Kama Wewe Ni Kijana Unayataka Mafanikio,..Huu Ndio Ukweli Unaotakiwa Kuujua Ili Kufanikiwa.

Inawezekana unasoma makala hii ukiwa ndio kwanza ni kijana uliyemaliza chuo na unasubiria kupata kazi lakini hupati kazi yenyewe kama ulivyokuwa ukifikiria awali. Inawezekana pia unasoma makala hii huku ukiwa umechoshwa na kazi unayoifanya na huitamani tena. Inawezekana hata pia unasoma makala hii ukiwa umekata tamaa na umekosa tumaini kubwa la kukufanya kusonga mbele katika maisha yako.

 
Upo uwezekano mkubwa ukawa katika hali tofauti tofauti ambazo zote hizo zinakukatisha tamaa na unaona kama huwezi kusonga mbele tena katika maisha yako. Natambua ukiwa kama kijana mwenzangu wa kitanzania unatamani kuona mambo yako yakiwa mazuri, ukiwa una kwako na kuweza kumiliki miradi muhimu uliyojipangilia binafsi. Lakini cha kushangaza huoni mambo yako yakienda kama unavyotaka.
Umekuwa ukiumiza kichwa kujiuliza ufanye nini? ni kweli uko sahihi kwa sababu umeamua kupigania maisha yako. Pamoja na harakati zote hizo lakini umejikuta ukiwa mtu wa kushindwa  kusonga mbele zaidi kama unavyotaka iwe. Katika makala ya leo nataka kuongea na wewe kijana wa kitanzania ambaye pengine umemaliza chuo hivi karibuni na huna kazi, ila una kiu kubwa ya kufanikiwa.
Nataka kuongea na wewe nikupe ukweli, hata kama utakuuma lakini utakusaidia kujua ni mambo gani hasa yanayokuzuia wewe kuweza kufanikiwa, ingawa una uwezo mkubwa wa kufanikiwa ndani yako. Sitaki kuona ukaendelea kuteseka na kuishi maisha unaishi. Ninachotaka kuona kwako maisha yako yanabadilika na kuwa ya mafanikio. Ni muhimu sana kuujua ukweli huu ukiwa kama kijana ili uweze kufanikiwa zaidi na kutoka hapo ulipo mpaka leo. Je, unajua ni ukweli gani?
1. Acha kutafuta mafanikio ya haraka sana.
Hili ni moja ya kosa kubwa ambalo wewe ukiwa kama kijana umekuwa ukilifanya na ndilo linalokuzuia kufikia mafanikio makubwa ni kwa sababu ya kutaka mafanikio ya haraka yaje kwako. Mara nyingi umekuwa ukifikiri unaweza kupata mafanikio kwa haraka zaidi. Na hizi ndizo fikra ambazo vijana wengi wamekuwa nazo katika maisha yao.
Kama utaendeleza fikra hizi ni wazi kuwa utazidi kukwama na utakuwa unajirudisha nyuma wewe mwenyewe. Katika ukweli wa mafanikio, hakuna kitu kinachoitwa mafanikio ya haraka. Mafanikio yote huanza kwa utaratibu na kuweka misingi imara itakayosimama. Hakuna mafanikio ya kulala leo maskini na kuamka kesho tajiri.
Kwa kuwa umelijua hili kuwa makini zaidi. Jiwekee mipango na malengo yako vizuri, kisha anza utekelezaji. Kukaa tu na kutaka mafanikio ya haraka hiyo itakuwa ndoto kwako. Watu wote unawaona wamefanikiwa hawakuanza jana ama leo kama unavyofikiri, walijipanga na kutengeneza mafanikio. Hicho ndicho kitu unachotakiwa ukifanye ili ufanikiwe.
2. Acha kuogopa kuchekwa kwa kile unachotaka kufanya.
Mara nyingi umekuwa na fikra za kuogopa kuchekwa kila unapojifikiria kufanya kazi ya aina fulani. Na hili linasababishwa hasa kila unapoangalia elimu uliyonayo unakuwa unajihisi huwezi kufanya kazi fulani kwa sababu ni ya watu wa chini sana katika maisha.
Kwa kuhofia kwako kuchekwa hivyo ndivyo ambavyo umekuwa ukizidi kujichelewesha kufikia malengo yako. Kumbuka kazi ni kazi, kama utaendelea kuogopa watu katika maisha yako kuwa watakucheka kwa jambo unalotaka kulifanya utakuwa unajichelewesha mwenyewe kufanikiwa.
Tambua maisha yako ni maisha yako wewe, usimuogope mtu na kuhisi kuwa atakucheka eti kwa sababu unafanya kitu fulani. Hata ikitokea wamekucheka hiyo  haitasaidia kitu endelea na maisha yako. Kuwa na fikra chanya, achana na mawazo potofu ya vijana wenzako ya kuamini kuchekwa. Ukiendekeza ugonjwa huu wa kuogopa kuchekwa, hakika huwezi kufanikiwa.  
3. Acha tabia ya  kupoteza muda wako sana.
Kuna wakati unaweza usifanikiwe sio kwa sababu huna malengo na mipango mizuri uliyojiwekea ila ni kwa sababu unapoteza muda mwingi katika mambo yasiyo ya msingi na  ya lazima katika upande wa maisha yetu. Na hili ndilo moja ya kosa kubwa wanalofanya vijana na linawazuia kufanikiwa.
Ni ukweli uliowazi ukiwa kijana umekuwa ukipoteza muda mwingi sana kwenye mitandao ya kijamii ambapo ukiangalia kwa makini hakuna unachokifanya huko kikubwa zaidi ya kupoteza muda wako wa thamani ambapo pengine ungeweza kuutumia kukuzalishia.
Kama unataka kugeuza maisha yako na kuwa ya mafanikio zaidi acha kuchezea muda wako kama unavyofanya sasa. Acha kujivunia ujana ulionao kwa kuamini unao muda wa kutosha. Mapinduzi makubwa juu ya maisha yako unatakiwa uyafanye ukiwa bado kijana. Sasa huwezi kuleta mabadiliko kama utakuwa ni mtu wa kupoteza muda sana. Pangilia muda wako vizuri kisha fuata malengo yako.
4. Acha kusikiliza ushauri mbaya juu ya maisha yako.
Mara nyingi umekuwa ukijaribu kutafuta ushauri karibu kwa kila mtu juu ya maisha yako. Hilo linaweza likawa ni sawa lakini mbaya zaidi umekuwa ukipewa ushauri ambao haukusaidii ama kwa namna moja au nyingine umekuwa ukikukatisha sana tamaa.
Wengi kati ya watu unaowaomba ushauri wamekuwa wakikwambia ama kukueleza kuwa huwezi kufanikiwa kama unavyotaka na wamekuwa wakikupa sababu zinazoonyesha ni kweli huwezi kufanikiwa katika maisha yako, wakati kitu ambacho kinaweza kisiwe kweli.
Kama unataka kufanikiwa ukiwa kama kijana na utoke hapo ulipo ni lazima sana kwako kuanzia sasa kuweza kujua kwamba ni muhimu kuwa na ushauri chanya wenye lengo la kubadilisha maisha yako. Usibebe kila wazo linalokupa ushari na kuamini ndilo sahihi, utakwama.
5. Acha kuishi na watu wasio sahihi kwako.
Maisha yako kwa sehemu kubwa umekuwa ukiyafanya kuwa magumu kutokana na kushikilia marafiki wengi ambao sio msaada kwako. Hebu jaribu kuchunguza wewe mwenyewe marafiki ulionao wanakusaidia vipi kukufikisha kule unakotaka kufika katika maisha yako.
Utakuja kugundua kuwa marafiki wengi ulionao ni walewale ambao hawana msaada sana kwako zaidi ya kukurudisha nyuma kimafanikio. Ukiwa katika hali hii upo kwenye hatari kubwa sana, kwani mara nyingi marafiki zako wana nguvu kubwa sana ya kubadili maisha yako kuliko unavyofikiri.
Ili kuweza kubadilisha maisha yako ni lazima kwako kubadili mwelekeo haraka sana na kuchagua marafiki watakaoweza kukusaidia kufanikisha malengo yako kwa sehemu kubwa. Ukiweza kufanya hivyo utakuwa umejiweka kwenye nafasi kubwa sana ya kuweza kufanikiwa.
Kwa kifupi, hayo ndiyo mambo ambayo yamekuwa yakikuzuia kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako. Ili uweze kubadilisha maisha yako ni lazima kwako kuweza kuchukua hatua sahihi, zitakazoweza kukutoa hapo ulipo na kukufikisha kwenye mafanikio halisi.
Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO ili kuweza kujifunza na kubadilisha maisha yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: