Mara nyingi huwa tunafanya mambo kwa mazoea. Na kutokana na mazoea hayo tunasahau kwamba matokeo ya kile tunachofanya yanaweza kuwa mabaya sana kwenye biashara zetu.

Kuna njia uliyozoea kufanya biashara yako ambapo kwa njia hiyo unafukuza wateja wengi zaidi ya wale ambao unawakaribisha. Na hii imekuwa inaumiza biashara yako kidogo kidogo na siku moja utashindwa kuendelea kabisa.

SOMA; Dunia Ya Wingi Na Dunia Ya Uhaba…

Kama hujui au umesahau, leo tukumbushane kidogo njia kumi rahisi za kufukuza wateja kwenye baishara yako.

1. Usijali kuhusu mteja, akija sawa, asipokuja sawa. Hata atakapofika usimuoneshe kwamba yeye ni wa muhimu kwenye biashara yako.

2. Jali kuhusu faida tu, mambo mengine hayana maana kwako.

3. Muahidi mteja kitu ambacho huwezi kukitimiza, na hakikisha analipia kitu hiko, japo hatokipata.

4. Anzisha ligi na mteja, akilalamika muoneshe kwamba hayo ni matatizo yake na sio yako.

5. Usijibu malalamiko ya wateja, watajua wenyewe.

SOMA; Jambo Moja Muhimu La Kuzingatia Ili Uwe Tajiri.

6. Mteja akishanunua bidhaa au huduma yako, asirudi tena kulalamika, hakuna garantii, akiondoka ndio imetoka.

7. Usitengeneze mazingira rahisi kwa mteja kupata kile anachotaka, fanya amzingira yawe magumu, mteja atajua mwenyewe, si ana akili. Atashindwaje kujua?

8. Kama mteja hanunui asikusumbue. Atakujaje kuulizia vitu vingi halafu hanunui?

9. Ongea na mteja huku unaongea na simu, au unachata, upo facebook, upo wasap, hata hivyo ujumbe unaojibu sasa ni muhimu kuliko mteja.

10. Mwambie mteja hujui kuhusu maswali anayokuuliza yanayohusiana na bidhaa au huduma unayotoa. Hujali kujua itamsaidiaje mteja, sio kazi yako, kwani ni wewe unatumia?

Haya ni baadhi ya mambo ambayo unaweza kujikuta unafanya ila yana madhara makubwa sana kwenye biashara yako. Yapo mengi ya aina hii, nina hakika umeshaanza kufikiria na mengine. Acha kufanya mambo haya au endelea kufanya kwa sababu biashara yenyewe unajaribu tu, hivyo unatafuta sababu kwa nini ishindwe.

Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.

Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.