Binadamu ni viumbe ambao tunazungukwa na viumbe wenzetu ambao ni binadamu pia. Hakuna njia ambayo unaweza kuitumia na ukaweza kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako bila ya kumhusisha binadamu mwingine. Tunategemeana sana ili kuweza kuwa na maisha bora na kufikia mafanikio makubwa.
Katika maeneo yetu ya kazi iwe umeajiriwa, umejiajiri au unafanya biashara kuna mambo muhimu unayohitaji kufanya ili kuongeza ushirikiano wako na wengine na kuweza kufikia mafanikio makubwa. Unahitaji kujua mambo haya na kuyazingatia kwani tabia zetu binadamu zinatofautiana sana. Usipokuwa makini unaweza kujikuta unakosana na kila mtu na maisha yako yakawa magumu sana.
Leo tutajadili mambo matano muhimu ya kuzingatia kwenye eneo lako la kazi ambayo yatakuwezesha kushirikiana na wengine vizuri na hatimaye kufikia mafanikio makubwa. Kwa kujua mambo haya na kuyafanya kutaongeza ushirikiano na watu watapenda kufanya kazi na wewe na hii itakuongezea nafasi za wewe kufanya vizuri na kufikia malengo yako.
1. Pokea maoni ya wengine.
Kitu muhimu na cha kwanza unachotakiwa kufanya ili kuongeza ushirikiano kwenye eneo lako la kazi ni kupokea maoni ya wengine. Chukua maoni mengi kutoka kwa watu mbalimbali. Watu hawa wanaweza kuwa wa karibu yako kikazi au hata wa mbali. Kazi yako wewe ni kupokea maoni mengi uwezavyo na kuyatafakari ni jinsi gani yanaweza kuboresha eneo lako la kazi.
Usiwe mtu wa kuona kile unachofanya ndio sahihi na hakuna mwingine wa kukupa maoni. Pokea maoni hata kama utaona ni ya kijinga na yafikirie vizuri unaweza kuona kitu kizuri sana kimejificha kwenye maoni hayo. Watu wana mawazo mazuri sana, yapate mawazo haya mara kwa mara na ona ni jinsi fani yanaweza kuboresha eneo lako la kazi au biashara yako.
2. Kuwa tayari kubadilika.
Eneo lako la kazi sio eneo la kuonesha msimamo au kuonesha kwamba mara zote wewe upo sahihi. Kwa kufanya hivi utawaangusha wengine na hawatafurahia kufanya kazi na wewe. Kuwa tayari kubadilika pale unapoona kuna haja ya kufanya hivyo. Kama utakuwa tayari kupokea maoni ya wengine na kuyafanyia kazi lazima utaona maeneo ambayo unahitaji kubadilisha. Sasa unapoyaona yafanyie kazi na usiache kubadilika kwa sababu tu unaona kwamba utaonekana hujui unachofanya.
Mabadiliko ndio kitu pekee ambacho kinatakiwa kukumbatiwa kwenye eneo la kazi. Usikubali hata kidogo kufanya kazi kwa mazoea. Maana kuna watu ambao huwa wanakaribisha maoni ila kila kitu wanachoambiwa hutafuta njia ya kukipinga na wakikosa watasema hatufanyagi hivyo. Kuwa tayari kubadilika, dunia yenyewe inabadilika kwa kasi kubwa sana, kama hutakuwa tayari kubadilika utaachwa nyuma na hali yako itakuwa mbaya zaidi.
3. Kubali kukosolewa.
Japokuwa mimi binafsi naamini kukosoa ni njia mbovu sana ya kumfundisha mtu, asilimia kubwa ya watu unaowafanyia kazi au wanaokufanyia kazi au unaofanya nao kazi watakukosoa. Haijalishi wamekukosoa kwa njia gani, unahitaji kukaa chini na kutafakari ni kitu gani umefanya ambacho kimewafanya wao wafikirie kwa tofauti. Unapokosolewa usikimbilie kubishana na kupinga kwamba wewe huhusiki, bali tafakari vizuri ni kwa njia gani kitu ulichofanya kimeleta matokeo ambayo hayakutegemewa.
Unapotafakari na kuona kweli umekosea, kiri kosa na ahidi kurekebisha chochote ambacho hakikuenda vizuri. Kama kuna tatizo limetokea na wewe hukuhisika bado sio nafasi ya wewe kupinga na kutafuta ushindi, bali kuwa mstari wa mbele kuhakikisha tatizo hilo linarekebishwa ili lisilete tatizo kwenye eneo lako la kazi. Kukubali kukosolewa kutawafanya watu wapende kufanya kazi na wewe sio kwa sababu watapata mtu wa kumlaumu, ila kwa sababu wanajua wanafanya kazi na mtu ambaye yuko tayari kuchukua majukumu yake.
4. Toa maoni yako ya kweli, epuka unafiki.
Unafiki sehemu ya kazi ni sumu kubwa sana maana haitaishia sehemu moja au kwa mtu mmoja tu, itasambaa kwenye kazi yote. Ili kuongeza ushirikiano kwenye eneo lako la kazi, toa maoni yako ya kweli na epuka unafiki. Kama kuna kitu mtu amefanya vizuri, msifie na mfanye aone kwamba amefanya kitu kizuri ana ambacho kinasaidia sana eneo lenu la kazi. Na kama kuna kitu mtu amekosea usikimbilie tu kumkosoa, bali mwelekeze ni jinsi gani ya kufanya kwa usahihi kwa wakati mwingine. Pia mfanye asiumie kwa kuona amewaangusha wengine ila mwoneshe kwamba alikuwa kwenye hatua za kujifunza na sasa ameshajua ni kitu gani akifanya anakosea na hivyo kuepuka kufanya kitu hiko.
Kwa mtazamo huu utaweza kushirikiana na wengine na wengi watapenda kufanya kazi na wewe.
5. Jua ni kitu gani watu wanataka kupitia kazi mnayofanya.
Mara nyingi sana wafanyakazi unaofanya nao kazi kuna vitu vya ziada ambavyo wanataka kupitia kazi hiyo ukiacha kipato wanachopata. Kwa kujua vitu hivi utakuwa umepata njia ya kuweza kuwahamasisha ili waweze kuwa na uzalishaji bora zaidi. Watu wanapenda kuonekana wa muhimu, wanataka waone mchango wao umeleta mabadiliko makubwa na wanapenda kusifiwa kwa vitu vizuri ambavyo wamefanya.
Weka hiki kuwa kipaumbele chako kwenye eneo lako la kazi. Wafanye watu waone kazi yao ni muhimu sana na mchango wao umekuwa na faida kubwa kwenye kazi mnayofanya. Pia wanapofanya vizuri wapongeze na wape motisha ambao utawafanya wakazane zaidi ili kuendelea kuwa bora zaidi.
Mafanikio yako kwenye eneo lako la kazi yanategemea sana ni jinsi gani unaweza kuendana na wafanyakazi wengine wenye eneo hilo la kazi. Fanyia kazi mambo haya matano na mengine utakayoendelea kujifunza na hakika utaona mabadiliko makubwa kwa wale unaofanya nao kazi na hata kwa kazi unayofanya. Kumbuka kila kitu kinaanza na mtazamo na unapokuwa na mtazamo sahihi kila kitu kinaanza kuonekana kwa usahihi.
Nakutakia kila la kheri kwenye kazi unayofanya, iwe ni ya kuajiriwa, umejiajiri binafsi au unafanya biashara. Una nafasi kubwa sana ya kuleta mabadiliko na kufikia mafanikio. Endelea kuweka juhudi na maarifa, hakuna kinachoshindikana.
TUPO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.