Mpenzi msomaji wa KISIMA CHA MAARIFA, bado tunaendelea kujifunza tabia ya shukrani katika kipengele hiki cha kujijengea tabia za mafanikio. Baada ya kuona umuhimu na jinsi ya kujijengea tabia ya shukrani, leo tutaona uhusiano kati ya tabia ya shukrani na mafanikio makubwa.

Kama unavyojua, lengo la KISIMA CHA MAARIFA ni kukupa wewe maarifa ambayo yatakuwezesha kufikia mafanikio makubwa. Hivyo tabia ya shukrani ni moja ya vitu vitakavyokuwezesha wewe kufikia mafanikio hayo makubwa. Na kama tulivyoona kwenye kujijengea tabia hii ya shukrani, huhitaji fedha za ziada au msaada mkubwa ili kuweza kujenga tabia hii. Bali unahitaji kutambua kila kinachoendelea kwenye maisha yako na kukithamini.

Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya tabia ya shukrani na mafanikio. Kwa kifupi naweza kusema hakuna mafanikio kama hakuna tabia ya shukrani. Kwa nini naweza kusema hivi? Mtu ambaye ana tabia ya shukrani anaweza kuvumilia zaidi kuliko mtu ambaye hana tabia hii. Mtu mwenye tabia ya shukrani atakuwa tayari zaidi kujifunza kutokana na changamoto anazopitia na kurekebisha zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Mtu ambaye hana tabia ya shukrani atakosa uvumilivu na kukata tamaa hasa anapokutana na changamoto. Hii ni kwa sababu anaona zaidi yale yaliyo mabaya kuliko yaliyo mazuri.

Kwa tabia hizo mbili, uvumilivu na kujifunza kutokana na changamoto, tabia ya shukrani inawafanya watu kufikia mafanikio makubwa zaidi kuliko wale ambao hawana tabia hii. Mahitaji makubwa ya mtu yeyote kufikia mafanikio ni uvumilivu na kujifunza kutokana a changamoto ambazo mtu anazipitia. Ukiwa mtu wa kushukuru utakuwa na tabia hizi zaidi.

Tabia ya shukrani inawafanya watu wawe tayari kufanya kazi na wewe. Watu wenye tabia ya shukrani wanawahamasisha watu kufanya kazi nao na kujitoa zaidi. Kutokana na watu hao kuwa tayari kushukuru na kujali mchango wa kila mtu, wanawavutia watu wengi kuwa karibu nao. Hata nikikuuliza wewe utapenda kitu gani, kufanya kazi na mtu ambaye hana shukrani na mlalamikaji tu au kufanya kazi na mtu mwenye shukrani na kujali mchango wako? Moja kwa moja utapenda kufanya kazi na mtu mwenye tabia ya shukrani. Mafanikio yako yanategemea ni kiasi gani unaweza kuwashawishi watu wengi wafanye kazi na wewe. Jinsi ambavyo watu wengi wanakuwa tayari kushirikiana na wewe ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kupata kile ambacho unakitaka kwenye maisha yako. Kama unataka kuwahamasisha watu wengi zaidi wafanye kile unachoamini ni sahihi kufanyika, unahitaji kuwa na tabia ya shukrani.

Watu wenye tabia ya shukrani hupata zaidi kile wanachopata na hivyo kufikia mafanikio. Hakuna mafanikio yanayotokea kama mvua, kwamba umepanga kuwa bilionea halafu mara moja unakuwa bilionea, HAKUNA. Kila lengo utakaloliweka utapitia hatua ndogo ndogo sana ambazo unaweza kuona haziwezi kukufikisha kwenye lengo hilo. Unapokuwa na tabia ya shukrani unaelewa hatua hizi ndogo ndogo na kushukuru hivyo kuendelea kupata zaidi. Mtu anayekosa tabia ya shukrani atadharau hatua hizi ndogo ndogo na hivyo kuharibu nafasi yako ya kufikia lengo kubwa alilojiwekea. Kama lengo ni kuwa bilionea, mtu mwenye tabia ya shukrani, atashukuru hata pale atakapopata shilingi elfu kumi, ataitunza vizuri na kuizalisha zaidi ili kuweza kufikia lengo lake. Lakini mtu ambaye hana tabia ya shukrani ataona elfu kumi ni fedha ndogo sana na haiwezi kumfikisha kwenye lengo la kuwa bilionea na hivyo kuitumia hovyo. Kwa kuitumia hovyo anaondoa uwezekano wowote wa yeye kufikia lengo kubwa alilokuwa amejiwekea.

Tabia ya shukrani ni muhimu sana kwako kama unataka kufikia mafanikio makubwa. Ni sheria ya dunia kwamba yule anayeshukuru kwa kidogo alicho nacho anaendelea kupata zaidi. Hii ni kwa sababu atakuwa akifikiria kile alichopata na jinsi gani ya kukiongeza zaidi. Ila ambaye hana tabia ya shukrani anaendelea kukosa zaidi, hii ni kwa sababu anakuwa akifikiria sana kile anachokosa au alichopoteza na hivyo kuendelea kukosa na kupoteza zaidi.

Anza kuifanya tabia ya shukrani kuwa sehemu ya maisha yako, anza kidogo kidogo kwa kushukuru kwa kila jambo linalotokea kwenye maisha yako. Jifunze kwa kila jambo na kila siku orodhesha mambo matatu unayoshukuru kwa kuwa nayo kwenye maisha yako. Utaanza kuona mafanikio yakijionesha wazi wazi tofauti na ulivyokuwa kwamba huna tabia ya shukrani.

Nakutakia kila la kheri katika kuitumia tabia ya shukrani kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA.