Moja ya njia rahisi za kuingia kwenye biashara au kukuza biashara yako ni kuingia kwenye ubia na mtu mwingine. Watu wengi wametumia njia hii, ila ni wachache sana ambao wameweza kufanikiwa kuendesha biashara zao vizuri kwa njia hii ya ubia. Watu wengi wanaoingia kwenye ubia wamekuwa wakiishia kugombana na kushindwa kuendesha biashara. Kuna wengine wengi ambao wapo kwenye ubia wa kibiashara ambao kama wangejua mwanzo wasingeingia kwenye ubia huo, maana umefanya maisha yao kuwa magumu.

Leo tutajadili mambo muhimu ya kuzingatia kabla hujaingia kwenye ubia wa kibiashara ili uweze kuendesha biashara unayoingia vizuri na kupata mafanikio pia. Sio kila mtu anayekuambia mfanye biashara kwa pamoja anafaa kufanya naye biashara, hata kama wewe ndio mwenye wazo na yeye ndio mwenye fedha, hakikisha unajiridhisha kwanza kabla ya kuingia kwenye ubia huo. Yafuatayo ni mambo muhimu ya kujiridhisha kabla hujaingia kwenye ubia wa kibiashara.

1. Jiridhishe na uaminifu wa mtu unayeingia naye kwenye ubia.

Kama mtu unayetaka kuingia naye kwenye biashara sio mwaminifu, usiingie kwenye ubia huo. Unajipeleka kwenye matatizo makubwa sana ambayo utashindwa kuyatatua. Watu ambao sio waaminifu mara zote hufanya mambo ambayo yanatengeneza matatizo. Epuka matatizo haya kwa kujiridhisha na uaminifu wa mtu kabla hujakubali kufanya naye biashara. Kumbuka biashara za karne hii zinaendeshwa kwa uaminifu kati ya mwenye biashara na mteja, sasa kama mmoja wa wamiliki wa biashara sio mwaminifu hata wateja wataliona hilo kutokana na jinsi mtakavyoendesha biashara yenu.

Kama wewe ndio sio mwaminifu hakikisha unabadili hili haraka sana. Anza kujijengea tabia ya uaminifu na itakusaidia mambo mengi kwenye maisha, sio biashara tu.

2. Muwe mnaendana kwa tabia.

Ili ubia wenu kwenye biashara uende vizuri ni vyema mkawa na tabia zinazoendana. Kama tabia zenu zinatofautiana sana ni rahisi kwa ubia kuvunjika. Kama mmoja nui mtumiaji wa pombe na mwingine hataki kusikia kabisa habari hiyo ya pombe kuna wakati mtakwazana. Kama mna tabia ambazo zinakinzana ni bora msipoteze muda kwa kuanza biashara kwa sababu hamtafika mbali. Hata kama tabia zenu zinatofautiana, basi hakikisha hazikinzani ili iwe rahisi kuvumiliana, ila zinapokuwa zinakinzana kutatokea mgogoro kati yenu.

3. Muwe na ujuzi au uwezo tofauti.

Ubia mzuri na unaoweza kudumu ni ule ambao kila mbia ana uwezo au ujuzi wa tofauti na wenzake na ujuzi wenu kwa pamoja unategemeana. Kwa mfano mmoja ni mtaalamu wa masoko, mwingine ni mtaalamu wa mipango. Au mmoja ni mbunifu na mtu wa kuja na mawazo mazuri na mwingine ni mtekelezaji na mfuatiliaji mzuri wa kitu mnachokubaliana. Ila wote mnapokuwa na uwezo au ujuzi wa aina moja, mtaishia kufanya kitu kimoja na vingine vitakosa mtu wa kuvisimamia vizuri. Wakati mwingine mnaweza kujikuta mkishindana kwa vile wote mnafanya kitu kimoja, ni hali ya kawaida kwa binadamu.

4. Muwe na malengo yanayoendana.

Ni jambo la kusikitisha kama wewe utakuwa na malengo ya kutengeneza biashara ambayo itasambaa Afrika nzima na mwenzako anapanga biashara ikue kwenye mkoa ambao mnafanyia biashara. Kama malengo yenu yanatofautiana mtajikuta mnavutana na kurudishana nyuma. Ni vyema mkawa na malengo yanayoendana ili kwa pamoja myafanyie kazi na kuweza kuyafikia kupitia biashara mnayofanya. Na hii sio kwa malengo ya biashara tu, bali hata malengo binafsi.

5. Morali wa kufanya kazi na kujitoa.

Biashara sio lele mama, biashara sio majaribio. Biashara ni kazi ambayo inahitaji umakini mkubwa na uvumilivu wa hali ya juu. Kuna wakati utahitaji kuweka nguvu za ziada kwenye biashara yenu. Kuna wakati mtahitaji kuacha mambo mengine ambayo mnapenda kufanya ili kuweka muda zaidi kwenye biashara yenu. Sasa kama mmoja wa wabia hana morali wa kazi na kujitoa, atakuwa kikwazo kwa biashara yenu kukua. Ni muhimu sana kuhakikisha mtu unayekwenda kufanya naye biashara yupo tayari kujitoa zaidi.

Jambo muhimu sana ninalokusisitiza uzingatie wakati unachagua mtu wa kufanya naye biashara ni kuangalia kama vitu hivi vipo. Watu hujidanganya kwamba mtu atabadilika mbeleni mwa safari, ila ukweli ni kwamba hakuna mtu anayebadilika kirahisi, hasa pale anapobadilishwa na wengine. Hakikisha vitu hivi muhimu vipo kwa mtu unayetaka kuingia naye kwenye biashara kabla hata hamjaanza. Itawasaidia kuendesha biashara ya ubia yenye mafanikio.

TUPO PAMOJA.