Kama tulivyoona kwenye makala zilizopita kwenye tabia hii ya kujiwekea kipaumbele, kuba faida nyingi sana za kujiwekea kipaumbele kwenye maisha yako. Tuliona jinsi ambavyo dunia ya sasa imejaa kelele nyingi hivyo kama hujachagua kitu kimoja cha kufanya utajikuta unafanya kila kinachojitokeza mbele yako.
Leo katika makala hii kwenye kipengele hiki cha kujijengea tabia za mafanikio tutaangalia uhusiano kati ya tabia ya kuweka kipaumbele na kufikia mafanikio makubwa.
Kwa kuanza tunaweza kusema watu wote wanaofikia mafanikio makubwa ni wale ambao wanaweza kujiwekea kipaumbele na kuheshimu maamuzi yao. Hawa ni watu ambao wanajua ni kitu gani muhimu sana kwao na wamejitoa ili kupata kitu hiko muhimu. Watu waliofanikiwa wanajua kwmaba muda ni mfupi na pia thamani yake ni kubwa hivyo bila ya kuweka kipaumbele ni vigumu sana kuwa na matumizi mazuri ya muda huu. Kipaumbele kinawawezesha kujua ni kitu gani wanafanya na kwa muda gani. Na kitu hiki kinakuwa muhimu sana kwao ili kuweza kufikia mafanikio makubwa.
Akili ya binadamu haiwezi kufanya mambo mawili au zaidi kwa wakati mmoja na kuyakamilisha kwa usahihi. Japokuwa wengi wetu tumekuwa tukiona kufanya hivyo ni kuokoa muda ila ukweli ni kwmaba ni kupunguza ufanisi na ubora wa kile ambacho unafanya. Akili ya binadamu inaweza kushikilia jambo moja kwa wakati na kulifanya kwa ufanisi mkubwa. Unapofanya mambo mengi kwa wakati mmoja, unaifanya akili ishindwe kujua ni lipi jambo muhimu na hivyo kupunguza ufanisi. Kama ufanisi wako ni mdogo, kama ubora wako ni mdogo basi unaweza kuwa na uhakika kwmaba huwezi kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Ili kufikia mafanikio makubwa unahitaji kuwa bora sana kwa kile ambacho unafanya. Unahitaji kutoa kazi ambayo itakuwa na thamani kubwa kwa yule anayekwenda kuitumia. Ili kupata ufanisi huu unahitaji kuweka kipaumbele ili uweze kufanya jambo moja kwa wakati mmoja.
Mtu anayekimbiza sungura wawili anakamata wangapi? Jibu ni hakamati hata mmoja. Nadhani hili halina ubishi. Unapokimbiza sungura wawili kwa wakati mmoja itakuwia vigumu sana kukamata hata mmoja. Lakini ukiamua kumkimbiza sungura mmoja tu, nafasi ya kumkamata ni kubwa sana hasa pale juhudi zako zinapokuwa kubwa. Hii pia ni kweli kwa kazi na biashara zetu. Unaweza kuoana kwa kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja ni faida kwako, ila ukweli ni kwmaba ungekuwa unafanya jambo moja kwa wakati mmoja ungepata manufaa makubwa zaidi. Kuweka kipaumbele kunakuwezesha kuweka mawazo yakoyote sehemu moja na kutoa thamani kubwa.
Kitu kingine kikubwa tunachoweza kuzungumzia hapa nu nguvu. Tunaweza kufanya kile ambacho tunafanya, na pia tunaweza kufikiri kwa sababu tuna nguvu. Nguvu hii ndio inayotuwezesha kuchukua hatua mbalimbali kwenye maisha yetu na kutuwezesha kufikia mafanikio makubwa. Kwa bahati mbaya sana nguvu huu haipo sawa kila wakati ndani ya siku moja. Unapoamka asubuhi unakuw ana nguvu kubwa ambayo unaweza kuitumia kufanya mambo vizuri. Kadiri muda unavyokwenda kwenye siku, nguvu hii inapungua na mwisho wa siku ambayo ni jioni unakuwa huna nguvu kabisa. Au nguvu unayokuwa nayo inakuwa kidogo sana kiasi cha kukufanya ushindwe hata kufanya mamauzi ya msingi. Ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako, unahitaji kuweza kutumia nguvu zako vizuri. Na njia bora itakayokuwezesha kutumia nguvu zako vizuri ni kuwa na kipaumbele. Lazima uianze siku yako kwa kufanya yale mambo ambayo ni muhimu sana kwako. Ukianza siku kw akufanya mambo ambayo sio muhimu, unamaliza nguvu zako na baadae unapotaka kufanya yale ambayo ni muhimu unakosa nguvu za kuyafanya na kujikuta unayaahirisha.
Kama huwezi kuweka kipaumbele kwenye maisha yako, basi umechagua kutokufikia mafanikio makubwa. Ili ufikie mafanikio makubw aunahitaji kuchagua mambo machache utakayokomaa nayo na pia unahitaji kuwa na matumizi mazuri ya nguvu zako. Yote haya utayaweza ikiwa utakuwa na kipaumbele kwenye maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika kuweka kipaumbele kwenye maisha yako.
TUPO PAMOJA.