Hakuna nchi duniani imewahi kuendelea bila ya watu kufanya kazi. Ukiangalia nchi zote ambazo zina maendeleo makubwa, watu wanafanya kazi sana. Watu wanazalisha bidhaa na huduma ambazo zina thamani kubwa kwa wengine na hivyo kuziuza na kupata fedha. Hakuna nchi inayoweza kuendelea bila ya watu kufanya kazi, tena kazi yenye thamani kwa wengine.
Ni kitu ambacho kimekuwa kinajulikana tangu kuwekwa kwa misingi ya maisha hapa duniani kwamba kazi ndio msingi wa maendeleo. Hata enzi zile ambazo watu walikuwa wakiwinda au kulima, haikuweza kutokea kwamba mtu amelala halafu ghafla chakula kikatokea. Ilikuwa ni lazima mtu atoke na kwenda porini kulima, awe na mbinu nzuri za uwindaji ndio aweze kurudi na kitoweo nyumbani.

 
Wakati kila mtu aliyeendelea duniani akiwa anajua kwamba kazi ndio msingi wa maendeleo, sisi huku Tanzania tunaamini kwamba msaada ndio msingi wa maendeleo. Hivyo ukianzia juu kabisa kama taifa tunatafuta sana misaada. Na hata ukirudi kwa mwananchi mmoja mmoja, wengi wanategemea misaada, kubebwa au kupewa nafasi fulani ya upendeleo ndio aweze kupata kile ambacho anataka.
Kwa kifupi ni kwamba sehemu kubwa ya watanzania hatufanyi kazi. Halafu tunajiuliza kwa nini sisi ni masikini! Sisi ni nchi masikini na tutaendelea kuwa masikini kwa sababu ni sehemu ndogo sana ya watu kwenye jamii zetu ambao wanafanya kazi. Sehemu kubwa wanawaangalia hawa wanaofanya kazi na wao kutafuta njia rahisi ya kupata fedha ambazo wengine wamezitolea jasho. Nchi imekuwa na watu wengi ambao wanaishi kiujanja ujanja na hili linaendelea kutuangamiza.
Katika kundi hili kubwa la watanzania ambao hawafanyi kazi, kuna makundi mawili ndani yake;
Kundi la kwanza ni watu ambao wana kazi ila hawaweki juhudi za kutosha kwenye kazi zao. Hivyo wanakuwa hawazalishi thamani kabisa au thamani wanayozalisha ni ndogo sana. Mfano mzuri kwenye kundi hili ni wafanyakazi wengi waliopo kwenye taasisi nyingi za umma. Tumekuwa tunaona jinsi ambavyo wengi wa wafanyakazi hawa hawajitumi kufanya kazi. Watu hawa wanakuwa na vishughuli vingi vidogo vidogo ambavyo vinapunguza muda w akufanya kazi.
Kwa mfano mtu anachelewa kufika kazini, anaweza kuwa na sababu au hata sababu hana. Akifika kazini anafanya vitu ambavyo havina uzalishaji wowote. Labda kupanga panga vitu au kuzurura zurura kwenye mtandao. Baada ya muda kidogo anakwenda mapumziko ya kunywa chai, hapo nako anapoteza muda wa kutosha. Anarudi tena kwenye kazi, anagusa kazi kidogo, halafu anapoteza tena muda wa kutosha, huku akijiandaa kwa mapumziko ya chakula cha mchana. Akienda mapumziko haya anapoteza tena muda wa kutosha, na akirudi anagusa kazi kidogo na kujiandaa kuondoka.
Katika masaa nane ya kazi kwa siku, watu wengi wanafanya kazi chini ya masaa manne. Hayo masaa manne mengine yanapotelea kwenye mapumziko, utumiaji wa mitandao, vikao visivyo vya msingi na mambo mengine mengi ambayo hayana uzalishaji wowote kwenye eneo la kazi. Hii ni hali ya kutisha sana kwa taifa ambalo linapigana ili kuendelea, ni vigumu sana kuendelea kama watu hawapo tayari kuweka juhudi kubwa kwenye kazi zao na kuzalisha kitu chenye thamani kwa wengine.
SOMA; Kilichotokea Afrika Kusini Na Somo Kubwa La Sisi Watanzania Kujifunza.
Kundi la pili ni watu ambao wana kazi ambazo hazina thamani kabisa. Hili ni kundi kubwa pia la watu ambao wana kazi lakini kazi hizi hazina thamani yoyote kwa wengine na hata kwa maendeleo ya nchi. Tunaweza kusema kwamba hili ni kundi ambalo linaonekana kama wana kazi ila ukweli ni kwamba hawana kazi yoyote na kikubwa wanachofanya ni kuwanyonya wale wachache ambao wanafanya kazi.
Kundi hili la watu walio na kazi ambazo hazina thamani lina makundi madogo madogo kutokana na kazi ambazo watu wanafanya. Hapa nitajadili makundi haya machache ya kazi ambazo hazina thamani yoyote kwenye uchumi wetu kama taifa na hivyo kuwa tunapoteza nguvu kazi na kutufanya tushindwe kufanikiwa.
1. Wapiga debe.
Kupiga debe ni kazi ambayo inaonekana ni rasmi kwa watu wengi, lakini ukweli ni kwamba hakuna thamani yoyote kiuchumi kwa mtu kupiga debe. Magari yote yanafahamika yanaelekea wapi na kwa bahati nzuri mengi yameandikwa kabisa. Na wewe mwananchi unapotoka nyumbani unajua kabisa ya kwamba unaelekea wapi. Sasa unatoka kwa akili zako timamu, ina unapofika stendi kuna mtu amejipa kazi ya kukuonesha gari la kupanda ni lipi! Yaani kweli kwamba mtu hawezi kupanda gari mpaka akipige debe? Kwamba gari ya ubungo ni hii, njoo upande, twende!!
Hii ni kazi ambayo pamoja na vijana wengi kujishikiza haina thamani yoyote. Tunapoteza rasilimali watu kwa kazi ambayo haina thamani yoyote. Na watu hawa wanategemea kulipwa kila wanapomwambia mtu apande gari ambalo alikuwa analiona na tayari anajua ni wapi anakwenda.
2. Dalali wa dalali.
Udalali ni kazi ambayo ina thamani, kwa sababu kuna watu ambao wanataka kununua kitu ila hawana muda wa kukitafuta vizuri. Au kuna watu ambao wanataka kuuza vitu lakini hawana muda wa kutafuta mteja mwenye sifa nzuri. Hapa ndipo uhitaji wa dalali unapokuwa wa thamani na anaweza kuwaunganisha wauzaji na wanunuaji. Kuna thamani kubwa kwenye udalali. Ila ndani ya udalali huu kuna udalali ambao hauna thamani kabisa. Na huu ni udalali wa dalali. Yaani kuna dalali wa dalali. yaani kwa dili moja linapita kwa madalali kadhaa ndio limfikie mhitaji. Sasa hapa katikati kuna watu wengi ambao hawajaongeza thamani yoyote ila wanataka walipwe.
Ngoja nikupe mfano ili uelewe vizuri. Chukua mfano kuna mkulima wa mahindi huko kiteto na soko kubwa la mahindi lipo dar es salaam. Mkulima huyu hawezi kuja kuuza mahindi yake moja kwa moja dar es salaam. Hivyo inabidi auze kwa mtu wa kati na yeye ndio aje kuuza dar es salaam. Sasa katika mchakato wa kuyatoa mahindi kwa mkulima kiteto, mpaka yamfikie mlaji wa dar kuna madalali wengi sana wanahusika hapo. Kuna dalali ambaye atamuunganisha mteja shambani na mnunuaji, anapata fedha yake. Mnunuaji akitoka na mzigo na kufika sokoni, kuna dalali wa kununua huu mzigo na kuuza kwa wanunuaji wa jumla, huyu naye analipwa. Mnunuaji wa jumla anapotaka kuuza kwa muuzaji wa reja reja hapa nako kuna dalali naye pia analipwa. Kwa mlolongo huu mrefu wa madalali unakuta kilo ya mahindi kiteto inauzwa tsh mia mbili ila inapofika kwa mtumiaji wa mwisho inakuwa tsh mia nane. Sehemu kubwa ya fedha hii inaishia hapo kati kati ambapo kuna watu wengi hawazalishi ila wanategemea kupata kipato.
SOMA; Mambo Matano(5) Ambayo Ni Marufuku Kufanya Kwenye Eneo La Kazi.
Tufaye nini ili tuweze kuendelea?
Hakuna miujiza yoyote ambayo tunahitaji ili kuendelea, bali tunahitaji kurudi kwenye msingi wa maendeleo ambao ni kufanya kazi. Kazi ndio msingi wa maendeleo. Na sio kazi tu, bali kazi yenye thamani kwa wengine na kuifanya kwa juhudi na maarifa.
Kama tutaendelea kuwa na watu wengi ambao wana kazi ila hawaweki juhudi au wana kazi ila hazina thamani, tutaendelea kuishi kwa kutegemea misaada na hata misaada hii haiwezi kuwa na manufaa kwetu kwa sababu watu wengi hawafanyi kazi.
Tunatakiwa kuwa tayari kuweka juhudi za ziada, kuwa tayari kuboresha kile ambacho tunafanya na kuwa na hamasa ya kufanya zaidi ili kuongeza thamani zaidi.
Tunatakiwa kuwa na watu ambao wanazalisha bidhaa na huduma ambazo zinaboresha maisha ya watu wengine kwa kiasi kikubwa. Tuweze kuuza vitu hivi ndani na nje ya nchi na hii ndio itatuletea maendeleo. Hakuna njia ya mkato kwenye hili, ni lazima kila mmoja wetu afanye kazi.
Haya yote yanaanza na mimi na wewe, tufanye kazi, tuache janja janja, njia yoyote unayofikiria ni rahisi ya kupata maendeleo ambayo haihusishi kufanya kazi ni njia ya uongo na itakuwa na madhara makubwa kwako au kwa wengine hapo baadaye.
Kazi ndio msingi wa maendeleo, kila mmoja wetu na afanye kazi yenye thamani kubwa kwa wengine. Huu ndio msingi wa mafanikio binafsi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Nakutakia kila la kheri katika mapambano ya kujikwamua kiuchumi na kujiendeleza wewe binafsi na taifa kwa ujumla.
TUPO PAMOJA.
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz