Kwa jinsi tulivyolelewa na kukuzwa, kushindwa ni kitu cha aibu
sana, ni kitu kinachostahili adhabu kubwa na kama utashindwa basi wewe ni mtu
ambaye hufai. Si ndio tulivyofundishwa shuleni? Na ndio maana tulipewa adhabu
kali pale ambapo tulishindwa kwenye kazi au mtihani.
Kinyume na ilivyo kwenye elimu na hata kwenye malezi uliyopewa,
kwenye maisha ya kawaida kushindwa ni kitu kizuri sana. Kushindwa ni muhimu kwa
sababu unajifunza mambo mengi kuliko unavyoshinda. Japo wengi hawaamini hili na
hawataki hata kusikia.
Kwa woga wetu wa kushindwa, wengi wetu wamekuwa wakiogopa hata
kuweka malengo makubwa kwa kuogopa kushindwa. Mtu anaona kama aliweka malengo
makubwa na akashindwa kuyafikia basi ni sawa na kujidhalilisha. Kwa sababu hiyo
anaweka malengo madogo ambayo yapo ndani ya uwezo wake na anayafikia
vizuri.
SOMA; Hii ndio faida ya kushindwa.
Sasa kuweka malengo ambayo yako ndani ya uwezo wako na
ukayafikia vizuri, unafikiri ni kitu gani kikubwa umejifuza? Hakuna, yaani
umeendelea kuwa vile ulivyokuwa na huwezi kufikia mafanikio makubwa.
Lakini unapoweka malengo makubwa, malengo ambayo hata wewe
mwenyewe yanakuogopesha, haya ndio malengo ambayo yatakusukuma ufanye zaidi na
hata kama hutayafikia, utamaliza ukiwa mbali kuliko ungeweka malengo
madogo.
Hivyo kuanzia leo na kwa muda wote uliobakia, malengo yote
uliyoweka mwanzo yazidishe mara kumi na anza kuangalia ni njia gani
zitakufikisha pale. Ndio weka mara kumi halafu umiza kichwa chako na weka juhudi
mpaka tone la mwisho. Huenda hutafikia mara 10 lakini utafikia mara 5 au hata
mara 3 ambayo ni bora zaidi ya kama ungeendelea na lengo lako la
mwanzo.
TAMKO LA LEO;
Najua naogopa sana kushindwa, najua naona kushindwa ni kama aibu
kwangu. Lakini nimeshajua kwamba kushindwa ni sehemu muhimu sana kwenye maisha
ya kila siku. Kuanzia sasa nitaweka malengo makubwa na ambayo yatanisukuma kila
siku ili kufanya zaidi ya ninavyofanya sasa. Kwa kuweka malengo makubwa hata
kama sitayafikia nitajifunza na kuwa mbali zaidi kuliko nikiweka malengo madogo
na ambayo naweza kuyafikia.
Tukutane kwenye ukurasa wa 176 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita
Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi
yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365
bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo
maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya
facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya
email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na
KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata
utaratibu.
TUPO PAMOJA.