Kama umejitoa ili kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako,
unahitaji kujifunza jinsi ya kutumia muda wako vizuri. Na kwa kuwa siku ina
masaa 24 tu na hakuna anayeweza kuyazidisha, hakuna njia ya kuongeza muda ambao
tunao.

Kwa kuwa tunahitaji muda mwingi zaidi wa kufanya kile
tunachofanya kwa ubora, basi tunahitaji kupunguza mambo mengi tunayofanya ili
tuokoe muda mwingi.

Ili kupata muda mwingi nimekuwa nawashauri watu kufanya
yafuatayo, ambayo hata mimi nafanya; usifuatilie habari, punguza sana muda
unaotumia kwenye mitandao ya kijamii, tenga muda wa kuwa mbali na simu yako pale
ambapo unafanya kazi inayohitaji umakini wako.

Watu wamekuwa wakipinga sana baadhi ya mambo haya, hasa
kutokufuatilia habari au kukaa mbali na simu. Watu wamekuwa wakisema lakini
nitapitwa…..

Najua na wewe unaona usipoangalia au kusoma habari siku moja
unaona unapitwa. Yaani unapitwa na habari ya mtu aliyejinyonga huko mpanda,
ukishaisikia inakusaidia nini? Utaniambia kuna habari muhimu kuhusu mambo
yanayoendelea. Kama habari ni muhimu kweli zitakufikia tu. Kwa mfano kama nchi
inaingia vitani, utajua hata kama huangalii habari. Lakini mambo ya mgombea gani
kapata wadhamini wangapi sio habari za mtu makini kushabikia, ni kupoteza muda
wako.

SOMA; Unacho Kila Unachohitaji Ili Kufanikiwa.

Asilimia kubwa ya watu wanaotumia simu ni kama wamefunga ndoa na
simu hizo. Kila dakika mtu upo na simu na hazipiti dakika tano unaangalia kama
kuna mtu katuma ujumbe au kapiga hukusikia. Na hata unapokwenda kulala, unaiweka
pembeni ya kichwa chako, ili usipitwe. Unapoteza muda mwingi sana, ni vigumu
kufanya kazi yenye maana huku unajibu ujumbe wa simu au kupokea simu kila mara.
Ni afadhali uweke simu hiyo kimya kabisa na ufanye kazi yako, bila ya
kuiangalia. Utasema lakini watu watanipigia na kunikosa, nitakosa dili nzuri.
Ukweli ni kwamba, na hapa nakuambia kwa uzoefu, kama mtu ana shida ya
kuwasiliana na wewe kweli, atakutafuta hata mara kumi. Ila anayepiga mara moja
na kuacha, hata ukija kumpigia baadae hakuna jambo kubwa na la haraka sana
alilokuwa anakuambia. Mwingine atasema labda mtoto wangu ataumwa ghafla inabidi
nipate taarifa, sawa umeshazipata unafanya nini? Maana hata kama wewe ni daktari
huwezi kumtibu mtoto wako, itabidi apelekwe tu hospitali. Sisemi usikae na simu
siku nzima, bali masaa machache hivyo taarifa hizi utazipata baadae na utafanya
maamuzi sahihi, huku umeshakamilisha kazi uliyopanga kufanya.

TAMKO LA LEO;

Nimekuwa najidanganya kwamba nitapitwa na hivyo kuwa karibu na
habari, kuwa karibu na mitandao na kuwa karibu na simu yangu kila mara. Hali hii
imekuwa inanipotezea muda wangu mwingi kwa kufuatilia vitu visivyo na maana na
kukosa muda w akufuatilia yale ambayo yataniletea mafanikio. Kuanzia sasa
natenga muda wangu wa kufanya mambo muhimu na muda huu hautaingiliwa na kitu
kingine chochote.

Tukutane kwenye ukurasa wa 179 kesho, Like page yangu ya
Coach
Makirita Amani
uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha
kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365
bonyeza hapa na uweke email.

Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo
maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya
facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya
email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na
KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata
utaratibu.

TUPO PAMOJA.