Wafanyakazi wako ni watu muhimu sana kwenye biashara yako. Hawa ni watu ambao wataiwezesha biashara yako kufanikiwa au kushindwa. Wafanyabiashara wengi wamekuwa hawalipi uzito eneo la wafanyakazi. Wengi wamekuwa wakiajiri wafanyakazi kwa sababu tu ni rahisi kuwalipa na hawatawasumbua, hivyo wafanyakazi hawa wanakuwa hawana ujuzi wowote wa biashara. Kwa kufanya hivi mfanyabiashara anaweza kuona anaokoa gharama ila anajizuia sana kukua kwenye biashara yake na kufikia mafanikio makubwa.
Mfanyakazi yeyote anayehusika na biashara yako, hakikisha ana mafunzo sahihi ya kibiashara. Haijalishi mfanyakazi huyu ndio anahudumia wateja, au anafanya usafi au hata kuzalisha bidhaa unayouza. Wafanyakazi wako wote wanahitaji mafunzo sahihi ya biashara ambayo yatawahamasisha na pia kuwapa mbinu za ziada za kuongeza uzalishaji, kuwahudumia vizuri wateja na kuweka juhudi ili kuongeza thamani ya kazi zao.
Wewe kama mfanyabiashara ambaye unataka kupata mafanikio makubwa kupitia biashara yako, unahitaji kuhakikisha wafanyakazi wako wanapata mafunzo ya biashara. Mafunzo haya wanaweza kuyapata kwa kuwahamasisha wao binafsi kusoma vitabu vya biashara ambavyo utawanunulia au kutembelea mitandao inayotoa elimu ya biashara. Lakini mara nyingi wafanyakazi wako wanaweza wasihamasike sana kutafuta elimu hii kwa kujisomea wao wenyewe. Hapa unahitaji elimu ya ziada ambayo itawafanya waweze kuchukua hatua.
Elimu ya ziada inayohitajika hapa ni kuwaandalia mafunzo ya semina ambapo wote watahudhuria na kujifunza kwa pamoja. Mafunzo hayo yanatolewa na mtaalamu wa biashara ambaye atawapatia elimu ya biashara na atawahamasisha. Mafunzo ya aina hii ni muhimu sana, kama unataka kuibadili biashara yako. Kama biashara yako ina wafanyakazi, hata kama ni mmoja, hakikisha anapata mafunzo haya mara kwa mara. Unaweza kuona unapoteza gharama kubwa, lakini utavuna kikubwa sana ukilinganisha na kiwango ulichoweka.
Kama wafanyakazi wako hawana ujuzi wa biashara, hawana hamasa ya kufanya biashara hiyo, halafu wewe unafikiria kufikia mafanikio makubwa kwenye biashara hiyo, tunaweza kusema unajidanganya. Haijalishi wewe unaweka juhudi kubwa kiasi gani, unahitaji kuwa na timu nzuri ya watu wanaojua ni kitu gani wanafanya, wanaojiamini na wenye hamasa ya kuweka juhudi zaidi ili kuzalisha zaidi. Yote haya utayapata kwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wako mara kwa mara.
Kama utahitaji mtu wa kuwafundisha na kuwahamasisha wafanyakazi wako, wasiliana na mimi kwa mawasiliano yangu. Kuna programu nzuri sana kwa mafunzo ya wafanyakazi itakayowawezesha kuongeza uzalishaji wao na hivyo kukuza biashara yako.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.
Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.