USHAURI; Wakati Sahihi Na Wakati Mbaya Wa Kuchukua Mkopo Wa Biashara Benki.

Habari za leo mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA, naamini unaendelea vizuri na harakati zako za kuboresha maisha yako kila siku. Kumbuka mafanikio hayatokei mara moja tu, ila yanajengwa kwa tabia ndogondogo unazorudia kufanya kila siku.
Katika safari hii ya mafanikio, kuna vikwazo vingi sana ambavyo vinakurudisha nyuma. Kuna vikwazo ambavyo unaweza kuvifanyia kazi na hivyo kuvivuka ila kuna vikwazo vingine vinaweza kuwa vikubwa sana kwako na hivyo kushindwa kujua unaweza kuondokanaje navyo. Ni katika hali hiyo ambapo tunakutana kwenye kipengele hiki cha USHAURI WA CHANGAMOTO mbalimbali ambazo zinakuzuia wewe kuweza kufikia malengo uliyojiwekea.
Leo katika kipengele hiki tutaangalia wakati sahihi na wakati mbaya wa kuchukua mkopo wa biashara benki. Swala la uchukuaji na kulipa mikopo ya benki imekuwa changamoto kwa watu wengi sana. Kuna wengi ambao wanaogopa kabisa kuchukua mkopo kutokana na mambo waliyopitia baada ya kuchukua mkopo au waliyoona wenzao wanapitia baada ya kuchukua mkopo. Baadhi ya hali hizi zimewafanya baadhi ya watu kuona kuchukua mkopo benki ni sawa na kujiandaa kufilisiwa. Leo tutajadili yote haya na kuona ni hatua gani uchukue.

 
Kabla hatujaingia kujadili changamoto hii ya leo, naomba tusome maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusiana na changamoto hii;

Changamoto inayonisumbua nipale wafanyabiashara wenzangu wanaponishauri niingie kwenye mikopo kwa kigezo cha kwamba HAWATAJIRIKI BILA KUKOPA wengi walifanikiwa wamekopa ndio nashindwa chakufanya ili kufikia malengo, na huwa nawaona wanaokopa hufilisiwa na mabenki naomba ushauri.
Z. M

Kuna kauli nyingi za uongo au ambazo hazijakamilika huwa zinazunguka sana kwenye jamii. Kwa sababu tu kauli ni maarufu basi wengi huamini ndio ukweli na kuishi nao, mpaka pale wanapoumia ndio wanagundua kwamba walikuwa wakidanganyika na wao wenyewe kujidanganya.
Moja ya kauli za aina hii ni kwamba HUWEZI KUTAJIRIKA BILA YA KUKOPA, kauli hii imekuwa maarufu sana siku za hivi karibuni kwa sababu imekuwa inatumiwa na wafanyabiashara wakubwa sana na waliofanikiwa. Kwa kuvutiwa na mafanikio ya wafanyabiashara hawa wakubwa, watu wamekuwa wakikubali kauli hii na kuichukua kama ilivyo. Wanapoifanyia kazi ndio wanagundua kwamba kuna vitu vingi walipaswa kujua kabla ya kuamini kauli hiyo.
SOMA; Mambo Matano(5) Ambayo Ni Marufuku Kufanya Kwenye Eneo La Kazi.
Kauli kwamba huwezi kutajirika, hasa kwenye biashara bila ya kuchukua mkopo, ni ya kweli kabisa. Kwa sababu unahitaji kukuza biashara yako zaidi na zaidi na hili litawezekana kama utaweza kupata fedha kutoka nje ya biashara hiyo. Lakini kauli hii haijakamilika na ndio maana wengi wa wanaoitumia wanaishia kupata hasara na kufilisiwa mali zao. Kauli hii haijakamilika kwa sababu haikuamii ni wakati gani wa kukopa na wakati gani sio wa kukopa. Haiwezekani kila wakati na kila mtu aweze kukopa, haiwezekani. Pale watu wanapolazimisha hili ndio wanaishia kufilisiwa na kulaani kwamba mikopo haifai, kumbe wao wenyewe hawakujua wakati sahihi kwao kukopa.

Mambo muhimu unayotakiwa kujua kabla hujachukua mkopo wa biashara benki.

Kabla hujaingia kwenye mkumbo wa kuchukua mkopo kwa sababu bila mkopo huwezi kutajirika, kuna mambo muhimu sana unayotakiwa kuyajua ambayo yatakufanya uweze kutumia mkopo huo vizuri na ukakuletea mafanikio.
1. Benki inafanya biashara kama wewe unavyofanya biashara.
Kuna baadhi ya watu hufikiri kwamba benki ipo pale kwa sababu ya kuwasaidia fedha tu, ukweli ni kwamba benki inafanya biashara kama wewe unavyofanya biashara. Hakuna mfanyabiashara yeyote anayetaka kupata hasara na hivyo benki inahakikisha inamkopesha mtu ambaye hawatapata hasara. Wao hawaangalii kama faida yao wataipata kama biashara yako itafanikiwa, wao wanajua pa kuipata faida yao hata kama biashara yako itakufa. Unajua ni wapi? Soma hapo chini.
2. Benki inapokuambia unakopesheka maana yake pia unafaa kufilisi.
Siku hizi benki ndio zinafuata watu na kuwaomba kuwakopesha, tofauti na zamani ambapo wewe ndio ungeenda kuiomba benki ikukopeshe na wakati mwingine wakunyime mkopo hata kama una vigezo(tuseme asante kwa uhuru wa kibiashara uliotengeneza ushindani mkali). Sasa benki itakuta kwako na kukuambia kwamba wewe unakopesheka, hawamaanishi kwamba wanakupenda sana wewe na hivyo wapo tayari kukusaidia fedha, hapana. Wanamaanisha kwamba hata kama biashara yako itakufa basi wanazo njia za kuweza kurudisha fedha zao kwa kuuza mali zako nyingine. Elewa vizuri kauli hizi.
3. Chukua mkopo ukiwa unajua unakwenda kuufanyia nini.
Kamwe, kamwe, kamwe usichukue mkopo halafu ndio uanze kufikiria utaufanyia nini, utaumia. Jua kwanza ni eneo gani kwenye biashara yako ambalo linahitaji msaada zaidi na hakikisha biashara inajiendesha kwa faida ndio uchukue mkopo. Na ukishachukua mkopo tafadhali sana utumie kwenye shughuli hiyo ya kibiashara tu. Usithubutu hata kidogo kuchukua mkopo huo na kuingiza kwenye matumizi mengine, hata kama unafikiria kwamba utarudisha baadaye, haitatokea. Na unapokosa nidhamu ndogondogo kwenye matumizi ya mkopo huo ndio unaanza kukaribisha uzembe na kukaribisha kufilisiwa.
SOMA; Kama Unataka Kumaliza Matatizo Yako Ya Fedha Fanya Kitu Hiki Kimoja.

Wakati sahihi wa wewe kuchukua mkopo.

Ili uweze kunufaika na mkopo wa biashara utakaochukua, unahitaji kujua ni wakati gani sahihi wa kuuchukua. Chukua mkopo wa biashara pale ambapo unafikia vigezo hizi.
1. Biashara inajiendesha kwa faida.
Kwa hali ya kawaida ya kibinadamu utaniambia wakati mzuri wa kuchukua mkopo ni pale ambapo biashara inapata hasara. Fanya hivyo na kama umeweka nyumba rehani uanze kutafuta nyumba ya kupanga. Ukweli ni kwamba kama biashara inajiendesha kwa hasara na bado hujajua hasara hiyo inatokana na nini na kurekebisha kwamba, kuchukua fedha nyingi na kuweka kutazidisha hasara hiyo mara dufu. Kama unaendesha biashara ya milioni kumi na unapata hasara ya milioni, ukiweka milioni mia utapata hasara kubwa zaidi ya unayopata sasa. Kama biashara inajiendesha kwa hasara, tatua kwanza tatizo hilo.
2. Unajua ni nini unakwenda kufanya na mkopo huo.
Chukua mkopo ukiwa tayari unajua unakwenda kuufanyia nini na ufanyie kitu hiko tu. Wanasema unapokuwa huna fedha unakuwa na mawazo mengi sana na mazuri, unapokuwa na fedha mawazo yote mazuri yanapotea. Ni kweli kabisa na hii inatokana na mtu kuona vitu vya kutamanisha pale ambapo tayari ana fedha. Utakapokuwa na fedha utaona vitu vizuri ambavyo unaweza kuvinunua kwa fedha hizo. Usijaribu kutumia mkopo huo kwa kitu kingine chochote.
3. Una nidhamu ya fedha.
Kama huna nidhamu ya fedha ndugu yangu, chonde chonde tengeneza kwanza nidhamu hii kabla hujachukua mkopo. Kwa kukosa nidhamu ya fedha unakaribisha matatizo hayo yote hapo juu na unapochukua mkopo unazidi kuongeza matatizo yako ya kifedha.

Wakati mbaya wa kuchukua mkopo wa biashara.

Kuna wakati mbaya sana kwako kuchukua mkopo wa kibiashara. Kama huna sifa hizo hapo juu tayari kwa sasa huna uwezo mzuri wa kuchukua mkopo na kuurudisha, hata kama benki inakwambia unakopesheka. Kama biashara haijiendeshi kwa faida, kama huna matumizi na mkopo na kama huna nidhamu ya fedha, ni vyema kusubiri kwanza urekebishe mambo haya ndio uingie kwenye mkopo. Kama unaona kusubiri urekebishe kwanza haya mapungufu yako ni kuchelewa kufikia utajiri, jiingize kwenye mkopo huo na uondoe kabisa ndoto zako za kuwa tajiri.

Maneno ya mwisho kwa msomaji aliyetuandikia changamoto hii.

Ndugu, kwanza usichukue mkopo kwa sababu wafanyabiashara wenzako wanakuambia uchukue mkopo. Mkopo sio fasheni ya nguo kwamba kwa sababu wengine wamevaa basi na wewe unaweza kuvaa. Ndio maana nimejaribu kukupa misingi ya kukuongoza wakati wa kuchukua mkopo. Chukua mkopo wa biashara yako pale ambapo wewe una uhitaji na unajua unakwenda kuuweka wapi ili uweze kukulipa. Hakuna anayejua biashara yako zaidi yako wewe mwenyewe, ndio maana hata kama watu watakushauri kiasi gani, bado wewe mwenyewe ndio utafanya maamuzi ya mwisho kuhusiana na biashara yako.
Pili wafanyabiashara wengine kuchukua mkopo na wakafilisiwa haimaanishi na wewe ukichukua utafilisiwa. La hasha. Wale walichukua mkopo kichwa kichwa bila ya kukaa chini na kujua kama kweli wanahitaji mkopo ule na kama wana vigezo vya kuweza kuulipa. Wewe mpaka sasa umeshapata elimu nzuri sana itakayokusaidia kwenye mambo ya mkopo(na kama hii haijakutosha nipigie simu kwenye 0717396253 tuongee zaidi). Tumia elimu hii kwenye kuchukua mkopo, kuutumia vizuri na hatimaye uweze kuulipa na wewe ufaidike na mkopo huo. Usiogope mkopo kwa sababu tu kuna wengine ambao wamechukua wamefilisiwa, utajinyima fursa nyingi kwa kuwa na mawazo ya aina hii.
Mikopo ni mizuri sana kwenye biashara kama itachukuliwa kwa wakati sahihi na kuwekwa kwenye matumizi sahihi. Ila kama mikopo itachukuliwa kwa kauli za kishabiki ni sumu kubwa sana kwa maendeleo ya biashara yoyote. Ni muhimu kujua wakati sahihi na ambao sio sahihi kwako wewe kuchukua mkopo wa kibiashara. Achana na kauli za kibiashara utakazoambiwa na benki, au wafanyabiashara wengine. Wewe pekee ndio unaijua biashara yako vizuri. Fanya maamuzi sahihi kwa ajili ya biashara yako.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
TUPO PAMOJA
Makirita Amani 
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: