Unapokuwa kwenye biashara, jukumu lako kubwa ni kumjua mteja wako kuliko hata anavyojijua wewe mwenyewe. Labda sio, lakini cha msingi lazima umjue mteja wako vizuri. Changamoto nyingi za biashara zinaanza pale mfanyabiashara anaposhindwa kumjua mteja wake vizuri na hivyo anashindwa kwenda naye vizuri kwenye biashara yake.
Kama unasema huna haja ya kumjua mteja kwa sababu atakuja tu, wewe unaendesha biashara yako kawaida na kwetu sisi KAWAIDA NI SAWA NA HOVYO. Yaani kama unafanya kitu kawaida maana yake unakifanya hovyo. Sisi tunafanya vitu vya tofauti, vitu vya kipekee ambavyo vinaleta majibu makubwa na ya tofauti. Ndio maana tunachukua hatua tofauti katika kufikia kile tunachotaka.
Eneo la kwanza muhimu analokwenda mteja wako na unatakiwa kulijua ni wapi anakwenda kabla ya kuja kwenye biashara yako. Yaani mteja wako anakwenda kwenye biashara gani kabla hajafika kwenye biashara yako? Hili ni eneo muhimu sana unalotakiwa kujua kwani litakuwezesha kukuza biashara yako zaidi.
Eneo la pili muhimu kujua ni wapi mteja wako anakwenda baada ya kutoka kwenye biashara yako. Jua mteja wako akishafanya biashara na wewe ni kwenye biashara gani anakwenda pia.
Kwa kujua maeneo haya mawili muhimu kutakuwezesha kujua njia za kumhudumia mteja wako vizuri na pia utajua watu muhimu wa kushirikiana nao kwenye biashara ili uweze kukuza biashara yako. Watu hawa wanaweza kuwa na wateja wengi ambao bado hawajaijua biashara yako. Hivyo unaweza kuwapata wateja hawa wengi zaidi.
Pia kama wateja wakitoka kwako wanakwenda kwa mfanyabiashara mwingine anayefanya biashara kama yako ni muhimu kujua ni kitu gani kinawapeleka kule. Na kama wanatoka kwenye biashara kama unayofanya wewe, jua ni kitu gani kimewatoa kule. Majibu haya utakayopata yatakuwezesha kuboresha biashara yako zaidi na zaidi.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.
Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.