Mitandao ya kijamii ni sehemu nzuri sana ya kutangaza biashara yako. Hii ni sehemu ambayo wateja wako wanakuwepo kwa muda mrefu na wanafuatilia mambo mbalimbali.

Lakini changamoto moja inakuja kamba wengi wa watu wanaotangaza kwenye mitandao hii, kiuhalisia hawatangazi, bali wanapiga kelele. Na kwa jamii ya sasa, watu hawataki kelele, na wanazikimbia haraka sana. Kwa kuwa lengo la kipengele hiki cha BIASHARA LEO ni kukupa mbinu za kukuza biashara yako, leo tutajadili hili la kutangaza kwenye mitandao ya kijamii na utajia njia nzuri ya kufanya hivyo.

Nimekuwa natumia mitandao ya kijamii kwa muda sasa. Na kwa hapa Tanzania, mitandao ambayo ina watumiaji wengi ni Facebook na Twitter. Na kwenye mitandao hii kuna watu ambao ni maarufu na wana watu wengi wanawafuatilia. Watu hawa wanapoweka chochote, watu wanapenda(like) na kuchangia pia. Sasa watu wengi wasiojua mbinu nzuri za kutangaza biashara hutumia nafasi hii kuweka matangazo yao. Wanasubiri hawa watu maarufu waweke kitu na katikati ya maoni wao wanachomeka tangazo lao.

SOMA; Teknolojia Katika Kilimo: Kilimo Cha Greenhouse Na Aina Zake.

Watu wanafikiri kwa njia hii wanawafikia wale watu wengi wanaochangia kwenye mada za watu hao maarufu, ila ukweli ni kwamba wanapiga kelele ambazo haziwafikii watu wengi.

Sikiliza kwa makini sana, kama unatangaza kwenye mitandao ya kijamii elewa kwamba zile enzi za kupiga kelele zimepitwa na wakati. Sasa hivi watu hawaji kununua kwako kwa sababu tu wameona tangazo lako ila kwa sababu wanakuamini na kukuamini huku kunatokana na urafiki ambao utakuwa umeijenga kupitia mitandao hii.

Hivyo jukumu lako la kwanza ni kujenga urafiki, andika vizuri kuhusu biashara yako(lakini sio matangazo) kwenye ukurasa wako wa mtandao wa kijamii. Kuna watu wataendana na vile vitu unavyoandika. Jichanganye nao, jibu maswali yao na wakishakuamini, waambie kuna huduma bora zaidi wanaweza kulipia na kupata, watakuwa tayari kufanya hivyo mara mia kuliko unapowapigia kelele wakati hata hawakujui.

Tumia mitandao ya kijamii kutengeneza mahusiano ya kirafiki kati yako na watu ambao wanaweza kuwa wateja wako. Na wala huhitaji kuwa na watu wengi kama watu hao maarufu, kazana kutengeneza marafiki 1000 tu ambao wanakuamini na wanafuatilia kile unachofanya. Moja ya kumi wanaweza kuwa wateja wako wazuri.

Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.

Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.

Jiunge na COACHING/MENTORSHIP PROGRAM ambapo utapata muongozo wa hatua kwa hatua mpaka ufikie mafanikio kwenye kazi au biashara unayofanya. Bonyeza haya maandishi kupata maelekezo ya programu hii.