Ngoja niende moja kwa moja, kama unataka kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako, basi achana na demokrasia. Ukiendekeza demokrasia na akili yako mwenyewe nakuhakikishia hutafika mbali.

Unajua kwa nini? Kwa sababu ukiipa akili yako nafasi ya kujieleza tu, umekwisha, utaisikiliza na mwishowe hutofanya. Unahitaji kuwa dikteta wa akili yako ndio utaweza kufanya jambo kubwa kwenye maisha yako.

Bado hujanielewa? Ngoja nikupe mfano mzuri.

Wakati naanza kujijengea tabia ya kuamka asubuhi na mapema(huwa naamka saa kumi asubuhi kila siku) haikuwa rahisi. Kuna siku ambazo alam ilikuwa inaita, naamka kabisa(kwa sababu alam huwa naweka mbali na kitanda) ila nikishaamka najishawishi kwa nini nirudi kulala. Akili inaanza kuniletea demokrasia zake, na hivi ndio vishawishi inakuja navyo…

Unajua jana ulilala umechoka sana, ni bora ukalale tena dakika tano tu…

Lakini leo ni jumapili, una muda wa kutosha wa kuandika baadae…

Sio mbaya ukilala leo siku moja tu, utalipiza huu muda uliolala kesho….

Nilikuwa nikisikiliza tu, narudi kulala, naamka saa moja na naanza kujisikia vibaya. Kwa nini nilikubali kulala tena.

Hivyo acha kabisa kutoa demokrasia kwa akili yako. Akili ni vivu, usiisikilize. Ukishaamua kwamba unafanya kitu, fanya hata kama kuna mawazo yanakujia kwamba umeshajaribu sana, au acha tu, au sio mbaya ukaishia hapa. Kataa mawazo hayo.

Usikubali kirahisi, komaa
Usikubali kirahisi, komaa

Kama ulipanga mwenyewe hakikisha unakamilisha ulichopanga. Usikubali demokrasia ya kusikiliza akili yako, itakurudisha nyuma.

Akili yako inaogopa maumivu, akili yako inaogopa kushindwa, akili yako inaogopa kukataliwa na akili yako inaogopa kuchekwa, kama utaisikiliza hutafanya chochote kinachopelekea matokeo hayo. Na ubaya ni kwamba huwezi kufanikiwa kama hutapata maumivu, kama hutashindwa, kama hutakataliwa na kama hutachekwa.

Kuwa dikteta, kwa akili yako, hii ni njia muhimu sana kwako kufikia mafanikio.

TAMKO LA LEO;

Najua akili yangu imekuwa inanidanganya sana na ndio maana nakata tamaa mapema au naishia njiani kwenye mambo mengi ninayofanya. Kuanzia leo nasema kwamba nimevunja demokrasia kati yangu mimi na akili yangu. Nitafuata kile nilichopanga kufanya hata kama akili italeta malalamiko yake. Nimeamua kuwa dikteta wa akili yangu ili niweze kuitumia vizuri inifikishe kwenye mafanikio makubwa.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.