Karibu kwenye kipengele hiki cha uchambuzi wa vitabu ambapo kila wiki unapata uchambuzi wa kitabu kimoja kinachokupatia mbinu na maarifa ya kuweza kufikia mafanikio makubwa. Mchakato wa kufikia mafanikio sio rahisi hata kidogo. Kuna vitu vingi sana vinatega muda wako na hivyo usipokuwa makini utajikuta unakosa muda w akufanya yale mambo ambayo ni muhimu kwako. Pia ni rahisi sana kuahirisha mambo mpaka dakika ya mwisho na kujikuta unashindwa kukamilisha mambo yako.

Kwenye kitabu EAT THAT FROG mwandishi Brian Tracy anatupa mbinu za kuweza kumla chura(kufanya jukumu kubwa lililo mbele yako) kila siku na kuwa ni jambo la kuanza nalo siku yako. Brian anasema kama kila siku ungetakiwa kumla chura, basi kusubiri subiri hakutakusaidia chochote. Ni bora umkamate chura na kumla ili uweze kuendelea na mambo mengine. Hivyo ndivyo ilivyo kwenye majukumu yako ya kawaida. Kila siku una jukumu kubwa unalotakiwa kufanya kwenye kazi yako au biashara yako. Kuahirisha jukumu hili kunakuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa, hivyo kitu cha kwanza cha kufanya kwenye siku yako ni kumalizana na majukumu makubwa.

Ufunguo wa furaha, kujitosheleza na mafanikio makubwa ni wewe kuweza kujitengenezea tabia ya kumaliza majukumu makubwa kitu cha kwanza kwenye kila siku yako. Kwa bahati nzuri hii ni tabia ambayo kila mtu anaweza kujifunza, kupitia kurudia rudia. Na unapojijengea tabia hii ya kuanza siku kwa kufanya yale ambayo ni muhimu, mafanikio yako ni ya uhakika.

Yafuatayo ni mambo 21 unayoweza kufanya ili kuweza kukamilisha majukumu yako ya kila siku na kuacha tabia ya kuahirisha mambo.

1. Jua hasa ni kitu gani unachotaka.

Kuwa wazi kwa kile unachotaka ni hitaji muhimu ili kuweza kufikia mafanikio. Andika malengo yako na mipango kabla hata hujaanza kutekeleza majukumu yako. Kwa njia hii utajua ni kitu gani hasa unahitaji kufanya kwanza na kipi cha kusubiri.

2. Ipange siku kabla hujaianza.

Kabla hujaianza siku, iwe ni usiku kabla au asubuhi na mapema, panga jinsi ambavyo utautumia muda wa siku yako. Jua ni vitu gani utafanya na utavifanya saa ngapi. Dakika moja unayotumia kwenye kupanga, unaokoa dakika tano za kufanya kitu hiko.

3. Tumia sheria ya 80/20 kwenye kila kitu.

Sheria hii inasema kwamba asilimia 20 ya vitu unavyofanya ndio inazalisha asilimia 80 ya mafanikio yako. Kwa kifupi ni kwamba mafanikio yako yanatokana na mambo machache kati ya mengi unayofanya. Jukumu lako ni kujua ni mambo gani yanakuletea mafanikio makubwa na kuyafanya hayo tu na mengine kuachana nayo maana yanakupotezea muda.

4. Jua madhara yatakayotokea.

Kwa kufanya kitu au kutokufanya kitu kuna madhara yatakayotokea. Jua ni madhara gani yatatokea kwa wewe kufanya kitu fulani au kutokufanya kitu fulani. Kwa kujua madhara haya kutakusukuma wewe kuchukua hatua ili uweze kufikia mafanikio.

5. Jitengenezee tabia ya kuahirisha mambo, kwa upande mzuri.

Kwa sababu huwezi kufanya kila kitu kinachokuja mbele yako, jijengee tabia ya kuahirisha mambo ambayo sio muhimu kwako. Hii itakuwezesha wewe kupata muda wa kutosha wa kufanya yale mambo ambayo ni muhimu sana kwako.

6. Tumia njia ya ABCDE kila mara.

Kabla hujaanza kufanya jukumu lolote, ni vizuri ukayapanga majukumu yako katika makundi mbalimbali ambayo yataonesha umuhimu wa kila jukumu. Katika kupanga majukumu haya unatumia njia ya ABCDE;

A ni majukumu ambayo ni muhimu sana wewe kufanya ili ufikie mafanikio. Mfano kazi au biashara unayofanya na vile vitu ambavyo ndio sehemu kuu ya kazi au biashara yako.

B ni majukumu ambayo yanaonekana ni muhimu kufanya ila hayana haraka yoyote kwa wakati huo. Ila majukumu haya yakiachwa muda mrefu bila kufanywa huja kuwa muhimu na haraka sana kufanya. Mfano ni mipango mbalimbali ya ukuaji wa kazi au biashara yako.

C ni majukumu ambayo yanaonekana ni mazuri kufanya ila hayana mchango wowote kwenye mafanikio yako. Mambo kama kuangalia tv, kupiga soga wakati wa kazi na mengine kama hayo.

D ni majukumu ambayo kuna mtu mwingine anaweza kuyafanya vizuri kuliko unavyoyafanya wewe na kwa gharama ndogo. Majukumu haya tafuta mtu anayeweza kuyafanya na mpe ayafanye.

E ni majukumu ambayo hayana mchango wowote kwenye maisha yako na mafanikio yako na unatakiwa uache kuyafanya mara moja. Mambo kama kufuatilia maisha ya watu, kufanya majungu ni vitu vya kuepuka kabisa.

7. Weka mkazo kwenye maeneo muhimu.

Katika kazi au biashara unayofanya, kuna maeneo ambayo ni muhimu sana na ndio yenye uzalishaji mkubwa. Kwa kujua maeneo haya na kuyafanyia kazi kunaleta mabadiliko makubwa sana kwenye kazi au biashara yako. Yajue maeneo haya na yawekee mkazo mkubwa ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

8. Tumia sheria ya TATU.

Jua mambo matatu ambayo unaweza kufanya kwenye kazi yako na yakaleta asilimia 90 ya mafanikio yako kwenye kazi hiyo. Na weka mkazo kwenye kufanya mambo haya matatu kila siku kabla ya kufanya jambo jingine lolote. Kwakufanya hivi utajikuta una muda mwingi sana wa kufanya mambo mengine muhimu kwako kama kuwa na familia yako.

9. Jiandae vizuri kabla hujaanza.

Kuwa na vitu vyote muhimu kabla hata hujaanza. Hakikisha una vile vitu utakavyohitaji katika jukumu unalokwenda kufanya ili uweze kulitekeleza kwa wakati. Lakini hii isiwe chanzo cha kuahirisha mambo kwa sababu tu hujawa tayari. Sio lazima uwe na vitu vyote kwa asilimia 100, ukishakuwa na vile muhimu unaweza kuanza.

10. Nenda hatua kwa hatua.

Safari ya maili elfu moja inaanza na hatua moja. Unaweza kumaliza safari yoyote ndefu kama unapiga hatua moja baada ya nyingine. Ukitaka kumla tembo humli mzima mzima, bali unakata vipande vidogo vidogo na kula. Kwa jukumu lolote ambalo linaonekana ni kubwa sana kwako, ligawe kwneye majukumu madogo madogo na yafanyie kazi majukumu hayo. Ukija kustuka unashangaa jukumu ulilokuwa unahofia kwa sababu ni kubwa limemalizika.

11. Ongeza maarifa yako.

Jinsi unavyokuwa na maarifa zaidi kwenye kile unachofanya ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kutekeleza majukumu yako kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu. Jifunze kila mara ili kuongeza maarifa na kujua mbinu bora za kufanya kile unachofanya.

12. Tumia vizuri vipaji vyako.

Wewe una vipaji vyako, vijue vipaji hivi na jinsi unavyoweza kuvitumia kwenye kazi au biashara yako. Kwa kujua maeneo ambayo upo vizuri na kuweka moyo wako wote kwenye maeneo hayo itakusaidia kuweza kufanya kwa ubora na kufikia mafanikio makubwa.

13. Jua vikwazo vyako.

Una vikwazo ambavyo vinakuzuia kufanya zaidi au kuwa bora zaidi. Vijue vikwazo hivi kwa sababu ndio vinakuzuia wewe usifikie mafanikio makubwa. Vikwazo hivi vinaweza kuwa ndani yako mwenyewe, kwenye kazi yako au biashara yako, au vinaweza kuwa vinatoka nje yako. Weka nguvu zako kwenye kuondoa vikwazo hivi ili uweze kufikia lengo lako.

14. Jiwekee hali ya tahadhari.

Fikiria kwamba unahitajika kusafiri kwa wiki moja au mwezi mmoja na unapokuwa safarini huwezi kufanya kazi, hivyo unahitaji kumaliza kazi zako zote haraka. Hali hii itakusukuma wewe kufanya yale majukumu ambayo ni muhimu kwako na kuepuka yale yanayokupotezea muda.

15. Tumia muda na nguvu zako vizuri.

Kila mtu ana muda ambao anakuwa kwenye uzalishaji mzuri sana. Muda huu mtu anaweza kutekeleza majukumu yake kwa uwezo mkubwa na kwa wakati. Kuna wengine muda wao ni asubuhi, wengine mchana na wengine jioni. Jua muda wako wewe ni upi na katika muda huu usifanye jambo la kupoteza muda. Bali fanya mambo yatakayokuletea mafanikio makubwa kwa sababu utayafanya vizuri.

16. Jihamasishe kuchukua hatua.

Mhamasishaji mzuri kwako wewe kuchukua hatua ni wewe mwenyewe. Angalia jambo zuri kwenye kila kitu kinachotokea. Angalia jinsi ya kutatua jambo badala ya kuangalia matatizo ya kila jambo. Mara zote kuwa mtu mwenye mtazamo wa kuweza ka kufanya kwa ubora kuliko mtazamo wa kushindwa. Hii itakuhamasisha kuchukua hatua bora na zitakazokufikisha kwenye mafanikio.

17. Tumia teknolojia vizuri.

Teknolojia ililetwa ili kurahisisha kazi na kuwawezesha watu kufikia mafanikio makubwa bila ya kutumia nguvu sana na kwa muda mfupi. Lakini teknolojia hizi zimegeuka kuwa chanzo cha kukosa mafanikio na kupoteza muda. Mtandao wa intanet na mitandao ya kijamii imekuwa sehemu kubwa ya watu kupoteza muda. Simu zimewafanya watu kuwa watumwa wa mitandao na mawasiliano badala ya kufanya kazi bora. Hakikisha wewe unafanya teknolojia ikufanyie kazi na sio ikufanye wewe kuwa mtumwa. Wakati wa kazi kaa mbali na mawasiliano yoyote, yatakuletea usumbufu na kukufanya ushindwe kufikia mafanikio makubwa.

18. Gawa majukumu yako kwenye majukumu madogo madogo.

Kazi yoyote unayoifanya, igawe kwenye majukumu madogo madogo ambayo hayatakuchosha au kukupa uvivu wa kuyafanyia kazi. Kisha yafanyie kazi majukumu haya madogo.

19. Tenga muda wa kufanya kazi zako.

Katika kila siku yako ya kazi, tenga muda ambao utakuwa unafanya kazi tu. Katika muda huu hakuna mtu atakayeweza kukuingilia au kukusumbua. Muda huu unakuwa huna mawasiliano na akili yako yote inakuwa kwenye kazi yako. Kwa muda mfupi kama huu unaweza kuwa na uzalishaji mkubwa kuliko wa siku nzima.

20. Tengeneza hali ya haraka.

Jambo ambalo linahitajika kwa haraka ndio ambalo huwa linafanyika haraka pia. Kwenye yale majukumu yako muhimu, weka hali ya haraka. Kila jambo unalofanya, lifanye kwa haraka na usahihi. Julikana kama mtu ambaye anafanya mambo yake kwa haraka na umakini mkubwa.

21. Fanya jambo moja kwa wakati.

Mtu anayekimbiza sungura wawili, hawezi kukamata hata mmoja. Ni muhimu sana kupanga majukumu yako kulingana na umuhimu wake na kuanza kufanya lile ambalo ni muhimu zaidi. Fanya jukumu hili moja tu mpaka liishe ndio uende kwenye jukumu jingine. Hii ndio siri kubwa ya kuweza kuwa na uzalishaji mkubwa na kufikia mafanikio.

Jenga tabia ya kufanyia kazi mambo haya kila siku kwenye kazi au biashara unayofanya mpaka pale yatakapokuwa ni sehemu ya maisha yako. Kwa kuweza kufanya haya, hakuna kitu chochote, narudia tena, hakuna kitu chochote kinachoweza kukuzuia kufikia mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri kwenye kumla chura wako kila siku.

TUTAKUTANA KILELENI.