Swali muhimu sana ambalo kila mmoja wetu anayetafuta mafanikio anatakiwa kujiuliza ni je kwa nini nayataka mafanikio? Kwa nini nafanya ninachofanya? Kwa nini wenzangu wanapokula raha mimi bado naendelea na kazi zangu? Kwa nini wengine wanapokuwa wamelala, mimi naamka na kuanza kujiandaa kuikabili dunia?

Haya ni maswali muhimu sana kila mmoja wetu anatakiwa kujiuliza na majibu ambayo tutayapata yatatuwezesha kujua kama kweli tutafikia mafanikio tunayotazamia au la. Sio kila sababu inayokufanya uweke juhudi za ziada itakufikisha kwenye mafanikio. Leo tutajifunza ni sababu zipi ambazo zitakufikisha kwenye mafanikio na zipi ambazo hazitakufikisha kwenye mafanikio.

Kwa kuwa wewe unataka kufikia mafanikio makubwa, kwa kuwa unataka kuwa WORLD CLASS kwenye kile unachofanya ni muhimu sana kuijua sababu ya msingi inayokufanya wewe uchague kuwa WORLD CLASS, sababu ambayo inakufanya wewe kutokukubali kuwa kawaida na kwenda hatua ya ziada.

Sababu moja maarufu na inayowatega wengi ni fedha. Unaweka juhudi zaidi kwa sababu unataka fedha zaidi. Unajifunza zaidi kwa sababu unataka kupata fedha zaidi. Unaamka asubuhi na mapema wakati dunia bado imelala kwa sababu unataka fedha zaidi. Sio kitu kibaya kutaka fedha zaidi kwa sababu fedha ni moja ya kipimo muhimu cha mafanikio. Tatizo ni pale ambapo fedha inakuwa ndio kitu pekee kinakusukuma kufanya kile unachofanya. Hapa unajiweka kwenye nafasi kubwa sana ya kushindwa au kukata tamaa na kuishia njiani.

Kwa nini kuweka fedha kama sababu ya wewe kufanikiwa kutakufanya ushindwe na kukata tamaa? Hii ni kwa sababu pale utakapoanza kuchekwa, na lazima hili litatokea itakuwa rahisi sana kwako kuona hata hivyo kuna vitu vingi vya kufanya na vikaniletea fedha. Pale utakapoanza kujishuku kama kweli unaweza kufanya kile unachotaka kufanya, utakapoanza kujiuliza kama kweli una uwezo wakufika kule ambapo unataka kufika, na hii pia itakutokea, itakuwa rahisi kwako kuona kama haupo bora kwenye hili kuna mambo mengi sana unaweza kuwa bora.

Changamoto ni kwamba hata kama utaacha hiko unachofanya na kwenda kuanza kufanya kitu kingine bado vitu hivi viwili vitakuandama popote unapokwenda. Watu watakucheka, watu watakukatisha tamaa, watu watakuambia huwezi na watu watakupa mifano ya watu wengi ambao walijaribu kama wewe na wakashindwa. Na wewe mwenyewe pia mambo yatakapokuwa magumu, na ni lazima yawe, utaanza kujiuliza mara mbili mbili, hivi naweza kweli? Hivyo kama msukumo pekee wa wewe kufanya ni fedha, nakuhakikishia hutofika mbali. Utagusa vitu vingi na kuacha na mwishowe kushindwa kupata fedha unazotazamia na hata kushindwa kupata mafanikio. Kupata fedha zaidi sio msukumo mzuri wa wewe kuwa bora sana kwenye kile unachofanya na kuwa na mafanikio makubwa?

Kama fedha sio msukumo mzuri, kama kupata fedha nyingi sio njia nzuri ya wewe kuwa WORLD CLASS, je ni kitu gani kitakufikisha kwenye mafanikio makubwa?

Kuna kitu kimoja ambacho kama utaweza kukifanya kuwa msukumo kwako kitakuwezesha kuwa WORLD CLASS na wakati huo pia kitakuwezesha kupata fedha nyingi sana. Yaani kwa kitu hiki fedha inakuwa sio lengo lako kubwa ila inakuja nyingi mpaka unaweza kushangaa ilikuwa imejificha wapi. Hiki ndio kitu kitakachokusukuma kufikia mafanikio makubwa sana. Hiki ndio kitakachokuwezesha kuendelea hata pale watu wanapokupinga na kukucheka. Hiki ni kitu kinachokuwezesha kuendelea hata pale mambo yanapokuwa magumu na kuhisi labda huwezi.

Kitu hiki ni mapenzi ya dhati kwa kile ambacho unakifanya. Kama unataka kuwa WORLD CLASS, kama unataka kufikia mafanikio makubwa na kama unataka kupata fedha nyingi basi una njia moja tu ya kufuata. Penda sana kile kitu ambacho unakifanya. Kichukulie kama sehemu ya maisha yako, kichukulie kama utambulisho wako. Wafanye watu wakikuona wasikuone wewe kama wewe tu, bali wakuone wewe kama mtu ambaye anafanya kile anachofanya.

Penda kile unachofanya kwa hatua kwamba huwezi kuacha kufanya kwa sababu ndio maisha yako hayo. Kama vile ambavyo huwezi kuacha kupumua, ndio iwe kwenye kile kitu ambacho unafanya. Weka akili yako, moyo wako na nguvu zako zote kuwa wa pekee na tofauti kabisa kwenye hiko unachofanya. Wakati wenzako wanaangalia ni saa ngapi muda unaisha ili wakafanye starehe au mapumziko wewe huna habari hizo. Wakati watu bado wamelala na kuvuta shuka, wewe unaamka asubuhi na mapema kujiweka vizuri kuhakikisha unakuwa bora sana.

Kwa mapenzi ya dhati hivi hakuna kitakachoweza kukuyumbisha, watu wakikucheka na kukukatisha tamaa, hutasikiliza na kuamua kuacha, bali utapata hasira ya kuwa bora zaidi ili kuwaonesha kwamba hawajui kile wanachosema. Pale unapoanza kujihisi mwenyewe kwamba labda haupo bora, labda huwezi kile unachotaka kufanya ndio inakupa hamasa ya kujifunza zaidi ili uweze kufanya kile ulichopanga kufanya. Kwa kufanya haya unajikuta unaendelea kuwa juu, unaendelea kuzalisha kazi ambayo ni bora sana na unajikuta unapata fedha nyingi sana.

Hivi ndivyo mafanikio yanavyokuja, hayaji kwa sababu unataka kupata fedha nyingi ila kwa sababu unafanya kitu ambacho unakipenda sana na huwezi kufikiria kufanya kitu kingine. Hiki ni kitu ambacho umeyatoa maisha yako kukifanya kwa ubora wa kipekee ambao haujawahi kufanywa na mtu mwingine yeyote. Na katika kufanya hivi unajiamini na kuwa na nidhamu ya kukuwezesha kufuata yale uliyojipangia kufanya.

Wewe kama mwana mafanikio, wewe kama WORLD CLASS nataka uondoke na kitu kimoja ambacho unakwenda kukitumia kwenye kazi yako au biashara yako. Kitu hiki ni kupenda sana kile kitu ambacho unakifanya. Ipende sana biashara unayofanya, ione biashara hiyo kama sehemu ya maisha yako, jione wewe kila unapoona kitu bora kinatoka kwenye biashara yako, na weka maisha yako yote kwenye biashara hiyo. Fedha hazitakuwa na ubishi tena. Kama unafanya kazi, penda sana kile unachofanya, usiwe kwenye kazi kwa sababu tu unapata kipato cha kuendesha maisha, hii ndio imefanya mamilioni ya watu kujikuta wamekwama kwenye mashimo ya kazi na hawaoni wanaelekea wapi. Wanaishi maisha ya kulipa madeni na kuanza kukopa tena, kila mwezi.

Maisha yako yana thamani kubwa sana zaidi ya kuamka asubuhi, kwenda kazini, kurudi jioni na kusubiri mwisho wa mwezi upokee mshahara na kulipa madeni halafu siku chache baadaye unaanza kukopa tena. Unaweza kuishi maisha zaidi ya haya kama utaamua kupenda kile ambacho unafanya. Hata kama kipato ni kidogo, hakitaongezeka kwa kufanya kwa kusukumwa. Bali kitaongezeka kwa wewe kupenda kile unachokifanya na kukifanya kwa utofauti. Hii itaongeza thamani sana kwenye kile unachofanya na moja kwa moja kipato chako kitaongezeka.

Najua wewe unataka mafanikio makubwa, najua wewe ni WORLD CLASS kwenye hiko unachofanya. Sasa jukumu lako kubwa ni kukipenda sana hiko unachofanya na ukione ni sehemu ya maisha yako. Mafanikio na fedha itakuwa ni kitu kidogo sana kwako kuhofia.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kuwa WORLD CLASS.

TUPO PAMOJA.