Kwa haraka tu na bila ya kuzunguka zunguka nikuambie kwamba biashara unayofanya kama wewe sio namba moja, au sio namba mbili basi acha kupoteza muda wako kwenye hiyo biashara. Kama sio namba moja au namba mbili kwenye biashara unayofanya maana yake huna biashara yenye wateja wa kutosha, unapata wale wateja ambao wanakuja tu kwa sababu wameona unafanya biashara, na wakiondoka hawarudi tena.
Ninaposema namba moja simaanishi namba moja dunia nzima au nchi nzima au hata eneo zima ulilopo, hakuna biashara ya aina hii kwa sasa. Ila nataka biashara yako wewe iwe namba moja kwa wale wateja wako. Kama unaijua biashara yako vizuri maana yake unawajua wateja wako ni watu gani. Sasa kwa watu hawa uliowachagua kama wateja wako, hakikisha wewe ni namba moja kwao. Kwamba wanapofikiria kuhusiana na biashara unayofanya, moja kwa moja wewe ndio unaingia kwenye akili zao.
Kama sio namba moja, au namba mbili, maana yake hakuna anayekufikiria na hivyo kuna kosa kubwa unalifanya kwenye biashara yako, au hujaijua biashara yako. Hivyo angalia ni kitu gani unaweza kufanya ili kuwa namba moja, na kama umekuwa unafuatilia makala hizi kwa makini, tayari majibu unayo, ni wewe kuyafanyia kazi tu.
Nakuwaje namba moja kama ulisema nisishindane? Swali zuri, kama ndio unajiuliza hivi. Ndio nimekuwa nikiwaambia wafanyabiashara wasipoteze nguvu zao kwenye kushindana, badala yake watumie nguvu hizo kuwa bora zaidi. Hivyo wewe kazana kuwa bora, hakikisha mteja akija kwako anapata huduma ambayo hajawahi kuipata kwingine, na hapo utakuwa namba moja.
Kama biashara yako sio namba moja au namba mbili kwamba upo kwenye nafasi ya juu kwa wateja wako, unapoteza muda. Unahitaji kufanya mabadiliko ya haraka kama unataka kufanikiwa kupitia biashara hiyo.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.
Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.