Mpaka sasa umeshajifunza mambo mengi sana kuhusu mbinu za
kuboresha kazi yako, biashara yako na hata maisha yako kwa ujumla. Lakini mbona
bado huchukui hatua yoyote ili kuweza kunufaika na yale ambayo
unajifunza?

Mpaka sasa unajua kabisa ya kwamba kwa kufanya kile ambacho kila
mtu anafanya utaendelea kupata matokeo ambayo kila mtu anayapata na ambayo sio
mazuri sana. Lakini mbona unaendelea kufanya hivyo?

SOMA; Maisha Ni Mchezo Na Sheria Za Kuushinda.

Mpaka sasa unajua kabisa kulalamika au kulaumu wengine
hakutakupatia wewe chochote unachotaka, sana sana kutakufanya ujione kama yatima
ambaye hana msaada wowote. Lakini bado unaendelea kulalamika na kulaumu, kwa
nini?

Kwa sababu huwezi!! Hili ndio jibu ambalo unajiridhisha nalo.
Kwamba siwezi kufanya tofauti, kila mtu ameshazoea vile nilivyo. Kwamba siwezi
kuweka muda zaidi kwenye kujifunza, kwa sababu nina mambo mengi ya kufanya.
Kwamba siwezi kuacha kuangalia tv kila siku, nitapitwa na mambo mengi. Kwamba
siwezi kuacha kukaa na jamaa zangu kila siku jioni tukipata moja moto na moja
baridi ili nifuatilie zaidi biashara na kazi zangu.

Kama haya ndio majibu yako, kwanza wewe mwenyewe unayaamini
kweli? Ni kweli kwamba huwezi kufanya mambo hayo ambayo yatabadili kabisa maisha
yako? Vipi kama maisha yako ndio yangekuwa yanategemea hivyo ndio uweze kuishi.
Kwa mfano unaambiwa kuchagua kuishi ila usiangalie tv au uangalie tv halafu
unakufa, ungechagua nini?

Najua ungechagua kutokuangalia tv, safi sana, una maamuzi
mazuri. Na ndio maana mimi siamini kwamba yale yote unayosema huwezi ni kwamba
huwezi kweli, bali ni kwamba hutaki tu kufanya.

Kwa hiyo mambo yote unayosema kwamba huwezi, ukweli ni kwamba
hutaki tu kufanya. Na kwa maana hii basi nakuomba kuanzia leo usiseme tena
SIWEZI, sema SITAKI.

Siku nyingine kabla hujaniambia huwezi hakikisha kwamba ukifanya
kitu hiko unakufa, vinginevyo ni sitaki.

TAMKO LA LEO;

Najua hakuna kitu kizuri na cha kubadili maisha yangu ambacho
siwezi kufanya. Vingi ninavyoona siwezi kufanya ni kwamba sitaki tu kufanya. Kwa
sababu kama maisha yangu yangekuwa yanategemea vitu hivyo ni lazima ningefanya.
Hakuna kinachonishinda kufanya, na kuanzia sasa nitaacha kutumia sababu hii
kwamba siwezi.

Tukutane kwenye ukurasa wa 191 kesho, Like page yangu ya
Coach
Makirita Amani
uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha
kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365
bonyeza hapa na uweke email.

Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo
maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya
facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya
email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na
KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata
utaratibu.

TUPO PAMOJA.