengine na wakayafanya vizuri. Yjue mambo hayo kwenye kazi na maisha yako na kisha tafuta mtu anayeweza kuyafanya vizuri na mpe ayafanye. Utaokoa muda wako mwingi ambao utaweza kuutumia kwenye mambo mengine ya uzalishaji zaidi.
ENEO LA NNE; SIO MUHIMU NA SIO HARAKA.
Haya ni mambo ya kupoteza muda tu. Yaani hayana umuhimu wowote na wla hayana haraka ya kufanya. Mambo kama kubishana vitu visivyo na msingi, kupiga soga, umbeya na majungu, na hata kutembelea mitandoa ya kijamii kila mara. Unatakiw akuacha mambo haya mara moja ili uokoe muda wako na uutumie kufanya mambo ambayo ni muhimu na haraka au mambo ambayo ni muhimu lakini sio haraka.
Kamilisha jedwali lako na lifuate kila siku kwa kuangalia ni kipi muhimu unatakiwa kuanza nacho kwenye siku yako. Kwa kushindwa kutumia jedwali hili, utajikuta unafanya kila jambo ambalo linajitokeza mbele yako, kitu ambacho kitakufanya uchoke sana na huku ukiwa huna jambo lolote kubwa ambalo unakuwa umekamilisha.
Muda ni muhimu sana, usipouwekea kipaumbele utashindwa kujua umepotelea wapi.
Nakutakia kila la kheri katika kuweka kipaumbele kwenye maisha yako.
TUPO PAMOJA.