Enzi zangu mimi bwana, hela ndogo ndogo kama hizi zilikuwa
hazinipigi chenga…..

Enzi hizo nilikuwa msanii maarufu sana sema basi tu sasa hivi
mambo yangu hayako vizuri…

Enzi zangu biashara niliyokuwa nafanya ilikuwa na mafanikio
makubwa sana. Sema sasa hivi tu mambo hayajakaa vizuri…..

Enzi hizo kazini mimi ndio nilikuwa kila kitu, ila hawa vijana
wa siku hizi wamekosa heshima na kunichukulia mtu wa kawaida tu…..

Kama umeshaanza kutumia moja kati ya kauli hizo hapo juu nikupe
pole kwa sababu umeshaondoka kabisa kwenye njia itakayokupelekea kwenye
mafanikio. Ila nikupe moyo kwamba kama utasoma hapa na kama umekuwa unasoma
makala nyingine kupitia mtandao huu basi una nafasi ya kubadili maisha
yako.

Kauli hizo hapo juu ni dalili ya kukata tamaa, dalili ya
kushindwa na dalili kwamba hakuna kitu kikubwa kinachoweza kutokea mbele yako.
Kauli hizi zinatokana na mtu kufikia mafanikio fulani na kujisahau, kwa kujiona
yeye ndio yeye n hivyo anaacha kujifunza na kuendelea kuweka juhudi. Baada ya
muda mtu huyu anaachwa nyuma na kujiona kwamba hawezi tena.

SOMA; Kauli Mbili Za Kuacha Kutumia Leo, Maana Zinaashiria
Kushindwa.


Kama wewe ni mmoja wa watu hawa, napenda kukuambia kwamba anza
leo kufanya tena kile ambacho ulikuwa unafanya. Acha mara moja kutumia kauli za
enzi hizo na fanyia kazi kile ambacho unataka kuwa vizuri. Haijalishi una miaka
20 au 50 au 80 kama unajua kitu ambacho ulikuwa bora ila kwa sababu fulani
ukajisahau, anza kukifanya tena. Anza kujifunza kuhusu kitu hiki, anza kuweka
tena juhudi, weka ubunifu na usikate tamaa.

Kwa kufanya hivi utaanza kuona mabadiliko, utaanza kuona watu
wakiheshimu tena vile viwango vyako na utarudi kwenye ngazi zako za
mafanikio.

Acha kutumia kauli zinazoonesha kwamba jana yako ilikuwa bora
kuliko leo, pambana kila siku inayokuja uwe bora zaidi kwenye kile unachofanya.
Kama ilivyo kwa miti kwamba inaendelea kukua mpaka pale inapokufa, na wewe kuwa
hivyo hivyo, endelea kukua kwenye biashara yako, endelea kukua kwenye kazi yako
na endelea kukua kwenye kipaji chako bila ya kujali ni umri gani unao.

Siku utakayojiona kwamba wewe ndio unajua kila kitu, wewe ndio
unaweza kila siku, hii ndio siku ambayo unajilaani mwenyewe na unaanza kurudi
nyuma na kushindwa kufikia mafanikio makubwa zaidi.

TAMKO LA LEO;

Kauli za enzi hizo ni kauli sumu kabisa kwangu kufikia
mafanikio. Kuanzia sasa nitahakikisha kila siku nakuwa bora kuliko siku
iliyopita. Sitaki nijisahau halafu nije kuona kwamba siku zilizopita nilikuwa
vizuri. Nitajifunza kila siku, nitaweka juhudi kila siku na kila siku ya maisha
yangu nitazidi kuwa bora kwenye kile ninachofanya. Najua hii ndio njia ya
uhakika ya kufikia mafanikio.

Tukutane kwenye ukurasa wa 169 kesho, Like page yangu ya
Coach
Makirita Amani
uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha
kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365
bonyeza hapa na uweke email.

Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo
maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya
facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya
email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na
KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata
utaratibu.

TUPO PAMOJA.