USHAURI; Kutoka Kwenye Kuajiriwa Mpaka Kujiajiri, Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kununua Uhuru Wako.

Kununua uhuru wa kazi na hata maisha, yaani kutoka kuwa mwajiriwa mpaka kujiajiri mwenyewe na hatimaye kuweza kuwaajiri wengine ni mpango wa watu wengi sana. Japo ni wachache sana wanaoweza kutimiza mpango huu kwa sababu sio kitu rahisi kufanya kama ilivyo rahisi kusema.
Unahitaji kudhamiria kweli, unahitaji kujitoa kweli na pia unahitaji kufanya tofauti sana na vile ulivyozoea kufanya au vile ambavyo kila mtu anafanya.
Leo katika kipengele hiki cha ushauri wa changamoto tutajadili changamoto ambazo zinawazuia watu wengi kuweza kununua uhuru wao na hatua gani za kuchukua ili uweze kununua uhuru wako.

HAKIKISHA UNASOMA KITABU HIKI, BONYEZA KUKIPATA

 
Kabla hatujaangalia ni kipi cha kufanya, naomba tupate maoni kutoka kwa msomaji mwenzetu ambaye anapitia changamoto hii. Na maoni ya leo ni marefu kidogo hivyo yasome kwa umakini ili tuweze kwenda vizuri.
Habari mkuu,
Mimi nafanya kazi na nina familia sasa majukumu yamekuwa mengi na kipato hakitoshi kabisa na nina plan ya kufanya biashara
sasa tatizo moja nina deni crdb nilikopa na kununua shamba kama heka mbili na pesa nyingine nilifanyia vitu vya ajabu nikajikuta imekwisha sasa kosa nimejifunza na sasa nahitaji kufanya biashara ili nije  kujenga nyumba yangu na niondokane na upangaji wa nyumba na nilikuwa na plan ya kujenga room mbili za kuishi ili niepuke kwanza upangaji wa nyumba halafu nikiwa hapo kwangu naweza kuendeleza kidogo kidogo. 
Sasa kuna saccos nimejiunga na inatoa mkopo kutokana na akiba uliyonayo ila mkopo wa kwanza hauzidi 3 milion nami nina mkopo bado crdb na ni wa miaka 4 yaani mpaka 2017 sasa nikaona bora niombe ushauri jinsi ya kufanya
nina jamaa yangu hapa mwanza na yeye ana duka na nilimwomba niweke m pesa, tigo pesa na airtel money ili nianze na biashara hiyo kidogo kidogo hapo dukani kwake kwa kumweka mtu wangu yaani namwajili mtu au mimi mwenyewe nakaa na pesa yangu na akija mteja wa kutaka kutuma au kutoa pesa nafanya kazi hiyo naongopa kumpatia pesa kwani si mwaminifu na pesa na pale kuna mzunguko mkubwa wa biashara hiyo.
Na plan nyingine ni kufuga kuku wa kienyeji ila sasa ili nifunge kuku wa kienyeji inabidi nihamie kwangu yaani kule nilikonunua shamba langu kwani hilo shamba nilienda halmashauri kwa dhumuni la kupima nipate viwanja na nikapewa gharama na mchoro pia na kuna viwanja kama 11 hivyo kichwa kinaniuma tena ni kupima eneo langu na kupata hivyo viwanja na kuviweka na plan ni kuja kuviuza kama 4 baadae baada ya miaka kama 3 nadhani bei itakuwa kubwa kwa eneo hilo hivyo kwa biashara ya kuku pale nitafanikiwa ila sasa lazima nijenge vyumba hata viwili vya kulala ili niwe hapo na kuanza plan hiyo
Plan nyingine ni kulima punga na kufanya biashara ya kununua na kuuuza mazao
sasa plan ya kuchukua mkopo na kufanya biashara ya mtandao yaani m pesa na tigo na airtel money ndiyo naona ina faida ambayo naweza kupata kila mwezi na kulipa kwanza deni hapo saccos halafu nikimaliza nabaki na mtaji wangu na naendeleleza kujenga na plan zingine pia 
ebu nipe ushauri kijana mwenzangu kwani na plan baada ya miaka mitatu niache kufanya kazi za watu niwe na kampuni yangu mwenyewe hivyo nipe mawazo nifanye lipi ili nisonge mbele nahitaji maisha mazuri ya kwangu na mke wangu na watoto wangu pia na mtoto wangu niwaachie maisha mazuri
wako 
F B
Kama umesoma kwa makini utaona msomaji mwenzetu ana mipango mingi sana lakini mipango yote hiyo anataka impelekee kuweza kuondoka kwenye ajira na kujiajiri mwenyewe na hatimaye kuwa na maisha mazuri kwake na kwa familia yake.
Karibu sasa tuangalie ni mambo gani muhimu ya kuzingatia ili uweze kutoka kwenye ajira mpaka kujiajiri na kuwa na maisha mazuri. Yote haya yataendana na changamoto za msomaji mwenzetu aliyetuandikia.
A. Umeshafanya makosa.
Kitu cha kwanza kabisa ambacho unatakiwa kukifahamu ni kwamba umeshafanya makosa. Na japo umekiri kwamba umefanya makosa sijui kama umejifunza kutokana na makosa hayo ili usije kuyarudia tena. Umetuambia kwamba ulichukua mkopo benki ukanunua shamba na hela nyingine ukafanyia vitu vya ajabu. Kimsingi ni kwamba mkopo wote uliochukua ulifanyia vitu vya ajabu.
Kuchukua mkopo ambao unaulipia riba na kwenda kununua shamba sio maamuzi sahihi, kama kweli unataka kufanikiwa. Chukua mkopo na ufanyie shughuli ya uzalishaji ili uweze kulipa deni na kupata faida zaidi ambayo itakuwezesha kuwa na fedha za kuweza kununua hivyo viwanja na vitu vingine muhimu unavyohitaji.
B. Achana na mipango ya kujenga kwa sasa.
Umeeleza vizuri sana kwamba unahitaji kujenga vyumba viwili tu ili uondokane na nyuma za kupanga. Unaweza kuona unafanya maamuzi sahihi sana lakini hapa unakwenda kupotea tena.
Kwanza kabisa unataka kujenga kwa kutumia mkopo, ambao unatakiwa kulipa kwa riba na wakati huo huo una mkopo mwingine, tafadhali sana acha kujiweka kwenye matatizo zaidi.
Pili ujenzi una gharama, hata kama ni vyumba viwili tu, kuna gharama nyingi sana ambazo huwezi kuzipigia mahesabu. Kwa kifupi kama umepanga kujenga nyumba ya milioni tano, unahitaji kuwa na fedha zaidi ya hiyo, angalau mara mbili yake. La sivyo utaishia njiani.
Tatu ujenzi unahitaji muda, utaanza kukimbizana na mafundi, mara sijui mtu w akumwagilia, mara mtu wa kufanya nini, haya yote yatazidi kuchukua muda wako na ushindwe kufanya mambo muhimu.
Hivyo kwa sasa futa kabisa mawazo ya kujenga, unakwenda kuzika hela ambazo sio hata za kwako.
SOMA; USHAURI; Usikimbilie Kujenga Kabla Hujawa Na Uhakika Wa Kipato.
C. Punguza mipango uliyonayo.
Una mipango mingi sana, usijidanganye, huwezi kuitekeleza yote, tena kwa wakati mmoja. Unataka kujenga, huku unataka kufanya biashara ya fedha, unataka kufanya biashara ya mazao na huku unafikiria kufuga. Huwezi kufanya vitu vyote hivi kwa wakati mmoja, hata kama utaanza na kimoja, inabidi usiendelee kufikiria vingine, maana vitakusumbua na kukufanya ushindwe kuzingatia kile ambacho umechagua kufanya.
Kujenga umeshaondoa kwenye mipango yako, tigo pesa na mpesa nazo utaziondoa, kwa sababu mbili ninazokupa hapo chini, kufuga nako unaondoa kwa sababu huna eneo.
D. Usifanye biashara na huyo rafiki yako.
Umesema kuna rafiki yako ambaye ana duka na unaweza kuweka huduma za fedha pale dukani kwake. Lakini pia umesema sio mwaminifu hivyo huwezi kumkabidhi pesa zako. Sasa hii ni sababu nzuri sana ya kutokufanya naye biashara kabisa. Mtu ambaye sio mwaminifu ni sio mwaminifu tu, hakuna njia yoyote unayoweza kutumia kumdhibiti hasa kwa hapa ambapo yeye ndio anakubeba wewe.
Kama hutaki matatizo zaidi epuka kujihusisha kibiashara na mtu huyu.
E. Biashara ya miamala ya fedha pekee haiwezi kukupa uhuru.
Moja ya mipango yako ni kuwa na biashara ya miamala ya fedha, yaani tigo pesa, mpesa na airtel money. napenda nikufahamishe kwamba biashara hii peke yake haiwezi kukupatia uhuru. Ndio zamani biashara hizi zililipa vizuri sana lakini kwa sasa mambo yamebadilika. Kamisheni sio nzuri tena kama zamani na biashara imekuwa inafanywa na watu wengi.
Kwa mawazo ya kuanza na mtaji kidogo hii sio biashara ya kutegemea, labda kama una biashara nyingine mama na hizi zikawa ni huduma nyingine zinazopatikana.
F. Kwa kuanzia, huna mpango wowote mpaka sasa.
Kwa haya tuliyojadili mpaka sasa ni kwamba huna mpango wowote ambao unaweza kukutoa hapo ulipo. Mambo mengi yanayokuumiza kichwa kwa sasa, yataendelea kukuumiza kichwa zaidi kama utaendelea kuyafikiria au utaamua kuyafanya. Hivyo sasa unahitaji kukaa chini na uje na mpango mwingine, huku ukiondoa kabisa mipango ya awali.
SOMA; USHAURI; Ni Biashara Gani Unaweza Kufanya Kwa Mtaji Mdogo Ulionao?
G. Ufanye nini sasa?
Kwa kuzingatia yote hayo ambayo tumejadili hapo juu naomba nikupe hatua za kufanya sasa ili kuweza kujiondoa hapo ulipo na kuwa na maisha bora.
Naomba nikupe angalizo kwamba hayo ninayokuambia yanahitaji muda, hivyo kama una haraka na unafikiri umeshachelewa hutaweza kuyafanya na mbaya zaidi utaendelea kuchelewa.
Hivyo kama upo tayari kuwa na maisha bora nakushauri ufanye mambo yafuatayo;
1. Endelea kufanya kazi uliyonayo sasa, kwa sababu una deni la miaka miwili ijayo, kazi hii itakusaidia kulilipa, hakuna biashara yoyote utakayoanzisha sasa itakuwezesha kulipa deni haraka na ikaendelea kuwepo.
2. Kaa chini na ufikirie biashara nyingine unayoweza kuifanya wakati unaendelea na kazi yako. Wakati huo unafikiria biashara hiyo, tenga fedha kidogo kwa ajili ya kuanzia biashara hiyo. Fedha hii utaweza kuipata kama utaondoa gharama ambazo sio za msingi kwenye maisha yako.
3. Anza biashara hiyo utakayoipata kwa fedha zako kidogo kabla hujaingia kwenye mkopo. Hii itakusaidia kuijua biashara na changamoto zake kabla hujaingia kwenye biashara na kupata hasara.
4. Jenga nidhamu kubwa sana ya fedha, kwa sasa sahau anasa au starehe ambazo umezoea kupata, unahitaji kujipanga na kufanya kazi kwa juhudi sana ili uweze kufikia lengo ulilojiwekea.
5. Unahitaji kujipa muda, kadiri unavyotamani kufanikiwa haraka ndivyo unavyoshawishika kujiingiza kwenye maamuzi ambayo yatakugharimu sana.
Fanyia kazi mambo hayo na kama utahitaji mwongozo zaidi tunaweza kuwasiliana.
Nakutakia kila la kheri katika safari hiyo ya kuboresha maisha yako, uweze kuondoka kwenye hali ngumu uliyonayo mpaka kuweza kufikia uhuru wa maisha yako. Hakuna ambacho kinashindikana, ila unahitaji kujitoa na kuweka juhudi kubwa.
TUPO PAMOJA
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: