Nakumbuka zamani kidogo, ulikuwa kama umezoea kununua vitu kwenye duka moja, na siku kitu ulichokuwa unataka hukukipata, ukaenda kwenye duka jingine ambapo mfanyabiashara anajua huwa unanunua wapi, angeweza kukataa kukuuzia.
Anaweza kukuambia kwamba kila siku unapita pale na kwenda kununua kwingine kwa nini leo uende kununua kwake. Mwingine anaweza kukataa kabisa kukuuzia kile unachotaka. Hali hii inakufanya wewe mteja ujione kama kununua sehemu fulani ni kosa kubwa kwako.
SOMA; Kwanini ni Muhimu kuwekeza kwa Muda Mrefu.
Sasa turudi kwako wewe mfanyabiashara, je na wewe unawachukia wateja ambao hawanunui kwako? Kila siku unamuona anapita na kwenda kununua kwa mwingine, halafu leo anakosa alichotaka kule na kuja kwako, je unampokea kwa furaha au unampokea kwa maneno makali kwamba mbona leo hujaenda ulikozoea kwenda?
Usimchukie mteja ambaye hanunui kwako, mteja ana haki ya kununua kokote nakotaka yeye, hela ni yake na ameitafuta kwa jasho lake. Na inapotokea akakosa huduma kule alikozoea na kuja kwako, mpokee kwa furaha sana. Mpatie huduma ambayo hajawahi kuipata kule alikozoea kwenda na hatakuwa na sababu ya kwenda kule tena.
Uzuri wetu binadamu ni kwamba hakuna asiyependa vitu vizuri. Hivyo kama utampatia huduma nzuri kuliko alizozoea kupata kwingine ataendelea kuja ili apate zaidi na zaidi.
SOMA; Jambo Moja Muhimu La Kuzingatia Ili Uweze Kufikia Malengo Yako.
Hivyo acha kupoteza wateja kwa kuendekeza hisia zako, ni kweli unaweza kuumia kwa nini mtu akupite na kwenda kununua kwingine. Ila kumbuka kila mtu ana uhuru na heshimu maamuzi yake. Hata kama mteja aliwahi kusema maneno mabaya kuhusu biashara yako, ila akaja na shida ya kupata huduma, mpatie huduma. Kwenye biashara hakuna uadui, bali kuna kufanikiwa na kushindwa.
Chukia wateja na utashindwa, penda wateja wote na utafanikiwa.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.
Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.