Katika makala za nyuma hapa kwenye KISIMA CHA MAARIFA kwenye kipengele cha kujijengea tabia za mafanikio tumeshajadili sana kuhusu matumizi mazuri ya fedha. Tulijadili mengi sana na hatua kwa hatua jinsi ya kuongeza kpato, jinsi ya kupunguza matumizi na hata jinsi ya kuwekeza ili fedha zako ziweze kukuzalia zaidi na zaidi na zaidi.

Lakini kama wote tunavyojua, matumizi ya fedha bado ni changamoto kubwa kwa wengi. Na ndio maana fedha inabaki kuwa msingi wa matatizo karibu yote duniani. Kuna ambao wanayo na hawajui waitumieje na kuna ambao hawana na hawajui waipateje.

Changamoto zote ambazo unapitia kuhusu fedha zinatokana na kitu kimoja kilichopo ndani yako; TABIA. Tabia zako kuhusu fedha ndio zinakufanya ujikute kwenye wakati mgumu kifedha kila mara. Na kama utakuwa na tabia nzuri basi utaweza kuondokana na sehemu kubwa ya matatizo haya ya kifedha.

Leo hapa kwenye WORLD CLASS tutakumbushana machache kuhusu fedha ili isiendelee kuwa kikwazo kwetu katika kufikia yale malengo yetu makubwa kwenye maisha. Hivi hapa ni vitu kumi muhimu vya kujifunz akw aharaka kuhusu matumizi yako ya fedha na maisha yako kwa ujumla.

1. Ondokana na madeni yote.

Hasa kama madeni haya hayazalishi. Madeni ni sumu kubwa sana kwako kufikia uhuru w akifedha. Kama bado unaingia kwenye madeni ambayo hayazalishi maana yake umeamua kupoteza fedha mwenyewe. Yaani ni sawa na kuweka maji kwenye kikapu, yataingia ila yatavuja na kuisha yote. Unapokuwa mtu wa madeni mifuko yako inaanza kuvujisha fedha, kila fedha utakayoweka itaondoka haraka na kwenda kulipa deni. Ukishalipa deni unaanza tena kukopa. Ondokana na mchezo huu wa kukopa kwa kuanza kupunguza matumizi ambayo sio ya msingi. Angalia kila njia ya kufanya ila kwepa sana kukopa fedha ambayo huendi kuitumia kuzalisha, utakuw aunapoteza fedha zako mwenyewe.

2. Kama ukinunua kitu kilipie mara moja.

Ili kuepuka kuingia kwenye madeni mapya ambayo yataendelea kukupotezea fedha, pale unaponunua kitu kilipie mara moja. Kama huwezi kukilipia jiulize je kitu hiko ni muhimu sana na hakiwezi kusubiri? Kama ni muhimu sana umiza kichwa chako ni jinsi gani utapata fedha ya kulipia kitu hiko. Uzuri ni kwmaba ukiamua kuumiza akili yako ni lazima utapata majibu ya kile unachotaka, ila ukiamua kuilegeza itakupeleka kwenye njia rahisi ambayo ni kukopa.

3. Weka akiba kipato chako, usikitumie hovyo.

Nafikiri huu ndio msingi muhimu sana kuhusu fedha ambao utajifunza kila mara. Weka akiba, tena kabla hujafanya matumizi yoyote yale. Weka sehemu ya kipato chako kama akiba na baadae akiba hii unawez akuiwekeza kwenye miradi mbalimbali inayowez akukuzalishia baadae. Matumizi siku zote huwa hayaishi, hasa pale unapokuwa na fedha, Hivyo kuepuka kuona kila kitu ni muhimu unapokuwa na fedha, hebu anza kuweka kiasi cha fedha pembeni kwanza, kiasi kidogo utakachobaki nacho utalazimika kukitumia vizuri na hii itakuondolea kufanya vitu ambavyo sio muhimu saa kwako.

4.  Sahau kuhusu dili za kutajirika haraka.

Sahau kabisa na wala usitake kusikiliza huu ujinga. Unataka njia ya kuwa tajiri haraka? Haipo. Kama huamini nenda kacheze kamari, utaishia kuliwa fedha zako zote na kuwatajirisha wengine. Wazo lolote la kazi au biashara ambalo halioneshi thamani halisi inayotengenezwa sio wazo zuri na likimbie haraka sana. Ukion amtu anaanza kukushawishi kwamba kuna njia rahisi ya kupata utajiri, kimbia sana maana anataka kukuingiza kwenye shimo baya sana. Kwa binadamu wanavyopenda urahisi, kungekuwa na njia ya kweli ya haraka ya kupata utajiri, kila mtu angeshaijua na angeshaitumia, njia ya aina hii haipo ila ni njia rahisi kwa matapeli kupata fedha zao kutoka kw awajinga. Sasa wewe ni mjanja, usikubali kuingia kwneye hili.

5. Kuwa makini sana kwa unaowakopesha fedha.

Kama hukopeshi kibiashara, basi nawez akukuambia usikopeshe fedha. Kama kuna mtu ana shida sana ya fedha unawez akumsaidia, lakini sio kukopesha. Unapokopesha hasa kwa watu ambao ni wa karibu, unatengeneza nafasi kubwa sana ya kutokurudishowa fedha zako. Unaweza kukataa hili lakini fikiria kw amakini ni watu wangapi wamewahi kukukopa fedha ila ilipofikia kulipa ikawa tatizo. Tena wakati mwingine mnaweza hata kuvunja mahusiano mazuri mliyokuwa nayo awali. Narudia tena kwa msisitizo, kama hukopeshi kibiashara, ambapo utatumia sheria kudai deni lako, na mtu ataheshimu kwa sababu ni biashara, epuka sana kukopesha hasa kw awatu ambao ni wa karibu kwako. Kama mtu ana shida msaidie, vinginevyo, epuka kukopesha. Kukopesha fedha hovyo ni njia rahisi sana ya wewe kujitengenezea umasikini.

6. Ondoa kabisa tamaa ya kutajirika haraka.

Hakuna kitu kinachopatikana haraka ambacho kinadumu kwa mud amrefu. Kuna raha sana pale ambapo unatumia muda wako kujenga utajiri wako na baadae kufikia kiwango kikubwa sana. Unapokuwa na tamaa kubwa ya kutaka kutajirika haraka ni rahisi sana kuingia kwenye mtego wa matapeli na ukaibiwa fedha zako na kupotezewa muda pia. Usikubali mtu yeyote akuondoe kwenye lengo lako kubwa kwenye maisha, tayari umeshachagua biashara unayotaka kufanya komaa nayo hiyo na jenga utajiri kwa kubobea hapo. Njia nyingine rahisi itakupoteza.

7. Usijilinganishe na wengine, mengi unayoona sivyo yalivyo.

Kuna wakati unawez akuona watu wengine kama wana maisha mazuri sana. Unawaona wanaishi maisha ya kifahari, wanakuambia mambo yao ni mazuri sana na unaweza kuona kama wewe ndio maisha yako hujui unayapeleka wapi. Leo nakuambia ukweli ambao utakukomboa; SIO KILA KITU UNACHOKIONA KIPO KAMA UNAVYOKIONA NA SIO KILA KITU MTU ANACHOKUAMBIA NI UKWELI. Kila mtu anapenda maisha yake yaonekane yako bora, hivyo wengi hudanganya na kuonesha wako hivyo, ila kiuhalisia yale sio maisha yao. Ishi maisha yako, haya ya wengine achana nayo.

8. Nunua vitu ambavyo unaweza kuvimudu na unahitaji kweli kuwa navyo. Usinunue vitu kwa sababu kila mtu anacho au kwa sababu ndio fasheni mpya au kwa sababu ndio itaonesha na wewe upo. Vitu kama nyumba, magari, mavari na vitu vingine vya starehe usinunue kwa mkumbo. Angalia hitaji lako kweli na uwezo wako wa kumudu unachotaja kununua.

9. Fanya kazi kwa hamasa na mapenzi makubwa.

Toa thamani kubwa sana kwa mteja wako kama unafanya biashara. Hakikisha mteja wako hawezi kupata huduma unayotoa wewe sehemu nyingine yoyote. Hata kama huduma hiyo inapatikana kila mahali, wewe itoe kwa utofauti ambao utamfanya mteja aone hii kweli ni thamani ambayo atakuwa tayari kuilipia. Kama umeajiriwa hakikisha unatoa thamani kubwa sana kwa mwajiri wako. Tekeleza majukumu yako na nenda hatua ya ziada. Hii itakutengenezea nafasi ya kuongeza kipato chako zaidi na zaidi.

10. Hakikisha mwenzi wako naye anakuwa na tabia nzuri za kifedha.

Hapa ndio kuna changamoto kubwa. Wewe unawez akuwa na tabia nzuri sana kwenye fedha lakini mwenzi wako, yaani mke au mume akawa na tabia za hovyo sana kwenye matumizi ya fedha. Wewe unakazana kutunza mwenzako anakazana kutapanya. Kama tayari unaye mwenza wa aina hii kaa nae chini na msaidie kuondokana na tabia hii. Unaweza kuona anafanya makusudi ila kwa asilimia kubwa ni tabia ambayo huenda amekua nayo tokea akiwa mdogo. Kama bado hujawa na mwenza hakikisha mtu unayechagua kuishi naye ana tabia nzuri kwenye matumizi ya fedha.

Mambo yote ya fedha yanaanzia kwenye tabia, anza kutengeneza tabia zako na mambo yako yatakuwa mazuri.

Nakutakia kila la kheri katika kujenga tabia nzuri kifedha na kufikia utajiri na mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA.