Kila mmoja wetu ana kitu kikubwa sana ambacho kipo ndani yake,
ambacho akikitoa anaweza kuleta mabadiliko makubwa sana kwa watu wengine. Lakini
tatizo kubwa ni kwamba wengi wetu hatutoi vitu hivi. Na tumekuwa tunaidhulumu
dunia kwa kiasi kikubwa sana.
Kazi ambayo nimekuwa naifanya, ya uandishi na kufundisha,
imekuwa inawasaidia watu wengi sana. Najua hili kwa sababu wengi wamekuwa
wakiniandikia jinsi ambavyo maisha yao yanabadilika. Wakati naanza kuandika,
nikiwa bado nakazana kutafuta njia gani ya uandishi ninaipendelea na nitapata
watu wa kunisikiliza na kufanyia kazi kile ninachoandika, kuna wakati niliona
hakuna kikubwa kwenye uandishi huu, nafanya kwa sababu napenda tu kuandika. Ila
kwa sasa, kama nikisema niache kuandika leo, nitakuwa nimefanya dhuluma kubwa
sana kwa dunia hii. Ni jukumu langu kuendelea kutoa maarifa ambayo yanawawezesha
watu kubadili maisha yao, na kuyafanya yawe bora zaidi ya yalivyokuwa hapo
awali.
Hata wewe pia una kitu kikubwa cha kutoa kwenye dunia hii.
Kupitia biashara au kazi unayofanya, usiangalie tu ni mshahara kiasi gani
unapata, usiangalie tu ni faida kiasi gani unapata, angalia ni thamani gani
unatoa kwa wengine. Angalia ni jinsi gani unayagusa maisha ya wengine. Fanya
hivi kwa moyo mmoja na kwa juhudi kubwa na ninakuhakikishia, ndio nakuhakikishia
kwamba dunia italazimika kukulipa, na itakulipa kwa kiwango kikubwa sana mpaka
mwenyewe utashangaa muda wote ulikuwa wapi hukulijua hili.
SOMA; Vitu
Ambavyo Ni Rahisi Kufanya…. Na Madhara Yake.
Wewe ni mwandishi? Andika mpaka mtu ashawishike kufanya kile
unachoamini ni sahihi kwake kufanya, na atakapofanya na akafanikiwa, atakulipa,
kwa kiwango kikubwa sana.
Wewe ni muimbaji? Imba mpaka watu wasimame, watu waache kufanya
wanachofanya wakusikilize, watu watafute wimbo wako wakati wanajisikia kukata
tamaa, na wautafute pia wakati ambapo wana furaha na watakulipa sana.
Wewe ni mwalimu? Fundisha mpaka watu waelewe, hakikisha hakuna
anayetoka akiwa mtupu na hata kama haelewi lile somo unalomfundisha basi
hakikisha unamfundisha chochote kitakachomsaidia kwenye maisha.
Wewe ni daktari? Toa huduma nzuri za afya zitakazookoa na
kuboresha maisha ya watu. Fanya kila unachoweza kuhakikisha kwamba mgonjwa
anayekuja kwako akiwa amekata tamaa kwamba maisha yake ndio yanafika tamati,
aondoke akiwa na maisha yenye matumaini, hata kama huwezi kumponesha, basi
umpunguzie hata maumivu. Na dunia italazimika kukulipa.
Hakuna kitu kizuri ambacho utakifanya na dunia ikaacha kukulipa,
nina uhakika na hili. Nakusihi sana, fanya leo. Hata kama ni mzazi, toa malezi
bora kwa mtoto wako na wanaokuzunguka pia, dunia itakulipa.
TAMKO LA LEO;
Najua nimekuwa naidhulumu dunia kwa kushindwa kutumia uwezo
mkubwa ambao upo ndani yangu. Kuanzia sasa nitafanya kile ninachofanya kwa moyo
mmoja na kwa ajili ya kufanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Najua dunia
itanilipa kwa hili na fedha haitakuwa tatizo kubwa kwangu. Kila siku
nitaikopesha dunia kwa kufanya mambo ambayo ni bora na najua dunia italazimika
kunilipa.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita
Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi
yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365
bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo
maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya
facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya
email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na
KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata
utaratibu.
TUPO PAMOJA.