Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakilalamika biashara ni ngumu, biashara hazina wateja, biashara zina ushindani mkali na mengine mengi. Lakini kila ukichunguza biashara nyingi unaona makosa mengi ya kijinga ambayo wafanyabiashara wamekuwa wanafanya na yanawafukuza wateja.

Yaani naweza kusema kwamba kama biashara inakufa, asilimia 90 ya sababu za kufa kwa biashara hiyo zipo ndani ya biashara yenyewe na asilimia 10 tu ndio sababu za nje ambazo wafanyabiashara huamini ndio chanzo kikubwa cha biashara kufa.

Kuna makosa mengi ya kijinga ambayo wafanyabiashara wamekuwa wakiyafanya na yanawagharimu wateja. Nasema ni makosa ya kijinga kwa sababu ukifikiria hasa sababu ya makosa hayo hupati picha. Yanatokana na ujinga au uvivu wa mfanyabiashara mwenyewe.

1. Sina chenji, kwa nini unatoa heka kubwa?

Hivi kweli? Yaani unanilazimisha nisije kwenye biashara yako kama sina hela ndogo? Na unaamini ni jukumu langu mimi kukutafutia wewe chenji? Asante, wacha niende kwa mwingine ambaye atajali kunitafutia chenji. Hivi ndio unavyopoteza mteja, hatakuambia yote hayo ila ataondoka kimya kimya na hutamuona tena. Na hata kama utaendelea kumuona jua hajatokea mwingine wa kumjali, akitokea tu, umekwisha.

SOMA; Unahitaji Mipango Mingapi Ili Kutangaza Kushindwa?

2. Sio muda wake huu/ au muda haujafika bado.

Kila ninapoingia kwenye biashara yoyote huwa najifunza mambo mengi, siondoki bila ya kuona ni kipi kizuri nimejifunza na kipi kibaya cha kuepuka. Nimewahi kuingia kwenye mgahawa siku moja na kuagiza chai, ilikuwa saa nane mchana. Mhudumu akaniuliza kwa mshangao, chai saa hizi? Kama uko makini na biashara yako, usiwapangie watu ni muda gani wanaoweza kupata kile wanachotaka.

3. Mali ikishauzwa hairudishwi.

Hapa ni sawa na kumwambia mteja kwamba ukishanunua tu imekula kwako. Chochote kitakachotokea ni juu yako, mimi sihusiki tena. Ni huduma mbovu sana kwa wateja na kama akitokea mfanyabiashara mwingine anayewajali wateja na kuwasaidia pale wanapopata tatizo, umepotezwa.

Hebu anza kufanyia kazi mambo haya matatu, hasa hilo la kwanza la chenji ni tatizo kwa wafanyabiashara walio wengi. Mteja hatakiwi kujuta pale anapokuja kwenye biashara yako, bali anatakiwa kuondoka akiwa na furaha zaidi ya alivyokuja.

Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.

Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.

Jiunge na COACHING/MENTORSHIP PROGRAM ambapo utapata muongozo wa hatua kwa hatua mpaka ufikie mafanikio kwenye kazi au biashara unayofanya. Bonyeza haya maandishi kupata maelekezo ya programu hii.