Jinsi Ya Kujijengea Uwezo Wa Kujiamini – 2

Ndugu msomaji karibu tena katika mwendelezo wa makala yangu ya namna ya kujijengea uwezo wa kujiamini. Naamini ulifaidika na machache kati ya mengi ambayo niliyaainisha katika juma lililopita. Nakukaribisha tena tuweze kuongeza ufahamu wetu kupitia jukwaa hili la JIONGEZE UFAHAMU.

Kama hukusoma makala ya wiki iliyopita isome kwa kubonyeza hapa; Jinsi Ya Kujijengea Uwezo Wa Kujiamini.

9. Tabasamu

Ninaposema tabasamu simaanishi kucheka bali ni hali ya kuonyesha bashasha usoni. Si tu kwamba kutabasamu kutaonyesha kwamba unajiamini bali pia huonyesha kwamba wewe ni mtu mwenye siha njema na hujasongwa na mawazo. Kutabasamu kutakusaidia kuonyesha kwamba wewe ni mkarimu. Ni rahisi zaidi kuwasiliana na mtu aliyetabasamu kuliko kinyume chake. Mtu kutokutabasamu inatuma ujumbe kwa watu kuwa yawezekana yeye hajiamini, mwoga au ana hasira na wakati mwingine husababisha mawasiliano yao na watu wengine kuwa magumu.

10. Mtazame unayeongea naye.

Hili tatizo la kushindwa kumtazama unayezungumza naye usoni linawakabili watu wengi, pengine mimi na wewe. Kumtazama unayeongea naye usoni huweza kutuma ujumbe kwamba uko makini na unayezungumza naye, unajali anachozungumza na kufurahishwa na mazungumzo yake. Pia huonyesha kwamba wewe unajiamini na siyo mwoga. Kumtazama unayezungumza naye haimaanishi kumkodolea macho muda wote kwani unaweza kumfanya akose kujiamini. Jifunze tabia hii kwani wataalamu husema kwamba macho ni lango la moyo na kupitia machoni unaweza kugundua mengi ikiwemo kujua kwamba yanayozungumzwa na msemaji ni ya kweli au uongo. Kumbuka kila mtu ana tabia ya kuona haya/aibu lakini inakupasa uishinde kwa mazoezi.

SOMA; Sheria Tatu Muhimu Za Kufanikiwa Kwenye Maisha.

11. Jiweke katika hali ya kutoogopwa

Jifunze kujiweka katika hali ya kufanya watu wawe rahisi kuzungumza na wewe. Kuna watu wamejitengenezea mazingira ya kuonyesha kwamba hawako tayari kuzungumza na watu. Watu hawa hujifanya kwamba wanatumia sana simu zao kwa kuongea ama ujumbe mfupi na mengine yanayofanana na hayo. Pia usipende kuzungusha miguu wala mikono yako kwani unatuma ujumbe kwamba hauko tayari kuzungumza. Kumbuka lugha ya alama huzungumza yaliyo ndani mwako hivyo chukua tahadhari. Ulivyo kwa nje inasadifu ulivyo kwa ndani.

12. Fahamu vipaji vyako

Kuna wakati ambao unaweza kujijisikia kukosa thamani. Katika kipindi hiki chukua kalamu na karatasi na uandike kuhusu vipaji vyako na vyote vizuri ulivyowahi kuvifanya. Achana na mabaya ama vitu ambavyo vitakufanya ujidharau. Kumbuka pongezi ulizowahi kupewa na ndugu, jamaa na hata marafiki. Jaribu kusahau mabaya yaliyosemwa juu yako na watu kwani hayana nafasi katika maisha yako. Kumbuka hata ukiwa mfano mbaya watu wengine wanaweza kujifunza kwa mfano wako. Kumbuka kuwa kama vile wewe usivyo mkamilifu ndivyo na watu wengine wasivyo. Fanyia kazi vipaji vyako na punguza au ondoa kabisa mabaya yako na kwa hali hii utakuwa mtu mwenye kujiamini sana. Kumbuka kujiambia kuwa wewe ni mshindi siku zote na acha kujihukumu.

SOMA; Haya Ndio Mambo Matatu Yatakayokuletea Matokeo Ya Kushangaza.

13. Kumbuka ulizaliwa ukijiamini

Unakumbuka ulipokuwa mtoto mchanga? Kipindi hicho ulikuwa mwenye kujiamini na ulifanya vitu uliyoona wewe vinafaa. Ulilia, ulitambaa, ulicheza na mengi kadhalika bila kumwogopa yeyote. Lengo langu kukumbusha haya ni ujue kuwa kutokujiamini kwako kumetokana na kuhukumiwa na watu na kunyooshewa vidole kila ulipokwenda. Lakini lililo jema zaidi ni kwamba kila mtu huja duniani bila kitu na hujifunza vyote hapa duniani. Kama vyote uliweza kujifunza unaweza pia kujifunza kujiamini na kuacha ama kusahau kutokujiamini.

14. Sio tatizo lako peke yako

Kuna msemo unasema kifo cha wengi ni harusi. Msemo huu unakusaidia kujua kuwa kila mtu hukabiliwa na matatizo kama wewe. Tatizo la kujiamini ni la dunia nzima. Kila mtu hukabiliwa na tatizo hili ila wengine wamejifunza kulishinda tatizo hilo na kulificha kwenye macho ya jamii. Kiukweli kila mtu huwa jambo analojiamini kwayo na yapo mengine mengi ambayo wanashindwa kujiamini. La muhimu zaidi acha kujifananisha na watu wengine kwani haya ni maisha yako na hupaswi kuwa sawa na mtu fulani. Hupaswi kuwa sahihi zaidi, mjanja zaidi ama mzuri zaidi bali kuwa mwenye furaha zaidi. Kumbuka kuwa kuweza kujiamini si suala la siku moja na huhitaji muda zaidi. Kuna siku waweza kushindwa lakini usife moyo, jaribu tena na tena.

SOMA; Hizi Ndizo Gharama Unazotakiwa Kuzilipia, Ili Uweze Kupata Kile Unachokihitaji Katika Maisha Yako.

15. Saidia wengine

Kusaidia watu wengine kutakuongezea uwezo wa kujiamini zaidi. Saidia pale unapoweza, pongeza panapostahili na punguza kuhukumu wengine. Kama kuna mtu anahitaji msaada wako jaribu kumsaidia hata kama hajakuomba kwani kuna watu wengine ni waoga wa kuomba msaada. Hii itakusaidia kujiamini, kujenga urafiki na pia kufungua milango ya wewe kusaidiwa kwani kadiri unavyotoa ndivyo unavyopokea. Utajisikia vizuri sana pale utakapojua kuwa Fulani kafanikiwa kwa sababu yangu pia.

16. Achana na wanakufanya ukose kujiamini.

Kuna watu katika hii dunia hupenda kuhukumu wengine kwa kila jambo walifanyalo liwe zuri au baya. Watu wa namna hii kaa nao mbali kwani siku zote utakuwa mdogo tu kwao na hutaweza kujiamini. Hawa hutafuta makosa na mapungufu yako siku zote. Kaa nao mbali kama wenye ugonjwa wa ebola lakini si kuwachukia. Chagua marafiki ambao watakufanya ujisikie vizuri katika ubora wako. Tabia na mafanikio yako huchangiwa kwa kiasi kikubwa na watu unatumia nao muda wako mwingi.

SOMA; Haya Ndio Matumizi Mazuri Ya Mshahara Wako Ambayo Yatakuletea Furaha Na Mafanikio.

17. Ongea na watu wageni kwako

Kujiamini ni zaidi ya kusoma ama kujifunza kupitia vitabu na makala, hii ni tabia ambayo hujifunzwa. Jifunze kuongea na watu wageni usoni kwako kwani huwezi kujua ni wapi utawahitaji. Itakuwia vigumu mwanzoni lakini baadaye utazoea kadiri siku zinavyokwenda na kadiri unavyoongea na wageni. Kuongea na watu usiowafahamu pia ni ukarimu.

18. Tegemea mafanikio

Katika kila jambo unalofanya tegemea mafanikio. Watu wengi sana hushindwa jambo kabla ya kulijaribu, kwa maana nyingine hushindwa mchezo nje ya uwanja. Ukitegemea kushindwa hutaweza kulifanya jambo kwa jitihada kwani huwezi kwenda mbali zaidi ya unavyowaza. Hivyo basi katika kujiamini amini pia kwamba inawezekana. Inawezekana anza sasa, usiahirishe kwani kamwe hutafanya ama utafanya katika hali ya taharuki.

Asante kwa kuuungana nami katika makala hii, tupo pamoja.

Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes ambae ni mjasirimali na mhamasishaji.

Unaweza kuwasiliana na naye kwa: simu: 0712 843030/0753 843030

e-mail: nmyohanes@gmail.com Pia unaweza kutembelea blogu yake: www.lifeadventurestz.blogspot.com kujifunza zaidi.

Makala imehaririwa kwa Kiswahili fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na Mjasiriamali Email: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s