Kama unafanya biashara kubwa maana yake una watu wengi ambao wanakusaidia kwenye biashara hiyo. Biashara yako haiwezi kukua na kuendelea kama huna watu wazuri ambao wanafanya kazi kwenye biashara hiyo. Na hata kama una biashara ndogo malengo yako ni kukua zaidi ya hapo ulipo sasa. Ili kukua utahitaji kuwa na wafanyakazi wenye uwezo mzuri na watakaoiwezesha biashara yako kukua.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifikiri kwamba wakishapata wafanyakazi wazuri na wakawaajiri basi kazi yao imekwisha na hivyo wanasubiri tu kuvuna matunda yanayotokana na wafanyakazi hao. Na hata wengine hufikiri kwamba ukishakuwa na wafanyakazi wenye uwezo mzuri na ukawa unawalipa mshahara mzuri basi watafanya kazi vizuri na wewe utapata faida kubwa. Hili ni kweli kwa siku za mwanzoni za kazi ila kadiri muda unavyokwenda ufanisi wa wafanyakazi wako unapungua.
Tumekuwa tukijadili hapa mara nyingi kwamba mazingira ya biashara yamebadilika sana. Na hata sasa hivi mabadiliko mengi sana yanaendelea. Hivyo kuwa na wafanyakazi wenye uzoefu wa miaka zaidi ya miwili iliyopita ni mzigo mkubwa kwenye biashara yako. Hata kama wafanyakazi walikuwa wazuri kiasi gani siku za nyuma, hii haimaanishi kwamba hata sasa wataendelea kuwa wawili. Wafanyakazi wanatakiwa kwenda na mabadiliko yanayotokea kwenye ulimwengu wa biashara. Na njia pekee ya kuwawezesha wafanyakazi wako kuwa hivi ni kutoa mafunzo ya mara kwa mara.
Wafanyakazi wako wanahitaji sana mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kwenda vizuri na mabadiliko yanatotokea kwenye ulimwengu wa biashara na hata kwenye biashara mnayofanya. Ni muhimu sana wewe mmiliki wa biashara kuandaa na kuendesha mafunzo haya mara kwa mara na kuhakikisha kila mfanyakazi wako anapata mafunzo haya. Kwa kuwa na mafunzo haya mfanyakazi ataongeza ufanisi wake kwenye kazi na kuzalisha zaidi.
Mafunzo unayohitaji kwa wafanyakazi wa biashara yako ni ya aina mbili;
Aina ya kwanza ni mafunzo ya maarifa ya biashara na ujuzi unaohusiana na biashara mnayofanya. Haya ni muhimu sana kufanyika mara kwa mara ili kuwakumbusha wafanyakazi yale mambo ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa biashara hiyo. Pia hapa watapata nafasi ya kujifunza mambo mapya ambayo yanaendelea kwenye biashara na hatua za kuchukua ili kunufaika na mambo hayo mapya. Kwa mfano inawezekana kuna mabadiliko ya kiteknolojia ambayo yanaweza kuboresha sana utendaji kazi wenu kwenye biashara. Kwa wafanyakazi wako kupata mafunzo haya itawawezesha kujua jinsi ya kutumia teknolojia hiyo mpya katika utendaji wao.
Aina ya pili ni mafunzo ya kuhamasisha. Unahitaji wafanyakazi ambao wana hamasa kubwa ya kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa. Kwa kuwa na wafanyakazi wenye hamasa hivi wataweza kufikia malengo yao na wewe mfanyabiashara kufikia malengo yako pia. Ila unapokuwa na wafanyakazi ambao ni wavivu na hawawezi kufanya kazi wenyewe mpaka wasukumwe, biashara yako ipo kwenye matatizo makubwa. Unahitaji kutoa mafunzo ya kuhamasisha wafanyakazi wako mara kwa mara. Mafunzo haya yatawafanya waone kwamba wao ni sehemu muhimu ya biashara yako. Na pia wataona kwa kuweka juhudi sio kwamba wanakunufaisha wewe tu, bali hata maisha yao yanakuwa bora zaidi. Wanajua mafanikio ya biashara yako ndio mafanikio yao. Na kama biashara yako ikifa basi na wao hawana ajira.
Mafunzo yote haya ya aina mbili unaweza kuyatoa wewe mwenyewe kama mmiliki wa biashara kwa sehemu moja, ila pia utahitaji mtoaji mafunzo ya kibiashara na kuhamasisha kuja kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wako. Unapochagua mtu wa aina hii hakikisha unakaa naye chini kwanza na kukubaliana ni mafunzo ya aina gani unataka wafanyakazi wako wayapate, ili aweze kutoa mafunzo yanayoendana na malengo yako ya kibiashara. Kama utahitaji mtoaji wa mafunzo kwa wafanyakazi wako tuwasiliane.
Nakutakia kila la kheri kwenye kuendesha biashara yenye mafanikio.
TUPO PAMOJA.