Mara nyingi wafanyabiashara huwa tunakuwa na mipango mizuri sana ya mambo yanapokwenda vizuri. Na mipango yetu hii tumeiweka tukiamini kwamba mambo yatakwenda vizuri wakati wote. Lakini haya ni maisha, na kama ilivyo sheria ya maisha, hakuna kitu kilichonyooka, hata bara bara nzuri bado ina kona. Hivyo kuna wakati kwenye biashara yako mambo hayatakwenda vizuri. Swali ni je unafanya nini pale ambapo mambo hayaendi vizuri? Au unafanya nini pale mambo hayaendi kama ulivyopanga? Hiki ni kitu muhimu tutakachojadili kwa siku ya leo.
Mambo yanapokwenda vizuri utasikia kutoka kwa watu wachache sana. Hawa watakuwa ni wateja wako waaminifu ambao wanakuamini sana na wamekuwa pia wakiwaambia wengine kuhusiana na biashara yako na hata kuwashawishi waje kwenye biashara yako. Hawa watakuambia wazi kwamba biashara yako imekuwa msaada mkubwa kwao na maisha yao yamekuwa bora sana kwa sababu wametumia bidhaa au huduma unayotoa.
Mambo yanapokwenda vibaya kwenye biashara yako, utasikia kutoka kwa watu wengi sana. Utasikia malalamiko mengi kutoka kwa wateja ambao hawajawahi kukuambia chochote wakati mambo yanapokwenda vizuri. Na pia utasikia kutoka kwa washindani wako wa kibiashara ambao watatumia hali yako ya mambo kutokwenda vizuri kuwafanya wateja wasije kwenye biashara yako. Utasikia kutoka kwa watu ambao sio hata wateja wako na hawajawahi kukutana na biashara yako kwa njia yoyote ile. Ni asili ya binadamu kupenda kusambaza habari mbaya. Hivyo biashara yako inapokuwa inakutana na changamoto jua ya kwamba kuna watu wengi wanasubiri kusambaza changamoto hizo.
Ni kama ilivyo kwenye maisha kwamba unaweza kutenda mema tisa na ukafanya baya moja na watu wakasahau mema yote tisa na kukumbuka baya moja tu. Ndivyo biashara zilivyo pia, mambo yatakapokwenda vibaya, kila mtu atazungumza lake kila mtu atalalamika na pia utapoteza wateja ambao walikuwa wapo wapo tu.
SOMA; Uchambuzi wa kitabu THE INVESTMENT ANSWER.
Je unafanya nini ili kuondoka kwenye wakati huu mgumu kibiashara?
Mambo kuwa magumu kwenye biashara yako sio kwamba ndio mwisho wa biashara, ila kama wewe mwenyewe utakata tamaa na kukubali mambo yakuvuruge basi utatoa nafasi kwa biashara yako kufa.
Unahitaji mpango mzuri ambao utaiwezesha biashara yako kuvuka katika nyakati hizi ngumu. Kwa kukosa mpango huu utakuwa hatarini kuondolewa kwenye biashara hiyo kwa mambo ambayo ni ya kawaida tu. Yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu kwako wewe mfanyabiashara kufanya katika wakati ambao biashara yako inapitia wakati mgumu.
Kwanza kabisa jua ni kipi hasa kimekupelekea wewe na biashara yako kuingia kwenye matatizo ambayo upo kwa sasa. Kujua tatizo ni nusu ya kulitatua. Kabla hujataharuki na kufanya mambo kuwa mabaya zaidi kaa chini na utafakari mambo yamefikaje hapo yalipo sasa. Kwa kujua chanzo halisi cha tatizo itakuwezesha wewe kuchukua maamuzi sahihi ambayo yatasaidia biashara yako kuendelea kusimama. Kama utakimbilia kuchukua hatua kabla hujajua chanzo kamili unaweza kuongeza tatizo zaidi.
Pili hakikisha hatua yoyote unayofanya inaiwezesha biashara yako kuendelea kuwepo. Lengo lako kubwa kwenye wakati ambapo biashara inapitia matatizo ni kuhakikisha biashara yako inaendelea kuwepo. Kama tatizo ni kubwa saba unaweza kupata mawazo ya kuachana nayo. Ila kumbuka kwamba umekuwepo kwenye biashara hii kwa muda mrefu sasa na umewekeza nguvu nyingi. Hakikisha maamuzi unayofanya yataiwezesha biashara yako kuendelea kuwepo.
Tatu kubali kupoteza sehemu ya biashara yako. Jambo la tatu na muhimu sana kuzingatia, kubali kupoteza sehemu ya biashara yako. Huenda utapoteza baadhi ya wateja, huenda utapoteza sehemu ya mtaji na huenda utapoteza sehemu ya wafanyakazi. Kuwa tayari kwa yote haya ili uweze kuirudisha biashara yako kwenye msimamo mzuri.
Mambo kwenda vibaya kwenye biashara ni kitu ambacho kinaweza kutokea kwenye biashara yoyote. Inawezekana ni kupata hasara kubwa, inawezekana ni bidhaa au huduma yako kuleta matatizo kwa watu na pia inawezekana ni jina la biashara yako kuharibiwa kwa sababu ambazo zipo nje ya uwezo wako. Fanyia kazi mambo hayo matatu ili kuweza kuirejesha biashara yako na iende vizuri.
TUPO PAMOJA.