Ili tuweze kufanikiwa katika maisha yetu kiukweli tunahitaji mambo mengi    ya kubadili mpaka kufikia mafanikio hayo. Kwa kubadili mambo hayo ambayo yanaweza kuwa mazoea, hulka ama tabia zetu tulizozipenda na kuzizoea zaidi ndiyo tunaweza kujikuta tukigusa mafanikio hayo tunayotaka yawe katika maisha yetu.
Pamoja na umuhimu wa kufanya mabadiliko hayo ambayo huwa ni wazi lazima yalete matunda ya mafanikio, lakini kwa wengi wetu huwa bado tena ni tatizo. Hili hasa huwa linatokea kutokana wengi wetu kuzidi kung’ang’ania sana tabia au matendo yanayoturudisha nyuma mara kwa mara katika maisha yetu.
Wapo ambao huzidi kung’ang’ania mazoea na wengine hushikila tabia mbaya zinazowakwamisha. Katika hili la tabia hil ndilo tunalotaka kuliongelea katika makala hii hasa kuhusu tabia hii ya kuwa na visingizio. Ni tabia ambayo wengi wamekuwa nayo na imekuwa ikuwakwamisha sana siku hadi siku katika maisha yao.
Hebu wewe mwenyewe binafsi jaribu kujiuliza ni mara ngapi umekuwa ukiwaza ama kusema huwezi kufanya jambo fulani kwa sababu hii  na ile, bila shaka ni mara nyingi. Wakati mwingine umekuwa ukijisemea “Aaaah sina muda, mimi ni maskini kwa sababu nimezaliwa katika familia maskini, au sina pesa kwa sababu sijaanda shule”. Hii ndiyo tabia ambayo umekuwa nayo kwa muda mrefu sasa.
Kwa kuwa na tabia hii ya visingio bila kujua ni tabia ambayo imekuwa ikukufanya ushindwe kufanikiwa kabisa, kwa nini? Ni kwa sababu inakuwa  kama inakujengea ukuta wa kufikia mafanikio ya kweli. Kitu ambacho usichokijua pengine, dunia haijali visingizio vyako. Kinachotakiwa kwako ni mafanikio tena makubwa kuliko unavyofikiri.
Sasa jiulize tena kwa kuwa na visingizio utaweza kufikia ndoto zako? Kama utauona ukweli kuwa hauwezi kufikia ndoto zako, umefika muda wa kuachana na visingizio katika maisha yako na kufuata malengo na mipango yako ya kweli. Je, ni kwa namna gani au mbinu zipi hasa ambazo wewe utaweza kuzitumia ili kuacha tabia ya kuwa na visingizio?
Hizi Ndizo Mbinu Nne Za Kukusaidia Kuweza Kuacha Tabia Ya Kuwa Na Visingizio Katika Maisha Yako.
1. Kuwa na mitazamo chanya.
Mara nyingi visingizio huweza kujitokeza katika maisha yako kutokana na wewe kuwa na mitazamo mingi hasi zaidi. Kwa kuwa na mitazamo hii hasi huwa unajiona hufai na huwezi kufanya karibu kila kitu. Kwa hiyo kila linapokuja jambo ambalo hata lipo chini ya uwezo wako kulifanya, mara nyingi kitu cha kwanza unakimbilia kuona ugumu wa kutoliweza na kutoa visingizio.
Ili kuweza kuondokana na hali hiyo ya kuwa na visingizio, unalazimika kuwa na mitazamo chanya zaidi. Unapojenga mtazamo chanya mambo mengi utayaona katika jicho la kuweza, badala ya kushindwa kama ilivyo sasa kwako. Hii ni mbinu mojawapo muhimu ya kuua visingizio katika maisha yako endapo utaitumia.

2. Chukua jukumu la kuwajibika zaidi.
Unaweza ukaliondoa tatizo la kuwa na visingizio pia kwa kuwajibika zaidi katika maisha yako. Tuchukulie mathalani unalalamika na kusingizia sana kuwa huanzishi biashara kwa sababu huna mtaji, hiyo ni sawa kwako. Lakini ili uweze kuondokana na hili unatakiwa kufanya kazi zaidi kuliko wengine ili kupata huo mtaji.
Kuwa kwako na visingizio tena visingizio bila kuchukua jukumu la kuwajibika zaidi juu ya maisha yako, hiyo itakuwa ni sawa na kazi bure na hutaweza kutoka hapo. Wengi huwa wanajikuta wanaharibu maisha yao kutokana na kuwa na visingizio visivyoisha, wewe ni shahidi juu ya hili, bila shaka umewahi kuwaona watu wa namna hii. Ukishaona una visingizio sana elewa kabisa unatakiwa kuwajibika zaidi.
3. Tafuta majibu ya lile linalokusumbua.
Kwa bahati nzuri sana kila tatizo lilopo hapa duniani lina majibu yake. Unaweza ukawa unakisingizio cha kuwa una tatizo la muda hiyo sawa sikatai, lakini unaweza ukatengeneza muda wa ziada kwa siku hata dakika kumi mpaka kumi na tano zinakutosha. Amka asubuhi na mapema kuliko kawaida yako utajikuta huo muda unaouhitaji tayari  unao angalau.
Unaweza ukasema ooh wewe ni maskini kwa sababu eti umezaliwa familia maskini nalo hilo ni sawa kwako pia.  Lakini jiulize pia ni wangapi walikuwa na hali ngumu kama ya kwako walitoka kwenye umaskini huo na kuwa ni watu wenye mafanikio? Hicho ndicho kitu unachotakiwa kukifanya hata wewe ili uweze kuondokana na visingizio. Tafuta suluhu siku zote.
4. Angalia malengo yako sana.
Kama wewe ni mtu wa kujiwekea malengo suala la kuwa na visingizio ni lazima uliweke pembeni. Ukishajiwekea malengo kwa vyovyote vile ni lazima  uyatimize kwa sababu unajua unakotaka kufika. Hakuna kitu wala kitu chochote kitakachoweza kukuzuia njiani juu ya hilo. Hii ni njia mojawapo muhimu ya wewe kuweza kuondoa visingizio katika maisha yako.
Ukiangalia na kuwafatilia wengi wenye visingizio sana katika maisha yao ni watu ambao maisha yao hawajajitoa sana kwenye malengo yao. Hapa ndipo tatizo kubwa la visingizio linapoanzia. Kitendo cha kukosa malengo basi kila kitu ugumu huanzia hapo. Ili kuondokana na hali  kama hii ni lazima kujua namna ya kujiwekea malengo na kuyafuata hapo tutakuwa tuna tibu tatizo la kuwa na visingizio kisawa sawa.
Ni ukweli wengi kwa namna moja au nyingine huwa ni watu wa kuwa na visingizio lakini hiyo isiwe sababu kubwa sana ama kizuizi cha kufikia mafanikio yetu. Tunaweza kabisa kuondokana na visingizio hivyo kwa kutumia  mbinu muhimu kama tulivyoziona katika makala hii.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi, tunakutakia kila la kheri.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,