BIASHARA LEO; Kutojali Kwako Kunavyokuletea Hasara Kwenye Biashara.
Jana nilikuwa kwenye ofisi moja, mama mmoja akatoka kwenda kutoa fedha kwa njia ya simu na kununua vocha pia. Baada ya muda alirudi akiwa amekamilisha zoezi lake na kutaka kuingiza vocha kwenye simu. Alipoangalia akakuta amepewa vocha mara mbili ya alizoagiza. Alinunua vocha ya shilingi elfu mbili ila akawa amepewa vocha za shilingi elfu nne. Zilikunjwa mara mbili hivyo kuonekana kama elfu mbili wakati ni elfu nne.
Nilimwambia ni vyema arudishe vocha hizo zilizozidi, akafikiria kidogo akaniambia ni afadhali nitupe hizi vocha bila hata ya kuzitumia kuliko kuzirudisha pale niliponunua. Hili lilinipa shauku ya kujua zaidi, hivyo nikamuuliza kwa nini amefikia maamuzi hayo. Alinieleza kwamba alipata huduma mbovu sana, alifika eneo hilo na kukuta mabinti wawili wanaoneshana kitu kwenye simu. Anawaambia nataka kutoa fedha, akajibiwa, toa, halafu wakaendelea na mambo yao. Akauliza namba ya wakala ni ipi hakujibiwa, akauliza tena akaoneshwa kwa mkono hiyo hapo juu, na wakaendelea na mambo yao.
SOMA; Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.
Baada ya hapo alipewa fedha zake na akanunua vocha na kuondoka, huku akiwa amejisikia vibaya sana. Baada ya maelezo haya nilikosa nguvu ya kuendelea kumshawishi arudishe vocha iliyozidi. Lakini nilitoka na somo hili muhimu ninalokushirikisha hapa kuhusu biashara yako.
Wajali sana wateja wako, onesha huduma bora kwa wateja wako. Usimfanye mteja ajione kama amekosea kuja kwako, usione mteja kama amekuja kukuharibia starehe yako, huna starehe nyingine zaidi ya kumhudumia mteja wako vizuri.
Na kama umeajiri watu kwenye biashara yako, kwama ilivyo kwa hawa mabinti, hakikisha wanafanya kile ambacho ni muhimu ili kukuza biashara yako. Usiajiri wafanyakazi wa kuokoteza au utakaowalipa bei rahisi. Ajiri watu watakaopenda kufanya kazi unayowapa na wahamasishe wafanye zaidi. Pia wape mafunzo ya mara kwa mara ili wawe na hamasa kubwa kwenye kazi zao.
Usiendelee tena kufukuza wateja wako halafu uje kutulalamikia kwamba biashara ni ngumu.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.
Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.
Jiunge na COACHING/MENTORSHIP PROGRAM ambapo utapata muongozo wa hatua kwa hatua mpaka ufikie mafanikio kwenye kazi au biashara unayofanya. Bonyeza haya maandishi kupata maelekezo ya programu hii.