Changamoto nyingi sana tunazokutana nazo kwenye biashara zinaanza na sisi wenyewe. Yaani wewe mwenyewe ndio chanzo kikubwa cha matatizo unayokutana nayo kwenye biashara yako. Japo huwezi kukubali hili ila nasikitika kukutaarifu hivyo.

Biashara zinaposhindwa watu wanakuwa na sababu nyingi sana, uchumi mbaya, wateja hakuna, washindani ni wengi na kila aina ya sababu wanayoweza kufikiria. Ila wanasahau sababu moja ya msingi sana, wao wenyewe.

SOMA; Njia Rahisi Ya Wewe Kuondokana Na Tabia Usiyoipenda.

Sababu kubwa ya ndani ya mtu mwenyewe ya biashara kushindwa ni mtazamo ambao hauendani na mafanikio ya biashara. Wafanyabiashara wengi sana wana mitazamo hasi juu ya biashara kwa ujumla na hata maisha yao. Hawaamini kwamba mambo yanaweza kuwa mazuri kwa wao kufanya kile ambacho kinakubalika. Na mbaya zaidi mitazamo hiyo imekuwa kikwazo sana kwenye mafanikio yao ya kibiashara.

Nimewahi kumshauri mfanyabiashara mmoja ambaye biashara yake ilikuwa inaelekea kufa na yeye mwenyewe anaamini bila ya kudhulumu watu huwezi kufanikiwa kwenye biashara. Hivyo akawa anawalipa wafanyakazi kiasi kidogo sana ukilinganisha na kile wanachotengeneza na mambo mengine yasiyo ya uaminifu. Kilichotokea wafanyakazi nao wakaiga tabia ya mmiliki, wakawa wanamwibia yeye na wanawaibia wateja pia. Biashara ikawa inapata hasara na huku inapoteza wateja, ilikuwa inakufa kwa kasi ya ajabu.

SOMA; Jinsi Unavyoweza Kutumia Changamoto Kama Fursa Ya Kujifunza Zaidi.

Ukweli ni kwmaba kauli hiyo kwmaba bila ya kudhulumu wengine huwezi kufanikiwa kwenye biashara ni ya uongo. Na kidhibitisho cha kwanza kwamba ni ya uongo, wote utakaokuta wanatumia kauli hiyo ni watu ambao hawajafanikiwa kwenye biashara. Ni watu ambao biashara inawapa changamoto kubwa lakini bado wanaamini hawajadhulumu vizuri ndio maana wanapata changamoto. Hivyo wanadhulumu zaidi na hivyo kujichimbia zaidi kaburi la kifo cha biashara zao.

Uaminifu ni muhimu sana kwenye biashara kama unataka kufanikiwa. Kinyume na hapo sahau mafanikio kupitia biashara. Kuwa mwaminifu kwako binafsi, kuwa mwaminifu kwa wateja wako na kuwa mwaminifu kwa wafanyakazi wako na wale unaoshirikiana nao kwenye biashara.

SOMA; BIASHARA LEO; Usianze Biashara Upya Kila Siku…

Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.

Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.