Tarehe saba ya mwezi wa saba kila mwaka ni sikukuu ya wafanyabiashara. Ni siku maalumu ambayo imetengwa na serikali kwa ajili ya wafanyabiashara kuazimisha kile ambacho wamekuwa wanafanya kwenye biashara zao. Msimu huu wa sabasaba kila mwaka hutawaliwa na maonesho ya kibiashara kwenye viwanja mbalimbali nchini. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakitumia msimu huu kutangaza biashara zao na kupata wateja wengi zaidi.

Leo tutajadili jinsi unavyoweza kutumia msimu huu vizuri kwa maendeleo ya biashara yako. Kwa sababu biashara yako haitadumu kwa kipindi hiki cha sabasaba tu, unahitaji kuwa na msingi sahihi ambao utawezesha biashara yako kukua zaidi na zaidi kila mwaka. Hapa nimekuandalia mambo muhimu ya kila mfanyabiashara kutafakari kwenye msimu huu wa saba saba.

1. Je biashara yako ina mchango chanya kwenye jamii.

Kama serikali imetujali wafanyabiashara mpaka kutuwekea siku yetu, imeona kwamba sisi ni watu muhimu kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Na huu ndio ukweli usiopingika, biashara ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi. Lakini je kwa jinsi unavyofanya biashara wewe, unachochea kukua kwa uchumi? Je unatoa bidhaa au huduma ambazo ni bora kwa watu wengine na zinawasaidia kuboresha maisha yao? Kwa sababu kama hufanyi hivi ni bora ukaachana na biashara hiyo kabla haijakufia mwenyewe kwenye mikono yako. Kuna ushindani mkubwa sana kwenye biashara kwa sasa na hivyo kama hutoi thamani utapotea.

2. Je miaka inavyokwenda biashara yangu inakua?

Usisubiri sabasaba ndio ukatangaza biashara yako na kukazana kupata wateja. Biashara yako haiwezi kuwa inategemea wateja wakati wa sabasaba tu. Swali ni kwamba, sabasaba ya mwaka jana biashara yako ilikuwa wapi na sabasaba ya mwaka huu biashara yako iko wapi. Pima maeneo yote muhimu ya biashara yako. Anza na mtaji, wateja, mauzo, sifa za biashara yako, ubora wa wafanyakazi na mengine mengi. Pia vitu vyote kwa mwaka mzima tangu sabasaba iliyopita na uone je unakwenda mbele au unarudi nyuma.

3. Jifunze kupitia biashara nyingine.

Hata kama wewe hutashiriki kwenye maonesho haya ya biashara, huu ni wakati mzuri sana wa kujifunza kuhusu biashara nyingine. Huu ndio wakati pekee ambapo unaweza kuzikuta biashara nyingi katika eneo moja. Na kila utakapoingia kwenye biashara utapewa maelezo yote muhimu kuhusiana na biashara hiyo na huduma au bidhaa wanazotoa. Hapa unaweza kujifunza mengi sana kama unafanya biashara inayofanana na ile. Na hata kama unafanya biashara tofauti unaweza kujifunza mbinu mpya unazoweza kutumia kwenye biashara yako na zikakuletea faida kubwa. Tafakari ni vitu gani unajifunza kupitia biashara nyingine. Hata kama hutaenda kwenye viwanja vya maonesho, bado kuna biashara nyingi zinakuwa na vipindi vya kwenye tv au redio.

4. Ni maeneo yapi unahitaji kuboresha zaidi.

Kama unataka sabasaba ijayo kuwe na tofauti kubwa kwenye biashara yako ukilinganisha na ilivyo sasa, lazima kuna maeneo ambayo unatakiwa uyabadili na kuyaboresha zaidi. Hili ni jambo muhimu la kutafakari katika kipindi hiki. Unajua ya kwamba kama utaendelea kufanya biashara jinsi ambavyo umekuwa unafanya, utaendelea kupata majibu ambayo umekuwa unapata. Kwa kuwa wewe unataka kufanikiwa kupitia biashara, basi unahitaji kuja na mikakati ambayo utaifanyia utekelezaji kwa mwaka mmoja ujao na utabadili sana biashara yako. Angalia wewe mwenyewe ni maeneo gani ambayo bado hujayafanyia kazi vizuri na pia angalia ni vitu gani umejifunza kutoka kwenye biashara nyingine na weka vitu hivi pamoja. Itakusaidia sana kusonga mbele kwenye biashara yako.

5. Ni mabadiliko gani yanayotokea kwenye biashara unayofanya.

Mara nyingi biashara zetu huwa zinatutinga mpaka tunakosa muda wa kufuatilia ni mabadiliko gani yanayoendelea kwenye ulimwengu wa biashara. Hii ni hatari sana kwa sababu kama utachelewa kujua mabadiliko yanayoendelea unaweza kuachwa nyuma au kuondolewa kabisa kwenye biashara hiyo. Tumia wakati huu kutafakari ni mabadiliko gani yanayoendelea na jinsi gani unavyoweza kuyatumia kukuza biashara yako zaidi. Jifunze kwa kuangalia mambo yanayoendelea kwenye biashara na pia kwa kuangalia maonesho ya biashara nyingine. Hapa utapata taarifa muhimu za mambo mapya yanayoingia kwenye biashara na jinsi unavyoweza kuyatumia.

Msimu huu wa sabasaba sio msimu wa kufanya maonesho ya kibiashara pekee, bali ni msimu wa kila mfanyabiashara kupata muda wa kutafakari kuhusu biashara yake na biashara kwa ujumla ili aweze kutoa bidhaa na huduma ambazo ni bora sana kwa wateja na hii ikaleta maendeleo kwa mfanyabiashara, mteja na taifa kwa ujumla.

Heri ya sikukuu ya sabasaba kwa wafanyabiashara wote.