Kuna tatizo kubwa la ajira, watu wengi wamesoma ila nafasi za kazi ni chache, hivyo wengi wanabaki mtaani wasijue wafanye nini. Vile vile kuna tatizo la uhaba wa wafanyakazi bora kwenye maeneo ya kazi. Sehemu kubwa ya wafanyakazi wapo kwenye kazi zao kwa vile tu ndio zinawapatia kipato. Ila ukipima thamani hasa wanayoitoa kwenye kazi hizo unakuta hakuna na mbaya zaidi kuna wengi ambao ni sumu kwenye kazi zao. Yaani sio tu kwamba haleti thamani ila pia anaharibu eneo la kazi na hivyo kuwa mzigo mbaya.
Leo katika makala hii tutajadili tabia tano za wafanyakazi ambao ni sumu kwenye eneo la kazi. Makala hii ni mahususi kwa makundi mawili ya watu. Kundi la kwanza ni waajiri ambao wamekuwa wakisumbuliwa na wafanyakazi. Hii itawawezesha kujua wafanyakazi ambao ni mzigo kwao na hivyo kuweza kuchukua hatua muhimu za kuokoa eneo lao la kazi.
Pia makala hii ni mahususi kwa wafanyakazi ambao wanataka kufikia mafanikio makubwa kupitia kazi zao. Hapa watajifunza tabia tano za kuepuka ili kuhakikisha wanaendelea kutoa thamani kwenye eneo lao la kazi na wanaepuka kuwa sumu kwenye eneo hilo la kazi.
Hivyo kama wewe ni mjasiriamali uliyeajiri watu wa kukusaidia kwenye biashara yako, makala hii inakuhusu sana na pia kama ni mfanyakazi makala hii ni yako pia.
Zifuatazo ni tabia tano za wafanyakazi ambao ni sumu kwenye eneo lao la kazi. Zijue na ujue hatua za kuchukua ili mambo yako yaweze kwenda vizuri.
1.     Wapikaji na wasambazaji wa majungu.
Majungu ni sumu kubwa sana kwenye eneo la kazi. Watu wakishaanza kusemana vibaya, wanaharibu uhusiano wao wa karibu, wanaacha kuaminiana na inakuwa vigumu kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja. Unapoona mfanyakazi ambaye anajihusisha sana na majungu jua huyu ana sumu kali na sumu hii itaharibu wafanyakazi wengine wote. 
Dawa ya wafanyakazi hawa kama wewe ni mwajiri ni kuachana nao, kuwafukuza maana sumu yao ni kali na huwa hawarekebishiki. Ukishaona mfanyakazi anaiongelea kazi hiyo vibaya kwa wengine au anawasema wafanyakazi wengine vibaya jua huyu ni sumu na ondokana naye haraka sana. Dunia tuliyopo sasa inahitaji kuaminiana kwa hali ya juu na kuweza kufanya kazi kama timu.
Kama wewe ndio mfanyakazi mwenyewe ambaye unajihusisha na majungu acha mara moja. Kama hujijui angalia tabia zako, je unapenda kuwasema watu vibaya. Je huwa unazungumza maneno ya chini chini kuhusu kazi yako au wafanyakazi wenzako. Acha, japokuwa unaweza usifuate hili, kuna siku watakuchoka na watakufukuza. Au watakunyima fursa nzuri za mafanikio kwako.
2.     Wanalalamika kuhusu kila kitu.
Tabia nyingine ambayo ni sumu mbaya kwenye eneo la kazi ni kulalamika kwa kila kitu na kila jambo. Kuna wafanyakazi ambao hawakosi kitu cha kulalamikia au kukosoa. Chochote kinachofanyika wao wanalalamika. Wakipangiwa majukumu wanalalamika na kuona kama wao wanaonewa na kuna watu ambao wanapendelewa. Hii ni sumu kali sana, maana kulalamika ni sumu ambayo inasambaa kwa kasi na wafanyakazi wengi wanapoipata, eneo la kazi linakuwa hovyo sana.
Kwa mwajiri, fukuza mfanyakazi yeyote ambaye anapenda kulalamika kwa kila jambo. Unavyozidi kumuacha anazidi kusambaza sumu yake mbaya kwa wafanyakazi wengine na muda sio mrefu eneo la kazi litakuwa kijiwe cha walalamikaji, kama bado halijafikia hali hii.
Kwa mfanyakazi, acha kulalamika. Kazi ulienda kuomba mwenyewe, achana na hadithi kwamba wewe unaonewa, au kuna wengine wanapendelewa. Kama kuna mtu anakuonea angeshakufukuza kazi. Acha kupika kelele na fanya kazi. Ongeza thamani kwenye kazi unayotoa na ukiona huthaminiki, achana na kazi hiyo na ukafanye mambo mengine ambapo utathaminika.
3.     Wanahitaji usimamizi wa moja kwa moja.
Kuna wafanyakazi ambao wanajua majukumu yao na wanayatekeleza kwa wakati na kwa ufanisi wa hali ya juu sana. Hawa ni wafanyakazi ambao wanaongeza thamani kubwa kwenye kazi wanazofanya. Wafanyakazi sumu wao wanahitaji usimamizi wa moja kwa moja ndio waweze kutekeleza majukumu yao. Wakiachiwa wafanye shughuli zao wenyewe hawawezi kabisa kuzikamilisha. Ni mpaka wasimamiwe na wakati mwingine kutishiwa kama watoto.
Kwa mwajiri, hasa kama ni mjasiriamali unayepigana kutoka, huna muda wa kuanza kumsimamia kila mfanyakazi kwa kila anachofanya. Hivyo wafanyakazi wa aina hii ni mzigo kwako na unaweza kufikiria kuondokana nao ili uweze kupata wafanyakazi bora na watakaokupa wewe nafasi ya kufikiria mambo makubwa zaidi. Na sio kutumia muda wako kuhakikisha mfanyakazi wako hashindi kwenye mtandao siku nzima ya kazi.
Kwa mwajiriwa, jifunze kujiongoza mwenyewe. Panga ratiba zako na zifuate, jua majukumu yako na yatekeleze kwa wakati na kwa ufanisi mzuri. Kama hili linakushinda unajiweka kwenye hatari kubwa sana.
4.     Hawakubali majukumu yao.
Hakuna mtu ambaye hakosei, na usije ukamfukuza mfanyakazi wako kwa sababu amekosea, kila mmoja wetu anakosea. Lakini mfanyakazi anapokosea na akakataa kuhusu alichokosea, huyu ni sumu kubwa. Kama mfanyakazi ameshapewa majukumu yake, ila anafanya janja janja ya kukwepa majukumu hayo, huyo ni sumu. Kama mfanyakazi ameshapangiwa majukumu yake ila kila mara anatafuta njia za kuonesha kwamba kitu fulani ambacho hakikufanyika au kimefanyika vibaya sio jukumu lake huyu ni sumu.
Mwajiri, mweleweshe vizuri mfanyakazi kuhusu majukumu yake na kama tabia hii inaendelea fanya utaratibu wa kuachana naye.
Mwajiriwa, hakikisha unayajua majukumu yako vizuri na unayatekeleza kwa ubora wa hali ya juu. Pia unapokosea kubali kwamba umekosea na hakuna mtu atakayekuua au kukufunga kwa sababu umekosea.
5.     Wanaangalia fedha tu.
Ukishaona mfanyakazi anachoangalia ni fedha tu, umebeba sumu ambayo itakumaliza wewe mwenyewe. Kama mfanyakazi anazungumzia fedha kila wakati, kama kila siku anataka kuongezewa kipato ili hali hatoi kazi ambayo ni bora, ni sumu. Na mara nyingi wafanyakazi wanaoangalia sana fedha huwa hawafanyi kazi ambayo ni bora.
Kwa mwajiri, kama mfanyakazi anaongelea tu fedha kila wakati, kama ukimwomba afanye jukumu dogo la ziada anataka na fedha za ziada, basi huyu hakufai. Ni sumu kubwa ambayo itaharibu sana eneo la kazi na mwishowe itakuwa ni eneo la udalali na vibarua. Achana na mfanyakazi wa aina hii.
Kwa mwajiriwa, kabla hujataka fedha za ziada weka kwanza kitu cha ziada. Kama unafanya kazi kwa kiwango kile kile ambacho ulikuwa unafanya mwaka jana, sasa unataka upewe ongezeko la fedha kwa sababu gani? Kama unafikiri maisha magumu ndio yanaamua uongezewe kipato, subiri utakapofukuzwa kazi ndio utajua nini maana ya kutoa thamani. Toa thamani kubwa na kama watu hawaijali, angalia ni wapi inaweza kujaliwa.
Eneo la kazi linapaswa kuwa sehemu ambayo watu wanafurahia kuwepo na wanashirikiana ili kutoa bidhaa au huduma inayowasaidia wale wateja wa kazi husika. Kama kuna mfanyakazi yeyote ambaye anakuwa kikwazo kwenye mchakato huu mzima huyu ni sumu na anapaswa kuchukuliwa hatua mara moja. Ushirikiano kati ya mwajiri, mwajiriwa na hata wafanyakazi kwa ujumla unahitaji kuwa mkubwa sana kama mnataka kufanikiwa kwenye dunia ya sasa yenye changamoto kubwa. Ila kama eneo la kazi lina watu ambao wanapika majungu, wanalalamika kwa kila jambo, wanataka hela tu na hawakubali majukumu yao, mafanikio ni vigumu sana kwenye eneo hilo.
Kila mmoja achukue hatua kwa pale anapohusika na mambo yatakuwa mazuri sana.
Nakutakia kila la kheri kwenye kazi yako na uweze kuitumia kufikia mafanikio makubwa.
TUPO PAMOJA.
Makirita Amani,