Katika ulimwengu tunaoishi sasa, kama utashindwa kufikia mafanikio unayotaka kwenye maisha yako basi umeamua wewe mwenyewe.
Kuna kauli moja maarufu ambayo imewahi kusemwa na tajiri namba moja duniani ndugu Bill Gates, alisema kwamba kuzaliwa masikini sio kosa lako, ila kufa masikini ni kosa lako. Nakubaliana naye kwa asilimia mia moja.
Kama unapata hisia zozote za kupingana na kauli hiyo, kwamba kwa wewe kuwa na maisha magumu au kushindwa kupata kile unachotaka ni sababu ya mtu au watu fulani na sio kosa lako, tafadhali sana ishia hapa, maana utakayoendelea kusoma hayatakufurahisha.
Sawa, sasa tumebaki na wale ambao tunajua ni nini tunafanya, turudi kwenye lengo letu sasa, kwamba kama utashindwa kufikia mafanikio, kama utakufa masikini ni umeamua kuchagua mwenyewe.
Labda tuseme kwamba hukubaliani lakini umetaka tu kusoma ujue ni kipi hasa tutazungumzia. Basi naomba unijibu swali hili, ukipanda mbegu za mahindi unavuna nini? Huhitaji cheti cha elimu yoyote kujibu swali hilo. Ukipanda mbegu za mahindi utavuna mahindi. Hakuna sayansi ya roketi hapo.
Sasa tuje kwenye mafanikio na kushindwa, ukitaka kufanikiwa unatakiwa kufanya nini? Na ukitaka kushindwa unatakiwa kufanya nini? Kama uko na mimi mpaka hapa utakuwa unajua wazo kwamba ukitaka kufanikiwa, FANYA MAMBO AMBAYO WATU WALIOFANIKIWA WANAFANYA. Na ukitaka kushindwa angalia walioshindwa wanafanya nini na wewe ufanye.
Najua hayo yote Makirita, ila sioni waliofanikiwa wa kuwaiga. Vizuri sana, basi una walioshindwa ambao wamekuzunguka. Angalia yale wanayofanya na usiyafanye kabisa. Yaani kama kuna kitu chochote ambacho mtu aliyeshindwa kwenye kazi au biashara au kwenye maisha kwa ujumla anapenda kukifanya acha kukifanya mara moja. Maana kwa kukifanya na wewe unakaribisha kushindwa.
Bado huamini kwamba kufa masikini ni chaguo lako mwenyewe? Weka maoni yako hapo chini.
TAMKO LA LEO;
Najua maisha ni kuchagua na kuwa na mafanikio au kuwa masikini ni kuchagua pia. Kuanzia leo nachagua kuwa na mafanikio. Na kama sina watu waliofanikiwa wa kuwaangalia wanafanya nini ili na mimi nifanye, basi nitaacha kufanya yale ambayo walioshindwa wanapenda kufanya. maana kwa kufanya kile ambacho walioshindwa wanafanya, najiandaa kushindwa pia.
Tukutane kwenye ukurasa wa 200 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.