Njia bora kabisa ya kutangaza biashara yako ni kushawishi mtu anayenunua kwako au mteja wako kuwaambia wengine kuhusu biashara yako. Yaani mteja wako anapata huduma au bidhaa kwako na anapokuwa na ndugu na jamaa zake anakuwa tayari kuwaambia kama mnataka huduma fulani, nendeni sehemu fulani(yaani kwako).

Hii ni njia bora ya kutangaza biashara yako na haina gharama kubwa. Ubora wake ni kwamba watu wanawaamini sana watu wao wa karibu. Kama rafiki yangu ataniambia kuna sehemu naweza kupata huduma nzuri ninayohitaji, nitamwamini zaidi yeye kuliko matangazo ninayoyaona. Hii ni kwa sababu kama rafiki yangu ametumia huduma hiyo na akaipenda, nitaamini na mimi nitaipenda pia.

SOMA; Siri Kubwa Unayotakiwa Kujua Kwenye Mahusiano Ya Kibiashara.

Pamoja na uzuri wa matangazo haya, watu wengi hawafanyi hivyo. Watu wengi inakuwa vigumu sana kwao kuwaambia wengine kuhusiana na biashara yako. Na baadhi ya vitu vinavyowafanya washindwe kufanya hivyo ni hivi hapa;

1. Kutokuwa na uhakika. Wanafikiria je kama nikimwambia mtu aende kwenye biashara hii ana uhakika wa kupata huduma nzuri kama nilivyopata mimi?

Jinsi ya kuepuka kikwazo hiki ni kutoa huduma bora sana na wakati wote. Hakikisha kila mata unatoa huduma zitakazomridhisha mteja. Kama leo mteja akipata huduma nzuri, kesho akapata huduma mbovu hawezi kuwa na uhakika na huduma zako.

SOMA; UKURASA WA 11; Watu Hawa Wanakurudisha Nyuma.

2. Kuhofia ataonekanaje. Kitu kingine kinachowazuia watu kutoa taarifa za bioashara yako kwa wengine ni kuhofia wataonekanaje kwa kusema kuhusu biashara yako. Wakati mwingine wanaweza kuoana watadharauliwa au wanawezaje kuwashauri wengine kupata huduma sehemu kama hiyo.

Jinsi ya kuepuka hili ni kutengeneza hadithi nzuri ya biashara yako na ambayo itamfanya kila mtu kupenda kuwa sehemu ya hadithi hiyo. Kujua jinsi ya kutengeneza hadithi ya biashara yako soma hapa; BIASHARA LEO; Umuhimu Wa Hadithi Ya Biashara Yako.

3. Kuthaminiwa kwa juhudi zao. Kitu kingine ambacho kinawafanya watu kushindwa kutoa taarifa za biashara yako kwa wengine ni kutokuwa na uhakika kama juhudi zao zitathaminiwa. Mtu anaweza kuwapa watu taarifa za biashara yako lakini anapokuja kwenye biashara haoni kama juhudi zake zinathaminiwa.

Unaweza kuepuka hili kwa kuthamini juhudi zinazofanywa na mteja katika kukuletea wateja wengi zaidi. Angalia njia ambayo unaweza kujua ni kiasi gani mteja ameleta wateja kwenye biashara yako na mpe zawadi kwa juhudi zake hizo. Utamhamasisha kuwaambia wengi zaidi kuhusiana na biashara yako.

Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.

Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.