Baada ya kujua ujasiriamali ni nini na sifa za kuwa Mjasiriamali bora, Leo tutajifunza uwekezaji ni nini na vitu vya kuzingatia ili uweze kuwa mwekezaji mzuri. Watu wamekuwa wakipata mtaji, au fedha lakini wanaogopa kuwekeza kwa sababu hawajui wapi pa kuanzia.
Uwekezaji ni nini?
Uwekezaji ni kitendo cha kutumia rasilimali, labda rasilimali fedha na kuitengeneza, kuijenga au kununua rasilimali nyingine kwa matarajio kwamba hiyo rasilimali utakayokuwa umeijenga au umeinunua itakuingizia fedha au pato baadaye katika namna ambayo itarudisha zile fedha ambazo ulizitumia na kukuletea faida zaidi. Unatakiwa kuijenga rasilimali ili irudishe pato au fedha uliyotumia katika uwekezaji na kupata faida.
Unaweza kuwekeza rasilimali muda wako, rasilimali fedha, na rasilimali nguvu yako na nk.
Vitu Vya Msingi Vya Kuzingatia Ili Uweze Kuwa Mwekezaji Bora au Mzuri

  1. Mtu Mwenye Uwezo Wa Kupata Taarifa;

Hii ni sifa ambayo inamsaidia mwekezaji kupata fursa zaidi katika uwekezaji. Katika uwekezaji taarifa ni fursa kubwa sana, unaweza kupata taarifa kupitia intaneti ukapata taarifa nyingi juu ya uwekezaji au ukasoma vitabu, ukajifunza kupata taarifa kupitia watu waliofanikiwa katika uwekezaji ambao unaufanya au unatarajia kuufanya.

  1. Mtu Mwenye Uwezo wa Kupima Majanga;

Hapa inahusisha faida na hasara ni namna gani au jinsi gani mwekezaji anaweza kuchukua risk au hatari, uwezo wa kupima kabla ya kufanya maamuzi, sasa mwekezaji akiwa ana uwezo wa kupima majanga atakuwa katika nafasi nzuri ya kukabiliana na changamoto na hapo atakuwa amepata sifa za kuwa mwekezaji mzuri.
SOMA; Hivi ndivyo unavyoweza kununua Hisa katika soko la Hisa la Dar es salaam (DSE)

  1. Mtu Mwenye Uwezo wa Kutengeneza Mtandao;

Mwekezaji anatakiwa awe na uwezo wa kujenga mahusiano na watu. Huwezi kufanikiwa bila watu, inahitaji utengeneze mtandao mkubwa wa watu ujenge mahusiano bora ili uweze kupata wateja wazuri baadae kulingana na uwekezaji wako ambao unaufanya au unatarajia kuufanya.

  1. Mtu Mwenye Tabia ya Kujifunza ;

Kama wewe ni mwekezaji halafu huna sifa ya kujifunza kila siku basi wewe ni rahisi kufeli, mfano kuna uwekezaji wa hisa ,uwekezaji wa hisa unahitaji kujifunza kila siku jinsi thamani ya fedha inavyobadilika kila siku. Hivyo mwekezaji anatakiwa kupata taarifa kila siku ambazo zitamsaidia kukabiliana na changamoto au jinsi ya kuboresha uwekezaji wako.
Kwa hiyo, Kila binadamu ni mwekezaji, uwekezaji katika biashara unawekeza rasilimali fedha, ambayo itakuletea faida zaidi. Usisubiri mpaka upate rasilimali fedha ndio uanze kuwekeza Anza kuwekeza SASA katika uwekezaji wa akili, wekeza katika ubongo wako kwani chakula cha ubongo ni maarifa.
Huna mtaji, anza kuwekeza katika rasilimali muda wako, akili yako, rasilimali nguvu yako nk. soma vitabu mbalimbali, sikiliza vitabu vilivyosomwa, hudhuria semina, jifunze kwa waliofanikiwa.
‘’ Maarifa ni kila kitu katika uwekezaji na ubongo wako ni injini ya mafanikio’’
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com