Wewe kama mjasiriamali kipato chako kinategemea mauzo ya bidhaa au huduma unayotoa. Hii ni sawa na kusema kwmaba kama huuzi basi huna biashara na kama huna biashara maana yake upo kwenye hali mbaya sana kifedha. Vile vile katika ujasiriamali, kipato hakilingani siku zote, kuna wakati ambao utakuwa na kipato kikubwa kutokana na mauzo mazuri na kuna wakati ambao utakuwa na kipato kidogo kutokana na mauzo kidogo. Leo tutaangalia mambo muhimu ya kufanya pale ambapo mauzo yako yanashuka ili uweze kuepuka kuingia kwenye matatizo makubwa ya kifedha.
Jua chanzo cha mauzo yako kushuka. Kabla hujapanga ufanye nini ni muhimu sana kujua chanzo cha tatizo la kipato kushuka au kuwa chini. Kama unaijua biashara yako vizuri ni lazima utakuwa unajua ni maeneo gani ambayo hayafanyi vizuri. Huenda kuna bidhaa au huduma ambayo haiendani na wateja wako. Au ni kipindi ambacho msimu hauendani na bidhaa au huduma unayotoa. Pia inawezekana kuna mabadiliko uliyofanya kwenye biashara yako ambayo yamechangia tatizo hilo, kama kupandisha bei, kubadili bidhaa au huduma na mengine. Unapojua tatizo lako vizuri itakuwezesha wewe kuchukua hatua ambazo zitakuwezesha kuondokana na tatizo ulilonalo.
Baada ya kujua tatizo ambalo limesababisha kushuka kwa mauzo sasa unaweza kupanga ni hatua gani utachukua. Kama tatizo ni msimu, basi badili bidhaa au huduma unazotoa ziendane na msimu uliopo kwa wakati huo. Kama tatizo ni mabadiliko uliyofanya kwenye biashara, angalia ni jinsi gani unaweza kufanya mabadiliko hayo yapokelewe vizuri kwa wateja wako. Kama umepandisha bei basi hakikisha na kiwango cha bidhaa au huduma wanachopata wateja kinaendana na ongezeko la bei. Watu wapo tayari kulipia bidhaa au huduma ambayo itatatua matatizo yako kwa kiwango wanachotaka wao. Kama kuna mpangilio wowote ambao umebadili kwenye biashara yako angalia ni jinsi gani unaweza kuufanya uonekane kuwa bora zaidi. Kuwa makini sana usije kuacha mabadiliko uliyofanya na kurudi nyuma, yaani kufanya kile ambacho ulikuwa unafanya mwanzo. Utapoteza wateja wengi zaidi kwa sababu watashindwa kukuamini, Cha msingi sana ni wewe kuwafanya wateja wajisikie bado wanapata huduma nzuri sana na tena iliyozidi kuliko ilivyokuwa kabla ya mabadiliko.
Kujua chanzo cha tatizo na kuanz akulifanyia kazi hakuta leta majibu haraka haraka, huo ni mchakato ambao utachukua muda kulingana na ukubwa wa chanzo cha tatizo lenyewe. Wakati mchakato huu unaendelea, kuna mambo muhimu unayohitaji kufanya ili usiendelee kupoteza fedha zaidi. Kwa sababu mpaka sasa mauzo yapo chini na huenda unaendesha biashara kwa hasara. Zifuatazo ni hatua muhimu unazotakiwa kuchukua mara moja wakati unaendelea kushughulikia tatizo lako la mauzo kushuka;
1. Punguza gharama za biashara. Kutegemea na biashara unayofanya, punguza gharama ambazo sio za msingi kwa sasa. Unapokuwa kwenye hali ya hatari hakikisha mambo unayofanya ni yale ambayo ni muhimu sana kwenye kuendesha biashara yako. Hata mwili wako unapokuwa na ugonjwa mkubwa, hupeleka damu maeneo muhimu kwanza kama moyo na ubongo. Na wewe fanya hivyo, hakkisha gharama unazoingia ni zile ambazo ni muhimu sana kwa maendeleo ya biashara yako, nyingine achana nazo kwa sasa.
2. Kuza soko lako. Hii pia itakuwezesha kukuza biashara yako zaidi. Huenda kilichosababisha mauzo yako kushuka ni mpinzani ambaye amefungua biashara karibu na pale ulipo. Kwa mfano wewe ndio ulikuwa mfanyabiashara pekee na sasa kaja mtu mwingine, ni wazi kwamba mauzo yako yatashuka. Hatua muhimu ya kufanya hapo ni kuangalia jinsi unavyoweza kukuza wigo wa soko lako, kuwafikia watu wengi zaidi ya unaowafikia sasa. Kila biashara inayo nafasio ya kukua kuliko ilipofikia sasa, hivyo tumia nafasi hiyo.
3. Boresha zaidi biashara yako. Hatua ya mwisho tutakayojadili hapa ni wewe kuboresha zaidi biashara yako kwa kuboresha bidhaa au huduma unayotoa. Angalia ni kitu ganio ukiongeza kwenye bidhaa au huduma unayotoa kitawavutia wateja wengi zaidi. Hata kama ni kitu kidogo kinaweza kuwa na maana kubwa sana kwa wateja wako.
Kila biashara inapitia nyakati ngumu, mauzo kuwa chini na kipato kuwa kidogo. Kitakachokupitisha kipindi hiki salama ni mipango yako kizuri na kuzingatia hayo tuliyojadili hapo juu. Ukishindwa unakuwa sehemu ya watu waliojaribu biashara na wakashindwa. Usikubali kuwa sehemu hii, weka juhudi na nina hakika utafanikiwa. Kila la kheri.
TUPO PAMOJA.