Karibu kwenye kipengele hiki cha kujijengea tabia za mafanikio. Hizi ni tabia muhimu sana kwa kila mmoja wetu ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kama ambavyo wote tunajua, kila kitu kinaanza na tabia, hivyo unavyojenga tabia bora unajiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwez akuboresha maisha yako.
Mwezi huu wa nne tunajijengea tabia ya kuwa na shukrani. Hii ni tabia muhimu sana ambayo watu wengi wenye mafanikio wanayo. Katika makala ya leo tutaangalia faida za kujijengea tabia ya shukrani. Kwa nini ni muhimu sana kwako wewe kuwa na tabia ya shukrani kwenye maisha yako?
Zifuatazo ni faida za kuwa na tabia ya shukrani.
1. Kuyafurahia maisha.
Kama tunavyojua, furaha kwenye maisha yako inaanza na wewe mwenyewe, na haitoki kwa watu wala kwa vitu ambavyo unavyo. Kuna watu wana fedha na mali nyingi lakini hawana furaha na kuna watu ambao hawajui watakula nini kesho lakini wana furaha sana. Furaha kwenye maisha inatokana na wewe kufurahia yale maisha ambayo unayo, kushukuru kwa kila ambacho kinaendele akwenye maisha yako. Na hapa ndipo tabia ya shukrani inapokuwa muhimu sana. Kama unaweza kushukuru wka pumzi unayoendelea kuvuta, kwa kuweza kufikiri, kwa kuweza kupenda na kupendwa basi maisha yako yatakuwa bora sana.
2. Kupata yale ambayo ni mazuri zaidi.
Unapokuwa mtu wa shukrani maana yake unaangalia sana yale ambayo ni mazuri kwenye maisha yako. Na kama ambavyo tunajua, kile ambacho unaangalia sana ndio ambacho kinatokea kwenye maisha yako. Kile ambacho unakifikiria sana ndio kinatokea kwenye maisha yako. Hivyo unapoangalia yale mazuri na kushukuru unapata mazuri mengi zaidi. Jinsi unavyoendelea kushukuru ndivyo unavyozidi kupata zaidi na zaidi.
3. Kujiepusha na mabaya.
Hii ni kinyume na hapo juu. Yaani unapokuwa mtu wa shukrani, huweki mawazo yako kwenye mabaya, wewe unaangalia ni kipi kizuri cha kushukuru. Kwa kuepuka kufukiaia yale mabaya muda wote unaepuka kuyapata zaidi kwenye maisha yako. Kile unachofikiria kw amuda mrefu ndio kinachotokea. Watu wasiokuwa na shukrani ambao muda wote wanaona matatizo tu huendelea kupata matatizo zaidi na zaidi.
4. Kuwa mvumilivu.
Tabia ya shukrani inakusaidia kuwa mvumilivu kwenye maisha. Kwa kuweza kushukuru wka vitu vidogo na kujua wkamba vikubwa vinakuja kunakuongezea uvumilivu wako. Pia kunakupa imani kwamba hakuna kinachoshindikana. Watu wote ambao wana tabia ya kushukuru ni watu ambao wana mtizamo chanya juu ya maisha yako na kile wanachofanya.
5. Kufikia mafanikio.
Hakuna mafanikio yanayokuja haraka, au yanayokuja kwa wakati mmoja. Mafanikio yanakuja kidogo kidogo na kwa muda mrefu. Unapokuwa mtu wa shukrani, utakuwa tayari kupokea mafanikio haya madogo madogo na hivyo kujiandaa kupokea yale makubwa zaidi. Ukikosa tabia ya shukrani utadharau haya madogo na kukata tamaa na hii itakuondoa kwenye njia ya mafanikio.
Tabia ya shukrani ina faida nyingi sana kwenye maisha yako. Jenga tabia hii ili uweze kuboresha maisha yako na kufikia mafanikio makubwa.
TUPO PAMOJA.